Posted by
khamisimussa77@gmail.com
at
5:25 AM
Mvutano
mpya umeibuka baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kumvaa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kikidai ofisi
yake inatumiwa na wasaliti wa chama hicho.
Pia,
chama hicho kimemtaka Jaji Mutungi ajitokeze hadharani kubainisha iwapo
yeye ndiye aliyemtuma msaidizi wake, Sistyl Nyahoza kutangaza kuwa
mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa hawana
sifa ya kugombea uongozi ndani ya chama hicho kutokana na kuzuiwa na
katiba ya Chadema.
Jana,
Nyahoza alikaririwa na vyombo vya habari akisema Mbowe na Dk Slaa
hawana sifa za kugombea uongozi wa chama hicho kutokana na katiba ya
chama chao kuwabana.
Alibanisha
kuwa kipengele cha ukomo wa mgombea katika katiba yao ya mwaka 2006
kiliondolewa kinyemela bila idhini ya mkutano mkuu.
Nyahoza
alisema katiba ya Chadema ya mwaka 2004, ilikuwa na kipengele cha ukomo
wa madaraka kuwa kiongozi aliyeongoza vipindi viwili vya miaka mitano
mitano, hawezi kuwania tena nafasi hiyo.
Jana,
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema Jaji
Mutungi hana mamlaka ya kubaini sifa za viongozi wa chama hicho, bali
wenye mamlaka hayo ni wanachama wa chama hicho pekee.
Mnyika
alisema mwaka 2006, katiba ya Chadema haikurekebishwa, bali iliundwa
upya na kuridhiwa na mkutano mkuu wa chama na kwamba Agosti 13, 2006
ilizinduliwa na nyaraka zote alikabidhiwa Msajili wa Vyama wa wakati
huo, John Tendwa.
Katika
uzinduzi huo wa katiba pamoja na bendera mpya ya Chadema, Tendwa
alikimwagia sifa chama hicho kwa kuonyesha mwelekeo na mwenendo mzuri na
kuvishauri vyama vingine viungane nacho kuunda chama cha upinzani
chenye nguvu nchini.
Akizungumzia
mabadiliko hayo, Mbowe alikaririwa na gazeti hili Agosti 15, 2013
akisema yalikuwa yanalenga kuimarisha mapambano ya kisiasa ya chama
hicho.
Mnyika
alisema: “Mkutano mkuu wa chama uliipitisha Katiba hiyo baada ya
mchakato mrefu wa kukusanya maoni kutoka kwa mabaraza ya wilaya na
majimbo. Hatukurekebisha katiba kama inavyoidaiwa. Ni makubaliano ya
wanachama wote ambao waliafikiana na mambo yaliyotakiwa kuwamo.”
Alisema
katika mchakato huo kulikuwa na makubaliano na mabishano katika baadhi
ya masuala lakini suala la ukomo wa uongozi liliafikiwa na wanachama
wote bila tatizo na kupitishwa kuingia katika katiba na Ofisi ya Msajili
ilipelekewa fomu ya marekebisho pamoja na katiba mpya kama sheria
inavyotaka... “Kama wameipoteza waseme tuwapatie katiba wairejee.”
“Tunachomtaka
Mutungi ni kuheshimu katiba ya chama na kuwaheshimu wanachama wa
Chadema na ayapuuze madai ya wasaliti wachache. Kama vipi asubiri aone
uamuzi wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu ubainishe kama katiba ilivunjwa,”
alisema Mnyika.
Mnyika alisema wameshtushwa na kauli ya ofisi hiyo na kuituhumu kwamba imeanza kutumika kisiasa na wasaliti.
Alipotakiwa
kutoa ufafanuzi wa suala hilo jana, Jaji Mtungi alisema: “Hili suala
lisimamiwe na chama husika kwa kuwasiliana na Ofisi ya Msajili… hakuna
haja ya kulikuza katika vyombo vya habari. Wanachama wa Chadema watapata
taarifa kutoka kwa viongozi wao ni nini kinaendelea.”
Kuhusu
madai kwamba ofisi yake inatumika kisiasa alisema: “Kama nilivyosema,
hayo tuyaache hii ofisi yetu ipo more technical (kitaalamu zaidi)
hatuingizi siasa. Wao (Chadema) waje kwenye ofisi yetu tuongee kama
taasisi, iwapo tunataka kuwasilisha jambo katika vyombo vya habari, basi
tutaitisha mkutano na waandishi wa habari,” alisema Mutungi.
Mamlaka ya msajili
Mnyika
aligusia pia mamlaka ya msajili huyo akisema... “Hana mamlaka ya
kutangaza sifa za mgombea wa Chadema. Sifa na uamuzi vimetajwa katika
katiba na kanuni za chama. Kifungu cha 6.3.2 cha katiba ya 2006
kinabainisha wazi kuwa kiongozi aliyemaliza muda wake na mwenye sifa ya
kugombea anaruhusiwa kugombea...?” Alisema hata katika uchaguzi wa ndani
wa mwaka 2009 viongozi wengi walichaguliwa na wakiwa wameshamaliza
ukomo wa uongozi na msajili wa vyama hakuzungumza chochote.
Alisema
hawababaishwi wala kuguswa na uamuzi uliotolewa na Ofisi ya Msajili wa
kwa kuwa mkutano mkuu wa Chadema unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka
huu, ndiyo utakaoamua hatima wa kiongozi yeyote wa chama hicho.
MWANANCHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: