GUINEA CONAKRY YAIMARISHA USALAMA TAYARI KUKABILIANA NA SHAMBULIO LOLOTE LA KIGAIDI

Guinea Conakry yaimarisha usalama tayari kukabiliana na shambulio lolote la kigaidi
Serikali ya Guinea Conakry imechukua hatua za kuimarisha usalama nchini humo kwa shabaha ya kujiweka tayari kukabiliana na shambulio lolote lile la kigaidi.
Viongozi wa Guinea Conakry wametangaza kuwa, wameimarisha usalama katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo baada ya kutokea mashambulio ya kigaidi katika nchi za Mali, Burkina Fasso na Ivory Coast.
Kabele Camara, Waziri wa Usalama wa Guinea Conakry ametangaza kuwa, sambamba na hatua hizo za kuimarisha usalama, nchi hiyo itaunda kikosi maalumu cha kupambana na ugaidi.
Amesema kuwa, kikosi hicho maalumu kitakuwa tayari kukabiliana na tishio lolote lile la ugaidi.
Duru za usalama za serikali ya Guinea zinasema kuwa, kikosi hicho maalumu kitaundwa kutokana na kikosi cha polisi na jeshi na kwamba, jukumu lake kuu litakuwa ni kupambana na ugaidi.
Shambulio la katikati ya mwezi uliopita nchini Ivory Coast lilikuwa la tatu kubwa kufanywa na kundi la kigaidi la Al-Qaeda katika eneo la kaskazini mwa Afrika (AQIM) tangu mwezi Novemba, ingawa lilikuwa ni la kwanza nchini Ivory Coast likitanguliwa na mashambulizi yaliyofanywa katika nchi za Mali na Burkina Faso.
Mashambulio hayo ya kigaidi katika nchi za jirani, ndio yaliyowafanya viongozi wa Guinea Conakry waimarishe zaidi usalama katika nchi hiyo.

0 comments: