Na Frank Mvungi- MAELEZO
Serikali imesema hakuna uhaba wa dawa ya usingizi katika Hospitali ya Rufaa
Bombo mkoani Tanga kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari
hapa nchini kuwa hali hiyo inachochea kuzorota kwa huduma za upasuaji.
Akifafanua suala hilo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt.
Asha Mahita amesema kuwa taarifa kuwa huduma za upasuaji katika
hosipitali hiyo zimesimama si za kweli na ukweli ni kwamba huduma
zinaendelea kama kawaida.
“Huduma
za upasuaji katika Hosipitali yetu zinaendelea kama kawaida na hakuna
tatizo kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari” Alisisitiza
Dkt. Mahita.
Akifafanua
zaidi Dkt. Mahita alisema kuna mgonjwa mmoja tu ambaye upasuaji wake
ulisogezwa mbele kutokana na sababu za kitabibu na si kwa sababu ya
kukosekana kwa dawa ya usingizi.
Aliongeza
kuwa sababu zinazoweza kusababisha kuahirishwa kwa upasuaji wa mgonjwa
aliye kwenye ratiba ni pamoja na uwepo wa wagonjwa wengi wa dharura hali
inayoweza kuchangia nguvu kubwa kuelekezwa katika kuhudumia wagonjwa
hao wakiwemo wahanga wa ajali.
Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kuwahudumia wananchi na
kuhakikisha kuna dawa za kutosha na vifaa tiba katika hospitali na vituo
vya kutolea huduma hapa nchini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: