Posted by
khamisimussa77@gmail.com
at
12:01 PM
Makamu wa kwanza wa Rais. Maalim Seif Sharif Hamad akiwasalimia maafisa wa Polisi Makao Makuu ya Polisi Zanzibar
Makamu
wa kwanza wa Rais. Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya
pamoja na Maafisa wa Polisi Ziwani alipofika kuwatembelea.
Na Khamis Haji, OMKR
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ametoa
wito kwa Jeshi la Polisi Zanzibar kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia
maadili ya kazi na kuhakikisha askari hawafanyi kazi kwa misingi ya
upendeleo, chuki, rushwa, wala ubaguzi wa aina yoyote.
Maalim
Seif ameyasema hayo leo wakati alipotembelea Makao Makuu wa Polisi
Zanzibar Ziwani, na kuzungumza na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan
Makame pamoja na maafisa wa Jeshi hilo.
Makamu
wa Kwanza amesema kwa kiasi kikubwa Polisi Zanzibar limepata mafanikio
makubwa katika kusimamia majukumu yake, hasa ya kupunguza matendo ya
uhalifu, lakini wapo miongoni mwa askari hujihusisha na matendo yaliyo
kinyume cha maadili yanayolitia doa jeshi hilo.
Alisema
zipo taarifa kwamba baadhi ya Maafisa wa polisi huvujisha taarifa na
kuwapa watuhumiwa wa dawa za kulevya, pale jeshi hilo linapojiandaa
kuwakamata na kuwafikisha mbele ya sheria.
Maalim
Seif amesema tabia hiyo haina budi kukomeshwa kwa nguvu zote kwa sababu
hudhorotesha mikakati ya kukomesha uingizwaji na biashara ya dawa za
kulevya katika visiwa vya Zanzibar.
Makamu
wa Kwanza wa Rais amesema dawa za kulevya zinasababisha madhara makubwa
kwa wananchi hasa vijana, na Polisi wanatakiwa kuwa mstari wa mbele
katika kudhibiti uingizwaji wake kwa kushirikiana na taasisi za Kitaifa
na Kimataifa.
“Nasikia
baadhi ya wakati taarifa huvujishwa na maafisa wa Polisi. Kitengo cha
Polizi cha Dawa za Kulevya lazima kiwe na watu waaminifu sana, Kamishna
hili ni tatizo kubwa lazima tulikomeshe”, alisema Maalim Seif.
Amelipongeza
Jeshi hilo kwa juhudi kubwa linazozichukua kuwakamata watuhumiwa wa
dawa za kulevya na kuwafikisha mbele ya sheria, lakini hata hivyo
amesema bado juhudi zaidi zinahitajika kuwamata wafanyabiashara wakubwa
ambao mara nyingi hawapatikanwi.
Amesema
Jeshi hilo litajipatia sifa kubwa zaidi na kuipatia sifa nchi, iwapo
litafanya kazi kwa kuzingatia weledi, ukakamavu na uwezo wa hali ya juu
katika kutekeleza majukumu yao na kuhakikisha utawala bora unazingatiwa
kikamilifu.
Ameeleza
kuwa Polisi wanatakiwa kujiepusha na tabia ya kufanya kazi kwa
upendeleo na wahakikishe wanawapatia haki sawa watu wote, iwe kwa
viongozi, watoto wa viongozi au wananchi wa kawaida.
“Sisi
wanasiasa tuna kawaida jamaa zetu wanapofanya makosa na kukamatwa
tunampigia simu Kamishna, msikubali kufanya upendeleo na kuwakandamiza
wananchi wanyonge, hakuna mtu aliye juu ya sheria”, alionya Makamu wa
Kwanza wa Rais.
Awali
akiwasilisha taarifa ya utendaji ya Polisi, Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Hamadan Makame amesema miongoni mwa changamoto zinazolikabili
jeshi hilo ni ukosefu wa vifaa vya kutendea kazi, uhaba wa nyumba za
kisasa kwa ajili ya askari, kuibukwa kwa uhalifu mpya wa kwenye
mitandao.
Changamoto
nyengine amezitaja kuwa kuibuka vikundi vya kidini vilivyosajiliwa na
baadhi ya maeneo ya ardhi yanayomilikiwa na Jeshi la Polisi kuvamiwa na
viongozi na baadhi ya wananchi.
Aidha,
Kamishna huyo amesema ipo haja Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilione
Jeshi la Polisi ni lake, licha ya kuwa lipo chini ya Serikali ya
Muungano, kwa kurejesha utaratibu wa zamani wa kulisaidia kufanikisha
baadhi ya majukumu yake, ikiwemo operesheni maalum zinazotekelezwa hapa
Zanzibar.
Hata
hivyo, Kamishna Makame alitaja miongoni mwa mafanikio makubwa ya Polisi
Zanzibar hivi sasa ni kupungua kwa matukio ya uhalifu mkubwa, kupungua
ajali na makosa ya barabarani, wananchi kuongeza imani kwa Jeshi hilo,
na kufanikisha vizuri suala la kudumishwa amani katika visiwa vya Unguja
na Pemba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: