ISRAEL YAZIDISHA HARAKATI ZA KUIYAHUDISHA QUDS TUKUFU

Duru za Palestina zimetangaza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umechimba mashimo mapya chini ya Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Habari hiyo imetangazwa na Kamati ya Kiislamu na Kikristo kwa Ajili ya Kulinda Quds na Matukufu yake. Katibu Mkuu wa kamati hiyo Dk, Hanna Issa ametahadharisha juu ya hatari ya mashimo hayo ya chini ya ardhi kwa majengo na taasisi za Msikiti wa Al-Aqsa na kueleza kwamba, idadi ya mashimo hayo ya chini kwa chini katika mji wa Quds ambayo yanaviunganisha pamoja vitongoji wa walowezi wa Kizayuni yamefikia 27.
Image Caption
Tangu utawala wa Kizayuni wa Israeli ulipouvamia na kuanza kuukalia kwa mabavu mji wa Quds mwaka 1967 hadi sasa unaendelea kuchimba mashimo ya chini ya ardhi katika mji huo hasa katika eneo lake la kale na kandokando mwa Msikiti wa Al-Aqsa ili kuwalazimisha Wapalestina wayahame maeneo hayo na kuweza kuyadhibiti maeneo yanayozunguka msikiti huo. Ili kuharakisha zoezi la kufikiwa lengo hilo na kuvunja Msikiti wa al Aqsa ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu, utawala huo ghasibu umekuwa ukichimba mashimo chini ya eneo hilo takatifu na kandokando yake kwa shabaha ya kudhoofisha msingi na nguzo zake. Suala hilo linahatarisha na kuzidisha uwezekano wa msikiti huo kuporomoka na kuvunjika iwapo kutatokea tetemeko dogo la ardhi na matukio mengine kama hayo. Vilevile Israel inafanya mikakati ya kuanzisha tetemeko la makusudi la ardhi kwa kulipua maeneo ya chini ya Msikiti wa al Aqsa, ili ionekane kwamba, uharibifu wa msikiti huo umetokana na suala la kimaumbile. Kwa sababu hiyo duru za kuaminika zinasema, njama na mipango ya utawala haramu wa Israel ya kuvunja Msikiti wa al Aqsa imeingia katika awamu nyeti na hatari sana.
Msikiti wa al Aqsa
Kwa miaka mingi sasa Israel imekuwa ikitekeleza mpango wa kubadilisha utambulisho wa Kiislamu wa mji wa Quds tukufu kwa kuharibu turathi za Kiislamu na za kale za mji huo na kuweka badala yake alama za Kiyahudi. Katika mkondo huo Israel imekuwa ikiharibu misikiti, majumba ya kihistoria, maeneo ya makaburi ya kale, vituo vya kiutamaduni, mashamba na nyumba za Wapalestina na kujenga maabadi za Wayahudi na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Hayo yanafanyika licha ya kwamba maazimio nambari 242 na 338 ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na vilevile kifungu nambari nne cha Mkataba wa Geneva vimepiga marufuku aina yoyote ya ujenzi na kubadilisha utambulisho wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina.  
Mashimo yanayochimbwa na Israel chini ya Msikiti wa al Aqsa
Jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel kama zile za kuharibu au kuvunjia heshima maeneo matakatifu ya Kiislamu au kuvamia maeneo hayo na kuwafukuza Wapalestina ni kielelezo cha siasa za kibaguzi za utawala huo dhidi ya wafuasi wa dini za mbinguni na uhuru wa kuabudu. Kwa msingi huo kuna udharura kwa jumuiya za kimataifa kuchukua msimamo mmoja na madhubuti wa kukabiliana kivitendo na siasa hizo za kibaguzi za Israel na zisitosheke kutoa maazimio yasiyokuwa na dhamana ya utekelezaji dhidi ya utawala huo.

0 comments: