Huku ulimwengu ukiwa bado haujasahau vifo vya kutisha vya maelfu ya
mahujaji wa nyumba ya Mwenyezi Mungu nchini Saudia, wafanya umra wapatao
19, wamepoteza maisha katika ajali nyingine mbaya ya basi nchini humo.
Kwa mujibu wa duru za habari nchini Saudia, wafanya ziara hao
raia wa Misri wamefariki dunia baada ya basi walilokuwa wakisafiria
kupinduka. Basi hilo ambalo lilikuwa limebeba wafanya umra wapatao 44
wote kutoka Misri wakiwamo watoto wawili, lilipata ajali kati ya mji
mtukufu wa Makkah na Madina. Watu wengine 22 wamejeruhiwa baadhi yao
wakiwa na hali mbaya. Chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana, ingawa
ripoti za awali zinaeleza kuwa ni dereva kuzidiwa na usingizi. Hisham al
Naqib, mmoja wa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje nchini Misri
amenukuliwa akisema kuwa, miili ya wahanga wa ajali hiyo iko hospitalini
mjini Madina. Kwa upande wake, Nawaf al-Muhammad, mkuu wa idara ya
usafirishaji ya mjini Madina amesema kuwa, kuna uwezekano mkubwa kwamba
dereva alizidiwa na usingizi. Hii ni katika hali ambayo Ijumaa
iliyopita, wafanya ziara 14 raia wa Palestina walifariki dunia katika
ajali nyingine ya barabarani mjini Makka, Saudia. Vifo hivyo vinatokea
katika hali ambayo hadi sasa ulimwengu wa Kiislamu unaendelea
kuilalamikia Saudia juu ya uzembe wake katika kusimamia ibada ya Hija na
kuitaka Riyadh ikabidhi jukumu hilo kwa nchi za Kiislamu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: