IRAN IKO TAYARI KUSHIRIKIANA NA SIERRA LEONE KATIKA KUPAMBANA NA UGAIDI

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria mashambulio ya kigaidi katika baadhi ya nchi za Ulaya na Afrika na kutangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kushirikiana na Sierra Leone katika kupambana na ugaidi na misimamo ya kufurutu mpaka.
Muhammad Javad Zarif ametangaza msimamo huo hapa mjini Tehran katika mazungumzo na Mohamed Gibril Sesay, Waziri wa Nchi Katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Sierra Leone aliyeko safarini hapa nchini.
Katika mazungumzo hayo Dakta Zarif amesema, kwa upande wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni, bara la Afrika lina umuhimu maalumu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na kustawisha uhusiano na nchi za bara hilo kumekuwa kukipewa kipaumbele na Iran tangu baada ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria pia uwezo na fursa za kiuchumi zilizopo katika uhusiano wa Iran na Sierra Leone na kueleza kuwa katika kipindi kipya cha uongozi wa Rais Hassan Rouhani, nchi hizi mbili zinaweza kustawisha zaidi uhusiano wao wa kiuchumi kwa kutumia mikakati ya kivitendo.
Kwa upande wake, Mohamed Gibril Sesay, Waziri wa Nchi Katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Sierra Leone amesisitizia umuhimu wa uhusiano wa nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kwamba kustawisha uhusiano katika nyanja zote ni jambo linalopewa kipaumbele na nchi yake.
Aidha ametilia mkazo nafasi na mchango muhimu wa Iran katika kuleta amani na uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati na mapambano dhidi ya ugaidi na kubainisha kuwa Sierra Leone iko tayari kushirikiana na Iran katika kupambana na ugaidi na misimamo ya kufurutu mpaka.../

0 comments: