MTIZAMO NA MAWAZO HURU YA MDAU


*
Wananchi hawaoni kama wanao uwezo wa kuishawishi Serikali
*Wengi wanafuata njia zisizo rasmi za kufanikisha mambo yao wenyewe

Wananchi walio wengi (70%) wanaripoti kuwa sauti zao hazisikiki katika maamuzi ya Serikali. Pamoja na haya, wananchi saba kati ya kumi (71%) wanaripoti kuwa, kwa maoni yao, upigaji kura ndio njia pekee ya kuleta ushawishi kwa Serikali. Kimsingi, haya yanaonesha hisia zilizofanana – kwamba mbali na uchaguzi unaofanywa wakati wa kupiga kura – wananchi wengi hawana ushawishi kwenye maamuzi ya Serikali au shughuli zake. Wananchi pia wanaonekana kuwa na imani ndogo na taasisi rasmi au maafisa wa Serikali za mitaa katika kushughulikia masuala yao: wananchi tisa kati ya kumi wakiwa wameripoti kuwa hawajawahi kuzungumza au kuwasiliana na mbunge wao ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita. Pia, wananchi (47%) waliripoti kutowahi kuzungumza na mwenyekiti wao wa mtaa/kijiji ili kujadili masuala yanayowahusu. Ni mwananchi mmoja tu kati ya saba (16%) aliye mwanachama wa chama cha siasa.


Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Wananchi wana uchu wa mabadiliko: Je, wananchi wanashiriki na wanaweza kuiwajibisha serikali? Muhtasari umetokana na takwimu ya Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu za mkononi kote Tanzania Bara.
Licha ya mwingiliano mdogo ulio wazi kati ya wananchi na mifumo rasmi ya serikali, wananchi 6 kati ya 10 (58%) wanaripoti kuwa wamewahi kushuhudia wananchi wakipeleka malalamiko kwa viongozi ndani ya kipindi cha miezi 12 iliyopita. Malalamiko haya kwa kawaida huandaliwa ili kudai maboresho kwenye huduma za umma katika ngazi za mitaa. Masuala yaliyoonekana kulalamikiwa sana yalikuwa ni pamoja na utoro wa walimu na upatikanaji haba wa maji safi na salama.
Linapokuja suala la kuibua na kuzungumzia masuala yanayoihusu jamii, Sauti za Wananchi ilibaini kuwa watu walijitahidi kuzungumzia matatizo yaliyowakabili. Wananchi nane kati ya kumi (84%) walizungumzia masuala yao walipokutana katika makundi. Wananchi wengine watatu kati ya kumi walipiga simu kwenye vipindi vya redio 32% na 31% walilalamika kwa marafiki zao. Katika kuchukua hatua za kuungana pamoja na kusimamia jambo, wananchi walionekana kuwa wenye uwezo mdogo wa kususia mijadala. Ni 9% tu walioripoti kuwa wameshawahi kususia mijadala ndani ya kipindi cha mwaka uliopita, 8% walishiriki maandamano, 6% waliokataa kulipa kodi na waliotumia nguvu kufanikisha suala la kisiasa  walikuwa (1%).

0 comments: