UVIKASA YAZIDI KUWAINUA VIJANA KWA KUTOA MIKOPO YA PIKIPIKI NA PESA.

 Na Mwandishi wetu - Kagera


Taasisi ya fedha inayojihusisha na kuweka Akiba na Kukopa ya Umoja wa Vijana Karagwe SACCOS LIMITED UVIKASA imekabidhi Pikipiki 37 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 85 kwa Vijana wa Wilaya za Karagwe na Kyerwa ikiwa ni sehemu ya Mkopo kwa Vijana hao ili ziwawezeshe kuwainua Kiuchumi.


Hafla ya kukabidhiwa Pikipiki hizo imefanyika Mnamo Julai 10, 2023 katika Viwanja vya Ofisi za Chama Cha Mapinduzi Wilayani Karagwe Mjini Kayanga, na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo wanachama wa Saccos.

Awali akiongea katika Hafla ya KUkabidhi Pikipiki hizo, Mwenyekiti wa Bodi ya UVIKASA Yahya Kateme ambaye pia ni muasisi wa Saccos hii, amesema kuwa pikipiki 37 zilizotolewa ni aina ya SANYA CC 150 zenye thamani ya shilingi milioni 85 na kusema kuwa licha ya Mkopo huo bado kuna changamoto ya Wanachama kutorejesha kwa wakati marejesho ya pikipiki hizo ambazo hutolewa kwa mkataba, na kuongeza kuwa mpaka sasa Kiasi cha Madeni zaidi ya Shilingi Milioni 900 zinadaiwa ikiwemo pesa Taslimu.

Naye mgeni Rasmi katika hafla hiyo Ndg. Anatory Nshange Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Karagwe amesema kuwa suala la Vijana ambao hawajarejesha mikopo litashughulikiwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Karagwe kwani ambao hawarejeshi wanakwamisha vijana wenzao kukosa fursa ya kukopa.

Mbali na Mikopo hiyo waliopewa, pia Wanachama hao wameunganishwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF ikiwa lengo ni kuwazoesha Vijana hao kuwa na utaratibu wa kuweka Akiba itakayowafaa baadae, na Komredi Kateme akithibitisha hilo kwa kuwalipia Mchango wa kwanza wa Shilingi Elfu Ishirini kila mmoja.

Aidha kwa upande wake Sajenti Mafulu Kahitila kutoka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani Wilaya  Karagwe Awali akitoa Mada juu ya Sheria za uendeshaji Vyombo vya Moto, amesema kuwa Vijana waliokabidhiwa Pikipiki hizo wanao wajibu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani, na kuongeza kuwa baadhi ya waendesha Pikipiki hasa kundi la vijana wamekuwa hawazingatii sheria za Usalama Barabarani hali inayosababisha baadhi ya Vijana kupata Vilema na wengine kufariki kabisa.

Mgeni Rasmi pamoja na Viongozi wakikabidhi Funguo za Pikipiki kwa Wanufaika wa Mikopo ikiwa ni Ishara ya kukabidhiwa Rasmi Vyombo hivyo vya Moto.
Mgeni Rasmi katika Hafla ya Kukabidhi Pikipiki Ndg. Anatory Nshange akikabidhi Kadi za Wanachama wapya wa NSSF ambao ni Vijana wa UVIKASA mara baada ya kuunganishwa na Mfuko huo wa hifadhi ya Jamii.
Mwenyekiti wa Bodi ya UVIKASA LTD Ndg. Yahya Kateme ambaye ni Muasisi wa SACCOS hiyo akitoa Salaam zake wakati wa Hafla ya Kukabidhi pikipiki hizo.
 Mgeni rasmi Ndg. Anatory Nshange Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilayani Karagwe akihutubia Wanachama na wageni wakati wa Hafla ya Kukabidhi Pikipiki 37 kwa Wanachama wa UVIKASA
  Sehemu ya Vijana wa UVIKASA ambao ni wanufaika wa Mikopo hiyo wakiwa katika Hafla ya kukabidhiwa Pikipiki zao.
Wafanyakazi wa UVIKASA wakiwa na Baadhi ya Wanufaika wa Mikopo ya Pikipiki mara baada ya kukabidhidhiwa Pikipiki zao
  Picha ya Pamoja Meza Kuu na Wafanyakazi wa UVIKASA LTD.

0 comments:

TIC KUDUMISHA MAHUSIANO YA UWEKEZAJI NA INDIA

 Na Mwandishi wetu - MAELEZO 

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesaini Mkataba wa Makubaliano (Momerundum of Understanding (MoU)) na nchi ya India kupitia Idara ya Ushirikiano wa Nje na Serikali ya  jimbo la Haryana (FCD, GOH) ikiwa ni kuelekea katika kusaini mikataba mbalimbali ya uwekezaji na kuvutia wawekezaji kutoka India kuja kuwekeza nchini.


Hayo yameelezwa na Gilead Teri  Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) katika Makao Makuu ya Kituo hicho Jijini Dar es Salaam, alipokutana na wawekezaji kutoka jimbo la Haryana ambapo mbali na kusaini mkataba huo, wamefika nchini kuhudhuria maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara Maarufu Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba.


“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu na historia ya maonesho ya sabasaba, wawekezaji zaidi ya sitini kutoka India wamekuja nchini kwaajili ya kutafuta fursa za uwekezaji, baadhi yao wameshiriki maonesho ya sabasaba lakini kwa kushirikiana na ubalozi wetu ulioko India pamoja na serikali ya Jimbo la Haryana, tumefanikiwa kuwashawishi wawekezaji zaidi kuja kuangalia fursa za uwekezaji, malengo yakiwa ni kuongeza ushirikiano kati ya taasisi zetu na taasisi ambazo ziko kwenye jimbo lao ili kukuza uwekezaji na kuleta uwekezaji hapa nchini,” ameeleza Teri

Teri amesema kuwa MoU iliyosainiwa itatumika kama Mfumo Mkuu wa kisheria wa kudhibiti uhusiano wa Tanzania na India kwa kuzingatia maeneo yaliyokubaliwa ya uwekezaji na kwamba wamejipanga kuongeza ushirikiano kati ya tanzania na serikali ya jimbo la Haryana.


“Maeneo ya uwekezaji yaliyokubaliwa chini ya Makubaliano haya ni pamoja na; Magari, Madawa, Viwanda vya Nguo, Vifaa vya Uhandisi/Mashine, nishati, kemikali na mbolea, uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo, sayansi, elimu, utalii na maeneo mengine yenye maslahi kwa pande zote, ni matarajio yetu kuwa kusainiwa kwa Makubaliano haya kutafungua zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na India katika masuala yanayohusiana na uwekezaji, tumekubaliana kwamba, kabla ya mwezi wa tisa kutakuwa na uwekezaji ambao tayari utakuwa umekuja nchini na kuanza kufanya kazi.” Amefafanua Teri.


Aidha, Teri amesema kuwa wataishawishi serikali ya jimbo la Haryana kuja kuwekeza katika kongani za viwanda, kutokana na kwamba jimbo hilo ndilo lenye Kongani za viwanda nyingi zaidi nchini India kuliko jimbo lolote.


Kwa upande wake Dkt. Raja Sekhar Vundru Mkuu wa Msafara Serikali ya Jimbo la Haryana na Katibu Kiongozi wa Idara ya Mambo ya Ushirikiano wa Nje amesema kuwa kutokana na Tanzania kuzidi kupiga hatua katika masuala ya uwekezaji na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kumewasukuma serikali ya jimbo hilo kuja kuwekeza nchini.


“Uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi yetu ndiyo sababu kuu imechangia sisi kuja kutafuta fursa za uwekezaji hapa Tanzania, tuko hapa kama serikali ya jimbo la Haryana kutoka India, ambalo ni miongoni mwa majimbo yaliyoendelea zaidi kiviwanda nchini India, naamini huu ni mwanzo mzuri, tutakuwa na ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na jimbo la Haryana.” 


Kituo cha Uwekezaji Nchini kimeeleza kuwa huo ni mwanzo wa ushirikiano na jimbo la Haryna kutoka nchini India lakini pia kitaendelea kuvutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali ili kukuza uchumi wa Mtanzania na taifa kwa ujumla.


0 comments:

BAHI KINARA UKAMILISHAJI WA MIRADI YA BOOST

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amekabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Godwin Gondwe madarasa 51, Vyoo 63 na nyumba 1 ya waalimu ikiwa ni sawa na shule 7 zilizokamilika katika Wilaya ya Bahi.

Akipokea shule na miundombinu yake Senyamule amepongeza uongozi wa Wilaya ya Bahi kwa kukamilisha mradi huo tarehe 28 Juni 2023 ikiwa ni siku mbili kabla ya tarehe iliyopangwa na Mkoa yaani tarehe 30 Juni 2023.


“Bahi mnajipambanua sana katika suala la elimu, awali tu tulikuwa tunaziambia Halmashauri zingine zije zijifunze kwenu kuhusu kufaulu, leo tutawatuma kujifunza kuhusu mnavyojipanga kukamilisha miradi ya ujenzi kwa wakati na viwango vya hali ya juu” Senyamule amesisitiza.

Amesema Mkoa wa Dodoma umepokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya 16 zenye miundombinu ya kisasa ikiwa ni pamoja na michezo ya watoto na uzio kwa ajili ya madarasa ya awali.

Akikabidhi madarasa hayo Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Godwin Gondwe amesema Wilaya yake imekamilisha ujenzi huo wa Shule na madarasa kwa muda ulioelekezwa kwa ubora na viwango elekezi, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pesa ya kufanikisha ujenzi huo.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa naomba upokee Shule hii na madarasa ambayo yamekamilika kwa viwango vya ubora wa hali ya juu kwa niaba ya wana Bahi naomba utufikishie shukrani zetu kwa Mhe Rais” Amefafanua Mhe. Gondwe

Kwa upande wake Afisa Elimu Wilaya ya Bahi Mwl. Boniphace Wilson amesema kukamilika kwa madarasa hayo ni suluhu ya msongamano wa wanafunzi katika madarasa ya awali ambapo Wilaya hiyo ilipokea fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya mbili zenye jumla ya vyumba 28, madarasa manne ya awali, majengo mawili ya utawala na vichomea taka.

Wilaya ya Bahi imekuwa Wilaya ya kwanza katika Mkoa wa Dodoma kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya mradi wa Boost ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa shule mpya za msingi, vyumba vya madarasa, madarasa ya mfano ya elimu ya awali, matundu ya vyoo na nyumba za walimu.

   Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizundua Shule ya Msingi Bahi Mission baada ya kukamika. Wilaya ya Bahi ilipokea kiasi cha Shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya mbili zenye jumla ya vyumba 28, madarasa manne ya awali, majengo mawili ya utawala na vichomea taka. 

0 comments:

VETA YATAKA VIJANA WAPATE MAFUNZO YA UFUNDI STADI

 
   Kaimu Mkurugenzi Mkuu CPA Anthony Kasore  akizungumza na waandishi katika moja ya banda katika Maonesho ya 47 ya Biashara Kimataifa Dar es Salaam yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Sabasaba Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Picha ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA  katika Mabanda ya VETA.

*Serikali imewekeza nguvu ya kutosha katika kuwafikia watanzania

Na Mwandishi wetu TV
MAMLAKA ya Elimu ya Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) imesema vijana wa kitanzania itumie fursa ya mafunzo ya ufundi stadi kutokana na kuwepo kwa ajira katika mapinduzi ya viwanda nchini.

Hayo ameyasema Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la VETA kwenye maonesho 47 ya Biashara Kimataifa Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Sabasaba Jijini Dar es Salaam.

Kasore amesema kuwa serikali imewekeza nguvu katika ujenzi wa vyuo mafunzo ya ufundi stadi katika kuhakikisha vijana wanapata ujuzi wa kuweza kuajiriwa na kujiajiri pasipo kuwepo kwa changamoto.

Amesema VETA inatarajia kujenga vyuo 64 ikiwemo kimoja cha Mkoa wa Songwe na vingine vyote vya wilaya.

Aidha amesema Serikali ya awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan iko bega kwa bega na VETA katika kuwapatia vijana ujuzi waweze kutengeneza ajira na maendeleo kwa ujumla.

Kasore amesema kuwa katika utoaji wa mafunzo kumekuwa na ubunifu ambapo wabunifu walimu na wanafunzi kazi ya VETA ni kuwashika mkono kwa kuwa na miliki ili watu wengine wasije wakazifanyia biashara.

Kasore amesema kuwa wenye viwanda na wawekezaji wasipate changamoto ya nguvu kazi kutokana na nguvu kazi hiyo imeshazalishwa na VETA.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu amesesma VETA inashirikiana na Costech katika kuhakikisha wabunifu wanakuwa wanatambuliwa na kuweza bunifu hizo kwenda mbali zaidi.

0 comments:

WAZIRI MKUU AKUTANA NA BALOZI WA TANZANIA NCHINI UTURUKI

-Amtaka akadumishe diplomasia ya uchumi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka balozi wa Tanzania Nchini Uturuki Seif Idd Bakari aweke msisitizo katika kusimamia utekelezaji wa sera ya mambo ya nje ikiwa ni pamoja na kudumisha diplomasia ya uchumi, kuhamasisha uwekezaji na upatikanaji wa masoko wa bidhaa za ndani.

“Kupitia mahusiano haya, zipo fursa nyingi ambazo tunahitaji kuzipata hasa za kiuchumi, Tanzania ni nchi ambayo inazalisha na inauza tukiwa peke yetu hatuwezi kumudu ndio maana tunashirikiana na mataifa mbalimbali kupitia mabalozi wetu”

Waziri Mkuu amesema hayo leo (Jumatano, Julai 05, 2023) alipokutana na Balozi huyo ofisini kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Majaliwa pia amemtaka Balozi Seif aweke mikakati itayoiwezesha nchi kunufaika na uwepo wake ikiwemo kusimamia mahusiano ya kibiashara “Tunakaribisha wafanyabiashara kwenye nchi yetu, tunahitaji kupata wawekezaji, wakija nchini tutanufaika kwa kupata teknolojia mpya na kuongeza idadi ya ajira kupitia uwekezaji wao”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Balozi Seif atumie fursa hiyo kuitangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania. “Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alianzisha program ya Royal Tour ambayo imevutia nchi nyingi, nenda kapime kwenye nchi yako wangapi wanaifahamu Tanzania, katumie majukwaa mbalimbali ya kuitangaza nchi yetu”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Balozi Seif kutafuta masoko kwa ajili ya bidhaa mbalimbali zinazotoka nchini “Uzalishaji wetu ni mkubwa na msisitizo bado unaendelea kupitia Sera ya nchi na Jumuiya zetu ikiwemo EAC na SADC tumekuwa na mkakati wa uzalishaji ili tuweze kuuza na kupata Dola.”
  Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Tanzania Nchini Uturuki, Seif Idd Bakari, mara alipomtembelea na kufanya mazungumzo naye, Ofisini kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam. Julai 05, 2023 (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU).


0 comments: