ZOEZI LA KUMTAFUTA MSHINDI WA TUZO YA RAIS YA HUDUMA ZA JAMII KUANZA KESHO

Picha  Na 2
Mkurugenzi wa Taasisi ya Uunganishaji na Shirikishi Wadau katika Tasnia ya Uziduaji (Extractive InterStakeholders Forum, EISF) Bi. Catherine Lyombe akielezea jinsi zoezi la kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji (Presidential Award on Corporate Responsibility and Empowerment –CSRE in Extractive Industry) litakavyoendeshwa katika kikao hicho

Picha Na 1
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Ngosi Mwihava akizungumza na jopo la majaji na sekretarieti inayotarajia kuanza kazi ya kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji (Presidential Award on Corporate Responsibility and Empowerment –CSRE in Extractive Industry)
Picha Na 3
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Ngosi Mwihava akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho.
……………………………………………………………………….
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Jopo la majaji lililoundwa kwa ajili ya kumtafuta mshindi wa tuzo ya Rais ya huduma za jamii na uwezeshaji katika miradi ya madini, gesi na mafuta linatarajia kuanza kazi yake kesho, imeelezwa.
Akizungumza katika kikao na majaji watakaoshiriki katika zoezi hilo kilichofanyika kwenye ofisi za Wizara ya Nishati na Madini Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Ngosi Mwihava amesema kuwa kazi hiyo inayotarajiwa kukamilika Septemba 24, 2014 itahusisha mikoa yote ambayo miradi ya madini, gesi na mafuta inaendesha shughuli zake.
Mhandisi Mwihava alisema lengo la zoezi hilo ni kushindanisha makampuni yanayoendesha shughuli za madini, mafuta na gesi katika utoaji wa huduma bora kwa jamii.
Alieleza kuwa mara baada ya jopo la majaji kumaliza kazi yake, litawasilisha ripoti kamili ya zoezi hilo ambayo itadurusiwa kabla ya kukabidhiwa rasmi kwa ajili ya maandalizi ya halfa ya utoaji tuzo inayotarajiwa kufanyika mapema Novemba mwaka huu.
“Tanzania imewaamini katika kazi hiyo, hivyo ni imani yangu kubwa mtatumia utaalamu na uzoefu wenu katika zoezi hilo pasipo kupendelea kampuni yoyote. “ Alisisitiza Mhandisi Mwihava.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Uunganishaji na Shirikishi Wadau katika Tasnia ya Uziduaji (Extractive InterStakeholders Forum, EISF) Bi. Catherine Lyombe aliainisha maeneo yatakayoangaliwa kama mchango wa makampuni yanayoendesha shughuli za madini, gesi na mafuta kuwa ni pamoja na elimu, maji, afya, ajira na miundombinu.
Akielezea zoezi litakavyofanyika Bi. Lyombe alieleza kuwa majaji watatembelea maeneo yote yenye makampuni yanayoendesha shughuli za madini, gesi na mafuta na kuzungumza na wahusika pamoja na kuzungumza na wananchi ili kupata picha kamili ya mchango wa makampuni husika kwa jamii
Bi. Lyombe alisisitiza kuwa mbali na kupata taarifa kutoka katika makampuni na maelezo kutoka kwa wananchi kama wataalamu watafanya ulinganisho wa maelezo yanayotolewa na wananchi na tathmini halisi ya utekelezaji wa miradi iliyotekelezwa na kampuni husika.
Aliongeza kuwa lengo la utoaji wa tuzo hizo ni mkakati wa kuhamasisha makampuni ya madini, mafuta na gesi kuboresha huduma zake kwa jamii.
“ Mshindi wa tuzo ya Rais ya huduma za jamii na uwezeshaji katika miradi ya madini, mafuta na gesi anapopatikana, anatia hamasa kwa makampuni mengine kuboresha huduma zake na wananchi kuendelea kunufaika na uwepo wa makampuni hayo” alisisitiza Bi. Lyombe.
Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji (Presidential Award on Corporate Responsibility and Empowerment –CSRE in Extractive Industry) katika miradi ya madini, gesi na mafuta ilizinduliwa mwaka 2012 na Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kama mkakati wa kuhamasisha makampuni ya madini, gesi na mafuta kuboresha huduma zake kwa jamii hususan katika maeneo ya elimu, maji, miundombinu, ajira na afya.

0 comments: