IRAN NA PAKISTAN KUIMARISHWA USHIRIKIANO DHIDI YA UGAIDI

Iran na Pakistan kuimarisha ushirikiano dhidi ya ugaidi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa ushirikiano kati ya Tehran na Islamabad katika nyuga mbalimbali hususan katika vita dhidi ya ugaidi.
Akihutubia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Pakistan, Islamabad, Rais Hassan Rouhani alisema nchi mbili hizo zimeafikiana kushirikiana katika kuzima harakati za makundi ya kigaidi yanayotishia usalama katika mipaka ya nchi hizo; mashariki mwa Iran na magharibi mwa Pakistan. Rais Rouhani ameongeza kuwa uhusiano wa Iran na Pakistan ni muhimu na kusisitiza kuwa, nchi mbili hizo zina mambo mengi yanayoziunganisha pamoja, yakiwemo ya kidini, kihistoria na kiutamaduni.
Kwa upande Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif amesema taifa lake linajivunia uhusiano mzuri na wa muda mrefu na Iran na kwamba, mkutano kama huu wa Islamabad ni wa tatu katika kipindi cha miaka zisizozidi mitatu.
Ameashiria kuwa kikao chake na Rais Rouhani mjini Islamabad kimegusia masuala mbali mbali yakiwemo ya kieneo na kwamba pande mbili hizo zimesaini makubaliano kadhaa katika nyuga tofauti kama vile ya kibiashara, sekta ya uchukuzi na nishati.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Waziri Mkuu wa Pakistan aliitembelea Iran Januari 19 mwaka huu.
Wakati tunaenda mitamboni, Rais wa Iran na Waziri Mkuu wa Pakistan walikuwa wanahutubia mkutano wa kibiashara mjini Islamabad.

0 comments: