CHADEMA WASHINDA UMEYA DAR

Na Anitha Jonas – MAELEZO
Tarehe 22/03/2016
Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Jiji la Dar es Salaam Bi. Sara Yohana amemtanganza Mhe. Isaya Chacha Diwani wa Kata ya Vijibweni (CHADEMA) kutoka Manispaa ya Temeke kuwa Meya Mpya wa Jiji hilo.
Kaimu Mkurugenzi huyo alimtangaza Isaya kuwa mshindi mara baada ya uchaguzi huo kufanyika leo  jijini Dar es Salaam ambapo mshindi alipata kwa kura 84 dhidi ya mgombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bw.Yenga Yusuph ambaye alipata kura 67 wakati kura 7 ziliharibika katika uchaguzi huo.
 “Tunawashuruku wapiga kura wote mlioshiriki zoezi hili la upigaji kura kwa utulivu bila vurugu na kuweza kufanikisha mpaka kumpata Meya wa Jiji hili” alisema Bi Yohana.
Kwa upande wa mshindi wa Kiti cha Meya wa Jiji Mhe. Chacha aliwashukuru wapiga kura wake wa kata ya Vijibweni kwa kumchagua kuwa Diwani pamoja uongozi wa chama chake kukubali kumpa nafasi ya kugombea kiti hicho.
“Nimejipanga kuleta maendeleo katika sekta ya elimu pamoja na kupambana na kero ya foleni katika jiji letu na nitahakikisha wananchi wote maskini wanafaidika  na mapato ya jiji hili ikiwemo kuendeleza miundombinu mbalimbali ,”alisema Chacha.
Aidha, Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Bw.Freeman Mbowe alisema idadi ya wapiga kura tu inaonyesha wazi kuwa ushindi wa kiti hicho cha Meya ni lazima uchukuliwe na  CHADEMA sababu  madiwani wengi wa Mkoa wa Dar es Salaam wanatoka katika chama hicho.

0 comments: