Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto) akizungumza na
wauza nguo wa Soko Kuu la mjini Chake Chake, Pemba. Wananchi hao
walikuwa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida bila wasiwasi wowote.
Waziri Kitwanga pia alisikiliza maoni ya wananchi hao kuhusu uchaguzi
mkuu na kuridhishwa na juhudi za kuimarisha ulinzi katika kisiwa hicho.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (wa pili kulia) akitembea
mitaani eneo la Chake Chake Pemba, Zanzibar kusikiliza maoni ya wananchi
kuhusu usalama wao katika kipindi cha uchaguzi kisiwani humo. Waziri
Kitwanga ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid
Abdullah (kulia), Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman
(wapili kushoto aliyevaa kaunda suti) na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kusini
Pemba, Ahmed Khalid Abdulla (kushoto, aliyevaa tai. Kitwanga
aliridhishwa na juhudi za kuimarisha ulinzi katika kisiwa hicho.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akizungumza na waandishi wa
habari (hawapo pichani) mara baada ya kuuzunguka msitu wa Taifa wa
Ngezi, uliopo Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba ambao baadhi
ya watu wasioitakia mema Zanzibar walisambaza taarifa za uongo kuwa kuna
wakimbizi wamejificha katika msitu huo baada ya kukimbia vurugu
kisiwani humo. Hata hivyo hakuna mkimbizi yeyote aliyekuwepo katika
msitu huo na wananchi wapo katika makazi yao wakiendelea na shughuli zao
za kujitafutia kipato. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba,
Omari Khamis Othman. Kulia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini
Pemba, Hassan Nasri.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (katikati) akizungumza na
wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, mjini Chake Chake, Pemba, kuhusu
masuala mbalimbali ya uimarishaji ulinzi katika kipindi cha uchaguzi
unaotarajiwa kufanyika Machi 20, 2016. Kushoto meza kuu ni Mkuu wa Mkoa
wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdullah na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akimuuliza swali Mkazi wa
Wawi, Chake Chake Pemba, bibi Zabibu Mohamedi, wakati Waziri huyo
alipokuwa anatembea mitaani kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu uchaguzi
unaotarajiwa kufanyika Machi 20, 2016. Hata hivyo wananchi hao
walimuahkikishia kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika siku hiyo ya
uchaguzi. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omari Khamis Othman.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga akiwahoji wafanyakazi wa
Bandari Kuu ya Pemba kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Machi
20, 2016. Wafanyakazi hao walimuhakikishia kushiriki kikamilifu katika
uchaguzi huo na pia wananchi hao wapo salama na wanaendelea na shughuli
zao zakujipatia kipato za kila siku.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kulia) akiwauliza maswali
wananchi wa mjini Chake Chake, Pemba kuhusu jinsi walivyojiandaa na
uchaguzi wa Machi 20, 2016 na kutoa maoni yao kama kuna tatizo lolote.
Hata hivyo wananchi hao walimuambia Waziri Kitwanga wanaendelea na
shughuli zao kama kawaida, hakuna vitisho vyovyote katika eneo
lao. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
…………………………………………
Na Felix Mwagara wa MOHA
WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amewataka wananchi wa
Zanzibar waondoe hofu kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu visiwani humo.
Akizungumza mara baada ya kufanya mazungumzo na wananchi hao wakati
alipokuwa anatembelea mitaa mbalimbali ya Soko Kuu la mjini Chake Chake,
Pemba aliwataka wananchi hao waendelee na shughuli zao za kujipatia
kipato kama kawaida na hakuna mtu atakayewabughudhi kwani ulinzi
umeimarishwa, na waachane na uzushi wa kutokea vurugu unaoenezwa
visiwani humo.
Waziri
Kitwanga alianza matembezi hayo mitaani mara baada ya kufanya
mazungumzo na Kamati ya Ulinzi na Usalama mjini Chake Chake ambapo
walimuhakikishia kuwa, Pemba yote ni salama na ulinzi umeimarishwa na
hakuna atakaye fanyiwa vurugu kwa mtu yeyote atakayefuata sheria.
Waziri
Kitwanga aliwataka wananchi hao kuondoa hofu wanapowaona askari
mbalimbali wakipita mitaani kwani wapo kwa ajili ya kuwalinda wananchi
hao pamoja na mali zao katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi
unaotarajiwa kufanyika Machi 20 mwaka huu.
“Musiwaogope
askari, na wala msiwe na wasiwasi, mnapowaona shangilieni kwani askari
ndio msaada wako kwa ajili ya usalama wako endapo inapotokea vurugu ya
aina yoyote, mtaenda kupiga kura salama na mtarudi salama, hakuna mtu wa
kuwabughudhi, msitishwe na mtu yeyote,” alisema Waziri Kitwanga na
kufafanua;“Leo nazunguka mitaa mbalimbali ya hapa Pemba, lengo ni
kuchukua maoni yenu pamoja na kuwaondolea hofu wananchi na
kuwahakikishia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimejipanga vizuri kwa
ajili ya kulinda usalama, hivyo jitokezeni kwa wingi siku ya uchaguzi
mkapigie kura kiongozi mnaemtaka.”
Hata
hivyo, Waziri Kitwanga alifanya ziara Mkoa wa Kaskazini Pemba katika
msitu wa Ngezi unaodaiwa kuwa kuna baadhi ya wakimbizi wamejificha
katika msitu huo ili kuokoa maisha yao baada ya kudaiwa kuwa kutatokea
na vurugu. Kitwanga akiongozana na Wakuu wa Mikoa ya Kusini Pemba na
Kaskazini Pemba pamoja na maafisa wa Jeshi la Polisi Pemba, walienda
katika msitu huo na kuukagua na hawakukutana na mtu hata mmoja
aliyejificha msituni humo kama inavyodaiwa na kusambazwa habari na
baadhi ya watu wasioitakia mema Zanzibar.
“Ndugu
waandishi wa habari, tumezunguka kwa pamoja kuungalia msitu huu,
kuwatafuta hao wakimbizi, hatujamuona mtu yeyote, ukisikia propaganda
ndio hii, watu hawaitakii mema Zanzibar na Tanzania kiujumla, mmeona
kuwa habari hii ni ya uongo, hakuna mkimbizi yeyote katika msitu huu
kama tulivyoshuhudia wote kwa ujumla,” alisema Kiwanga.
Aliongeza
kuwa, baadhi ya wananchi ambao wana mipango yao binafsi wanawatia hofu
wananchi kwa kutunga habari za uongo kuwa Zanzibar imechafuka, wakati
habari hizo hazina uhalisia wowote.
Hata hivyo, wananchi wa Pemba
walimuhakikishia Waziri Kitwanga wanafanya shughuli zao za kuwapatia
kipato kama kawaida na pia siku ya uchaguzi wataenda kupiga kura kama
kawaida kwani wanaamini amani itakuwepo kama ilivyokuwa sasa.
Waziri
Kitwanga alifanya ziara Zanzibar katika Kisiwa cha Unguja na kuzungumza
na Maafisa wa Jeshi la Polisi na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama,
na baadae kumalizia ziara yake kwa kutembelea katika mikoa yote ya
Pemba ikiwa ni hatua ya kuangalia hali ya usalama visiwani humo katika
kipindi hiki cha uchaguzi mkuu katika maeneo hayo.
0 comments: