WAZIRI WA AFYA AKAGUA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA KATIKA MAJIMBO YA MTWARA VIJIJINI, MASASI NA NDANDA

Ummy Mwalimu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu (wa pili kushoto) akiwasili katika hospitali ya Rufaa Ndanda Mission.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari wametembelea Hospitali ya Mji wa Masasi (Mkomaindo), Hospitali ya Rufaa Ndanda Mission na Kituo cha Afya cha Nanguruwe kilichopo Jimbo la Mtwara Vijijini.
Katika ziara hiyo ya siku 2 Mh. Ummy alipata fursa ya kukagua shughuli mbalimbali za sekta ya afya ikiwemo kukagua wodi za wagonjwa, maabara pamoja na kusikiliza kero mbalimbali kutoka kwa watumishi wa idara ya afya na wananchi katika utoaji wa huduma za afya katika maeneo hayo.
Mh. Ummy alisema kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe Dk. John Pombe Magufuli imejikita zaidi katika kuwahudumia wananchi hasa wa kipato cha chini kwa kuimarisha Nidhamu na Uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma. Pamoja na kusimamia Uwazi na matumizi bora ya rasilimali za Taifa.
Licha ya kukiri kuwa sekta ya Afya inakabiliwa na changamoto mbalimbali Mh. Ummy aliwapongeza na kuwashukuru madaktari na wauguzi kwa kazi na nzuri wanayoifanya ktk kutoa huduma kwa wananchi. Alieeleza kuwa Serikali inatambua na kuthamini kazi yao na imedhamiria kutatua changamoto zilizoko katika utoaji wa huduma ikiwemo kuongeza watumishi wa afya na kununua vifaa tiba na kuboresha mazingira ya kazi ya watumishi wa afya hasa walioko pembezoni.
Aliwaasa wananchi kuwathamini madaktari na waaguzi na iwapo kuna malalamiko dhidi ya watumishi hao basi wananchi wazingatie Sheria, Kanuni na Taratibu ktk kuonyesha malalamiko yao badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Alisema, Hata hivyo wapo watumishi wachache ambao wanafanya kazi kwa kutozingatia maadili ya kazi na viapo vyao, hivyo aliwataka wabadilike kwani Serikali ya awamu ya 5 haitamvumilia mtumishi yeyote anaejihusisha na vitendo vya rushwa na uzembe kazini.
Ummy Mwalimu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu akiongea na wananchi Ndanda mission.
Pia aliwaasa watumishi hao kujiepusha na mambo ambao yanaweza kuleta mgongano na hisia mbaya kwa wananchi. Mfano tuhuma dhidi ya mfamasia wa Wilaya kumiliki maduka matatu ya 3 ambapo mhe Waziri ameelekeza uchunguzi wa TAKUKURU ufanyike.
Katika Hospitali ya Mkomaindo, Mhe Ummy ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Masasi kwa mafanikio waliyopata ktk ukusanyaji wa mapato ambapo baada ya kufunga mfumo wa kukusanya mapato wa kielektronik mapato yao yameongezeka kutoka shs 500,000 hadi 1,500,000 kwa siku. Amezitaka Halmashauri zote nchini kuiga mfano wa hospitali ya Mkomaindo kwa sababu hatua hii itachangia sana kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi ikiwemo uwezo wa Halmashauri wa kununua dawa na vifaa tiba.
Katika Kituo cha Afya cha Nanguruwe Mh. Ummy aliihimiza Halmashauri kukamilisha ujenzi wa wodi mbili ili Kituo hicho kiweze kupandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya. Pia aliwataka kuongeza jitihada katika kuingiza wananchi/kaya nyingi katika Bima ya Afya kwani asilimia 5 wa waliojiunga ni ndogo sana.
Ummy Mwalimu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu akiongea na wananchi ili kujua kero zao katika ziara ya siku mbili mkoani humo.
Katika Hospitali ya Rufaa ya Mission Ndanda Mhe Ummy ameipongeza kwa kufanyia kazi agizo lake la wiki mbili zilizopita la kuzitaka hospitali za Taasisi za Dini zinazopokea ruzuku ya Serikali (Fedha na au Watumishi) kutekeleza kwa vitendo sera za Taifa za Serikali ikiwemo ya Matibabu Bure kwa Wajawazito, Watoto chini ya umri wa miaka 5 na Wazee. Hospitali ya Rufaa Ndanda imekubaliana na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kuanza utekelezaji wa jambo hili kuanzia Julai 1, 2016.
Mh. Ummy pia amepongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi na matibabu bure ya Ugonjwa wa Kifua kikuu hospitalini hapo ambapo alisema ni asilimia 10 tu ya vituo vya afya/Hospitali binafsi nchini zinazotoa huduma hizo licha ya Serikali kuwa tayari kuvipatia vifaa vya uchunguzi na dawa bure. Mhe Ummy amezitaka hospitali nyingine binafsi kuunga mkono jitihada za Serikali za kutokomeza ugonjwa wa Kifuu kikuu kama sehemu ya mchango wao kwa jamii.
Mhe Ummy pia ametembelea Chuo cha Maafisa Tabibu na Chuo cha uuguzi vilivyoko Masasi.
IMG-20160331-WA0025
Waziri Ummy akiongea na wagonjwa aliowakuta wakisubiri huduma katika hospitali ya Mkomaindo Masasi.
Mohammed Bakari
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari akizungumza na Watumishi wa Afya Ndanda Mission katika ziara aliyoambatana na Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu.
Mohammed Bakari
IMG-20160331-WA0023Baadhi ya watumishi wa afya wakimsikiliza kwa makini Waziri wa afya Mh.Ummy Mwalimu (hayupo pichani) wakati ziara yake tar 30 Machi.
Ummy Mwalimu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu akizungumza na mmoja wa wakinamama aliyelazwa kwenye wodi ya wazazi alipokua akikagua maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo.
Mussa Rashid
Kaimu Mganga mkuu Halmashauri ya mji wa Masasi DK. Mussa Rashid akitoa taarifa kwa Waziri wa afya alipotembelea chumba cha vipimo katika hospitali hiyo. Kulia ni Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammed Bakari.
Ummy Mwalimu
Waziri Mh. Ummy Mwalimu akibadilisha mawazo na Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Bernard Nduta. Kulia Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Rufaa Ndanda, Fr. Silvanus Kessy.

0 comments: