NDUGU WA MTUHUMIWA WA UJAMBAZI ALIYEUAWA NA POLISI MKOANI ARUSHA WADAI NDUGU YAO ALIKUWA JAMBAZI KWELI

MMOJA wa WANAODAIWA KUWA majambazi watatu waliouawa juzi na polisi jijini Arusha wakati walipokuwa wakijiandaa kuiba kiasi cha Sh milioni 100 kutoka kwenye duka la utengenezaji na uuzaji wa vigae, linalojulikana kwa jina la Arusha Ceramic Center lililopo eneo la Esso, ametambuliwa na ndugu zake, huku wakisema walimuonya kwa muda mrefu lakini hakusikia.Mtu huyo ametajwa kuwa ni Seleman Walii, maarufu kwa jina la Madenge, mkazi wa Kaloleni jijini Arusha. Ndugu hao walimtambua Madenge katika chumba cha maiti cha hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru. Walichukua mwili na kuuzika jana mchana mjini hapa.
Mmoja wa ndugu wa marehemu huyo, akizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina, alisema ndugu yao huyo alikuwa ni mdokozi aliyeogopewa na kwamba walimuonya mara kadhaa kuachana na tabia hizo, lakini alikuwa mkaidi.

“Tulikuwa tukimuonya mara kwa mara aache tabia hiyo ya wizi hakusikia, na sisi tulimwachia Mungu na juzi tuliposikia kuwa amekufa ilibidi tukipokee kifo hicho na leo hii tumemzika’’.

Juzi, Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas alithibitisha kuuawa kwa majambazi watatu, waliokuwa wanajiandaa kuiba Sh milioni 100 katika duka la vigae lililopo eneo la Esso.

Alisema walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa kuna majambazi, wanajiandaa kuvamia duka hilo na kuiba fedha. Ingawa awali hawakuwa wamefahamika, walitajwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 na 30.

Kamanda Sabas alisema mara baada ya kupata taarifa hizo polisi walijipanga na kuanza kufanya doria maeneo hayo, ndipo walipoliona gari namba T 762 CWE aina ya Toyota Corolla eneo la relini na ndipo watu hao walipowashtukia polisi na kuanza kuwarushia risasi.

Alisema baada ya majambazi hao kuanza kuwarushia polisi risasi, polisi nao walijibu mapigo na kuanza kufukuzana nao hadi kwenye kona ya TBL, ambapo majambazi wawili walishuka kwenye gari hilo na kuanza kukimbia wakiwa na bunduki aina ya shotgun yenye namba za usajili A 947514M Action Pump.

Alisema kwenye gari kulikutwa majambazi ambao walidhibitiwa, lakini walikufa wakiwa njiani kupelekwa hospitali ya Mount Meru kwa matibabu.


Alisema walipokagua gari hilo, walikuta risasi 3 na ganda moja la risasi. Miili mingine imehifadhiwa hospitali ya mkoa, ikisubiri kutambuliwa.

0 comments: