KUTIMIA MWAKA MMOJA WA MASHAMBULIO YA KIVAMIZI YA SAUDIA ARABIA DHIDI YA YEMEN

Kutimia mwaka mmoja wa mashambulio ya kivamizi ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen
Jumamosi ya jana tarehe 26 Machi ilisadifiana na kutimia mwaka mmoja tangu Saudi Arabia ilipochukua uamuzi wa kuivamia na kuishambulia kijeshi nchi ya Yemen.
Abdul Malik al-Houthi, Kiongozi wa Harakati ya Wananchi ya Ansarullah ya Yemen amesema kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja wa uvamizi wa Saudia dhidi ya Yemen kwamba, vita na uvamizi huo ulianza na unaendelea kwa ridhaa ya Marekani na uungaji mkono wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Sambamba na kutimia mwaka mmoja wa uvamizi wa kijeshi wa utawala wa ukoo wa Aal-Saud na washirika wake, Abdul Malik al-Houthi amesisitiza kuwa, Saudia haikuheshimu haki ya ujirani mwema na Yemen na kumshambulia bila haki jirani yake huyo. Aidha al-Houthi amesema, Saudia ikiwa na uungaji mkono kamili wa Marekani, Uingereza, Israel na mamluki wake iliishambulia Yemen ili kuurejesha madarakani utawala wa kidiktea, lakini kuwa macho wananchi wa Yemen na vikosi vya Yemen kumesambaratisha njama hiyo. Hii ni katika hali ambayo, katika mashambulio hayo ya mwaka mmoja ya Saudia dhidi ya Yemen, wavamizi wakitumia silaha zilizopigwa marufuku wamefanya mauaji ya kinyama dhidi ya raia. Katika mashambulio ya anga ya majeshi ya Saudia na mamluki wake dhidi ya makazi ya raia, wahusika wamekuwa wakilenga hospitali, shule, bandari, barabara, taasisi, vyombo vya usafiri na uchukuzi, majengo ya serikali, vituo vya umeme na hata makaburi na hivyo kufanya uharibifu mkubwa. Ripoti kutoka Yemen zinasema kuwa, miundo mbinu ya nchi hiyo imeharibiwa vibaya na kuyafanya maisha ya wananchi kuwa magumu kila siku iendayo kwa Mungu. Hivi karibuni Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch na asasi nyingine saba zilitoa ripoti ya pamoja ambayo mbali na kuashiria jinai za kivita huko Yemen ilitaka Saudia iwekewe vikwazo vya silaha. Aidha mtandao wa Intaneti wa Foreign Policy umeashiria kutimia mwaka mmoja wa vita vya Saudia huko nchini Yemen na kuandika: Vipi Marekani, Uingereza na Ufaransa zinaendelea kuitumia silaha Saudia katika hali ambayo marubani wa ndege za kijeshi za Riyadh wamekuwa wakiwadondoshea mabomu raia wasio na hatia wa nchi hiyo? Mwaka mmoja wa mashambulio ya Saudia dhidi ya Yemen unatimia katika hali ambayo, asilimia 83 a wananchi wa nchi hiyo wanategemea misaada ya kibinadamu. Hii ni katika hali ambayo, mazungumzo ya amani ya Yemen yanatarajiwa kufanyika tarehe 18 ya mwezi ujao huko Kuwait. Baada ya mwaka mmoja wa vita huko Yemen, Wasaudia wanatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Harakati ya Ansarullah na kujadili namna ya kuhitimisha vita hivyo.
Tangazo la utayarifu wa Saudia la kushiriki mazungumzo ni sawa na kuikubali Harakati ya Wananchi ya Ansarullah kuwa ni upande wenye taathira katika matukio ya Yemen. Aidha hatua hiyo ni ithbati ya kukiri Wasaudia kushindwa katika vita huko Yemen na kusimama kidete muqawama wa wananchi dhidi ya wavamizi.

0 comments: