TAMKO LA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KULAANI KUBAKWA NA KULAWITIWA KWA MTOTO KATIKA MANISPAA YA MIKINDANI, MKOANI MTWARA
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 7:43 AM
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesikitishwa na kukemea vikali tukio la mzazi kumbaka na kumlawiti mtoto wake wa kufikia mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu, kitendo kilichofanywa na John Donald (35) mkazi wa Kiyangu, Manispaa ya Mikindani mkoani Mtwara.
Tukio hili la kubaka na kulawitiwa ni ukatili wa hali ya juu dhidi ya mtoto maana husababisha maumivu makali ikiwa ni pamoja na kumdhuru mtoto kimwili, kisaikolojia, kijamii na kihisia. Aidha, vitendo hivi, vinaacha kovu la kudumu kimwilini, kiakili, kimaadili, kijamii, ulemavu, maumivu, na wakati mwingine husababisha kifo; jambo ambalo linahitaji ulinzi thabiti katika kuhakikisha watoto wanaishi mazingira salama na rafiki.
Ukatili alilofanyiwa mtoto eneo la Kinyangu, manispaa ya Mikindani, ni ukiukwaji mkubwa wa haki za mtoto ambao huchangia kurudisha nyuma ustawi na maendeleo ya Mtoto na ni kinyume cha Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.
Wizara inatoa pongezi kwa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara kwa kumkamata mtuhumiwa na kumfikisha mahakamani ili hatua za kisheria zichukuliwe. Vile vile, Wizara inaipongeza Mahakama ya Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es salaam dhidi ya Omary hamisi (25), mkazi wa Gongo la Mboto, Dar es salaam, ya kutumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka tisa mwenye ulemavu wa kusikia na kuongea. Uamuzi huu ni kielelezo kuwa, wananchi wakitoa ushahidi wa matukio ya ukatili dhidi ya watoto, watuhumiwa watachukuliwa hatua kali ili kuwa fundisho kwa wananchi wanaowanyanysa watoto.
Wizara inamwelekeza Afisa Ustawi wa Jamii na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Mtwara kuwasiliana na wadau wengine katika ngazi zote kuhakikisha mama na mtoto wanapata huduma ya afya na ushauri na kufuatilia mwenendo wa shauri hili.
Imetolewa na
Erasto Ching’oro
Msemaji wa Wizara
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: