BASHIR WA SUDAN AKATAA KUGOMBEA TENA KITI CHA RAIS

Bashir wa Sudan akataa kugombea tena kiti cha rais
Rais Omar al-Bashir wa Sudan amesema kwamba hatagombea tena kiti cha rais wa nchi hiyo. Amesema ifakapo mwaka 2020 ataondoka madarakani na kumuachia mtu mwingine fursa ya kuiongoza nchi hiyo.
Mwaka 1989 Bashir akiwa angali ni kanali katika jeshi la Sudan, aliongoza mapinduzi ya kijeshi yasiyo ya umwagaji damu yaliyomuondoa madarakani Swadiq al-Mahdi, Waziri Mkuu wa wakati huo na hivyo kutwaa uongozi wa nchi. Licha ya kuwa aliimarisha nafasi yake hiyo kupitia chaguzi kuu zilizofanyika mwaka 2010 na 2015 lakini wapinzani wake wamekuwa wakitilia shaka uhalali wa chaguzi hizo. Vyama vya upinzani vilisusia uchaguzi wa bunge na rais uliofanyika mwaka jana nchini humo. Vyama hivyo vilichukua hatua hiyo kwa hoja kwamba hakukuwepo ushindani wa kiuadilifu kati ya al-Bashir na wagombea wenzake kutokana na kuwa, kinyume na walivyokuwa wao, rais huyo alikuwa na fursa ya kutumia mali ya umma na vyombo vya habari vya serikali kwa ajili ya kuendeshea kampeni zake za uchaguzi, alibadilisha katiba ya nchi kwa maslahi yake, kupewa fursa ya kuwateuwa wakuu wa mikao katika hali ambayo wanapaswa kuchaguliwa na wananchi na kuendelea mapigano katika majimbo ya Darfur, Jabal an-Nuba, Blue Nile pamoja na kutoruhusiwa uchaguzi kufanyika katika majimbo hayo. Wapinzani pia wanakosoa vikali kutokuwepo nchini mfumo mzuri wa mahakama huru zisizopendelea upande wowote. Majaji wa mahakama kuu ya mfumo huo unaodhibitiwa kikamilifu na serikali ya Rais Bashir wanaajiriwa na kufutwa kazi na kiongozi huyo. Wanachama wa Tume Kuu ya Uchaguzi pia wanachaguliwa na rais wa nchi. Kwa mtazamo wa wapinzani tangazo la Rais al-Bashir kuwa hatagombea tena kiti cha rais wa nchi hiyo si jingine bali ni ujanja na hadaa tu ya kisiasa. Inaonekana kuwa maneno hayo ya hivi karibuni ya Bashir yana lengo la kuzua mgongano na mgawanyiko katika kambi ya upinzani na hivyo kupunguza upinzani wa ndani dhidi ya serikali yake. Hivi sasa Wasudan wengi wanasema kuwa Bashir hafai tena kuiongoza nchi hiyo kutokana na kusakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Kushindwa serikali ya Khartoum kuboresha uchumi wa nchi ni sababu nyingine inayopunguza uungaji mkono wa wananchi kwake na kuzidisha upinzani dhidi yake. Viwanda vingi vya Sudan vimefilisika na deni la nje la nchi kuongezeka maradufu. Kuenea ufisadi mkubwa miongoni mwa viongozi wa serikali, kujitenga Sudan Kusini na hivi sasa kusikika uvumi wa kutaka kujitenga jimbo jingine la Darfur na ardhi ya Sudan yote hayo ni mambo yanayotumiwa na wapinzani wa serikali ya Khartoum kudai kuwa Bashir hafai tena kuiongoza nchi hiyo. Hali ya Sudan inakaribia kulipuka ambapo wapinzani ambao zamani walikuwa wakionekana tu katika maeneo ya mbali ya nchi hiyo sasa wanaonekana katika miji muhimu ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Khartoum pamoja na maeneo ya katikati mwa nchi. Licha ya kuwepo ukandamizaji mkubwa kutoka kwa vibaraka wa serikali kuu, lakini wananchi wengi wa nchi hiyo wanataka kuwepo marekebisho ya kidemokrasia nchini humo. Baadhi yao wanasema kuwa matamshi ya hivi karibuni ya al-Bashir yanahusiana na masuala mengine yaliyo nyuma ya pazia. Wanasema kuna uwezekano mkubwa kwamba matamshi hayo yanahusiana na maradhi na afya mbaya aliyonayo rais huyo na hivyo kumfanya asiweze tena kuendelea kuiongoza nchi.

0 comments: