TAASISI ZA SERIKALI WARUHUSUNI MAAFISA HABARI KUSHIRIKI KATIKA VIKAO VYA MAAMUZI- NNAUYE

PAZ1
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akisalimia wananchi wa Mkoa wa Katavi alipowasili katika mkoa huo jana kukutana na wadau wa sekta anazozisimamia pamoja na kutoa vitendea kazi kwa maafisa habari wa mkoa wa Katavi na kutembelea mitambo ya kurushia matangazo ya TBC. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Mpanda , Paza Mwamlima.
PAZ2
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akizungumza na watendaji wa Mkoa wa Katavi alipowasili katika ofisi za mkoa huo na badae kukutana na wadau wa sekta anazozisimamia pamoja na kutoa vitendea kazi kwa maafisa habari wa mkoa wa Katavi na kutembelea mitambo ya kurushia matangazo ya TBC.
PAZ3
Wadau wa sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mkoa wa Katavi wakimsikiliza Waziri mwenye dhamana na sekta hizo, Nape Nnauye (hayupo pichani) alipofanya kikao nao jana mkoani hapo na kuahidi kutatua baadhi ya kero zinazowakabili.
PAZ4
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akikagua iPad kabla ya kumkabidhi Mkuu wa wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima iPad nne kwa ajili ya maafisa habari waliopo katika Mkoa wa Katavi na Wilaya zake jana mkoani Katavi.
PAZ5
Mkuu wa wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima akifurahi na kumpa mkono Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo baada ya kupokea iPad nne kwa ajili ya maafisa habari waliopo katika Mkoa wa Katavi na Wilaya zake jana mkoani Katavi.
Picha na: Genofeva Matemu – Maelezo, Katavi
…………………………………………………………………………………………….
Na: Genofeva Matemu – Maelezo, Katavi
Tarehe: 05/04/2016
Taasisi za serikali zimetakiwa kuwashirikisha maafisa habari waliopo katika taasisi zao katika vikao vya maamuzi ili waweze kua na taarifa na kufahamu maamuzi ya michakato inayoendelea hivyo kupata nguvu na uelewa mzuri wa kwenda kueleza umma pale wanapotakiwa kutolea ufafanuzi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye wakati wa ziara yake jana katika Mkoa wa Katavi kukutana na wadau wa sekta anazozisimamia pamoja na kutoa vitendea kazi kwa maafisa habari wa Mkoa huo na kutembelea mitambo ya kurushia matangazo ya TBC.
 Nnauye amesema kuwa maafisa habari katika taasisi za serikali wamekuwa wakinyimwa nguvu ya kushiriki katika vikao vya taasisi hivyo kushindwa kutolea maamuzi masuala mbalimbali pale wanapohitajika katika vyombo vya habari.
Aidha, Nnauye amewataka waandishi wa habari kufanya kazi kwa kufuata sheria kanuni na taratibu kwani serikali inawajali na kuwathamini kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuelimisha jamii.
“Mswada wa sheria ya huduma wa vyombo vya habari umelinda maslahi ya waandishi wa habari na Sheria hii imebana vigezo ambapo kama itapita itasaidia kupambana na utitiri wa vyuo visivyokuwa na sifa pamoja na changamoto zingine zinazoikabili sekta hii” amesema, Nnauye.
Aidha, Nnauye amewaomba watu wa TCRA kusimamia vizuri maudhui ya Radio na Television kwa  kuwa wakali na kuacha kucheka na watu ambao wanaweza kutumia vibaya  mabadiliko ya sayansi na teknolojia kuwaga jamii yetu kidini, kikabila, kikanda na rangi kwa kufanya matangazo ya kuligawa taifa letu.
Naye mwandishi wa habari kutoka Clous FM Bw. Ezron Mahanga ameiomba serikali kuendelea kupambana kulinda maslahi ya waandishi wa habari kwa kuwasimamia kwa karibu ili wamiliki wa vyombo vya habari waache kuwatumia kwa maslahi yao binasfi bila kujali utu wa waandishi wa habari wanaofanya kazi katika mazingira magumu.

0 comments: