NAPURU WATERFALLS YATWAA TUZO YA UTALII WA IKOLOJIA AFRIKA MASHARIKI

 

Kivutio cha Maporomoko ya Maji ya Napuru, kilichopo katika Shamba la Miti Meru jijini Arusha, kinachosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kimetwaa tuzo ya ubora katika vivutio vya asili na utalii wa maporomoko ya maji katika tuzo za East Africa Sustainability and Conservation Excellence Awards (ESCEA) 2026.
 
 
Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa TFS jana Oktoba 31, 2026, katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Mohamed Ally, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo, Dkt. Andrew Komba.
 
 
Akizungumza katika hafla hiyo, Mohamed alisema tuzo hiyo ni utambuzi wa mchango wa TFS katika uongozi, ubunifu na juhudi za kuendeleza uhifadhi wa mazingira, matumizi endelevu ya rasilimali za asili na maendeleo endelevu katika Afrika Mashariki.
 
 
Kwa upande wake, Afisa Utalii wa Shamba la Miti Meru, Mhifadhi Masanja Kayanogu Juma, alisema tuzo hiyo ni chachu kwa TFS kuendelea kuimarisha juhudi za kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu zinazowezesha kuibua na kuendeleza vivutio vya utalii wa ikolojia.
 
 
Shamba la Miti Meru ni miongoni mwa maeneo yenye fursa za utalii wa ikolojia jijini Arusha, likiwa na Maporomoko ya Maji ya Napuru kama kivutio chake kikuu, kinachovutia wageni wanaotafuta uzoefu wa utalii unaotegemea urithi wa asili.
Hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliwakutanisha viongozi wa Serikali, wafanyabiashara, wataalamu wa uhifadhi wa mazingira, wawekezaji, wadau wa utalii na wawakilishi wa mashirika mbalimbali kwa lengo la kutambua mafanikio katika uhifadhi na kuimarisha mahusiano ya kibiashara.







0 comments: