SERIKALI YA CONGO BRAZZAVILLE YATAKA MASHIRIKA YA SIMU KUKATA MAWASILIANO WAKATI WA UCHAGUZI HAPO KESHO

Serikali ya Congo Brazzaville yayataka mashirika ya simu kukata mawasiliano wakati wa uchaguzi hapo kesho
Serikali ya Jamhuri ya Congo Brazzaville imeyataka mashirika mawili makubwa ya simu nchini humo kukata mawasiliano yote wakati wa kufanyika uchaguzi wa Rais hapo kesho.
Taarifa ya serikali ya Congo Brazzavile imeeleza kuwa, imeyataka mashirika mawili makubwa ya simu ya MTN Congo na Airtel Congo kukata mawasiliano yote ya simu hapo kesho wakati wa kufanyika zoezi la uchaguzi wa Rais na vilevile siku ya Jumatatu. Kwa mujibu wa serikali hatua hiyo imechukuliwa kwa sababu za kiusalama.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Congo Brazzavile ameziambia duru za habari kwamba, uamuzi huo wa kutaka kukatwa mawasiliano ya simu umechukuliwa kutokana na sababu za kiusalama.
Rais wa nchi hiyo Denis Sassou Nguesso anawania tena kiti hicho kwa mara ya tatu na ametangaza kuwa ana matumaini makubwa ya kushinda licha ya wapinzani wake kusema anaona ndoto za mchana. Wapinzani wa serikali ya Brazaville wanasema kuwa, hatua ya kiongozi huyo ya kugombea kiti hicho kwa mara ya tatu mfululizo inakiuka katiba ya Jamhuri ya Congo Brazzaville.
Rais Nguesso ambaye ameingoza nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 30, Oktoba mwaka jana alibadilisha katiba na kuondoa kipengee kinachoweka ukomo wa vipindi viwili kwa Rais na kujiandalia mazingira ya kubakia madarakani.

0 comments: