Ripoti mbalimbali kutoka nchini Bahrain
zinaonyesha kuwa, utawala wa kifalme wa nchi hiyo umeendelea kutumia
mbinu na miamala yake ya kipolisi dhidi ya wanaharakti wa kisiasa huku
ukiendelea kuwatia mbaroni na kuwahukumu vifungo vya muda mrefu jela
wapinzani hao kwa kuwabambikiza tuhuma mbalimbali.
Katika kipindi cha mwezi mmoja
uliopita, makumi ya wanaharakati wa Bahrain wametiwa mbaroni. Aidha
Jumatano ya jana mahakama moja ya nchi hiyo iliwahukumu kifungo cha
maisha jela wanaharakati sita wa nchi hiyo, hatua ambazo zinabainisha
kuendelea vitendo vya ukandamizaji dhidi ya wananchi wa nchi hiyo.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Bahrain
alidai Jumatano ya jana kwamba, wanaharakati hao sita ambapo wawili kati
yao hawakuweko mahakamani wakati wa kutolewa hukumu hiyo, wamepatwa na
hatia ya kupigana na vikosi vya usalama mjini Manama mwaka jana. Wakati
huo huo, baada ya Nabil Rajab, Mkuu wa Kamati ya Haki za Binadamu ya
Bahrain kushikiliwa kwa miezi mitatu katika chumba ya peke yake,
Jumatano ya jana alipelekwa hospitali kutokana na matatizo ya moyo
yanayomkabili.
Jinai za utawala wa kifalme wa Aal Khalifa nchini Bahrain dhidi ya
wananchi wa nchi hiyo zinaendelea kushuhudiwa katika hali ambayo,
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limetangaza kuwa,
muamala mbaya dhidi ya wafungwa ikiwemo vitendo vya mateso dhidi ya
wafungwa hao vingali vinaendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo
inayotawaliwa kwa mfumo wa kifalme.
Wananchi wa Bahrain wanaoshikiliwa
katika magereza na korokoro za nchi hiyo wametangaza mara chungu nzima
kwamba, wanakabiliwa na mateso makali na kwamba, wamekuwa wakiteswa ili
wakiri makosa ambayo kimsingi hawajayafanya. Hatua hizo zinathibitisha
kwamba, mahakama za Bahrain hazina hata vigezo vidogo kabisa vya
kimataifa za utoaji hukumu kwa uadilifu. Vitendo vya dhulma na
ukandamizaji nchini Bahrain vimekithiri kiasi kwamba, Shirika la Kutetea
Haki za Binadamu la Human Rights Watch limeutaja mfumo wa kimahakama
nchini humo kwamba, ni " Mfumo Kwa Ajili ya Dhulma" na kusisitiza
kwamba, mahakama za nchi hiyo ya Kiarabu zimekuwa na nafasi muhimu
katika kuusauidia utawala wa nchi hiyo katika kutekeleza siasa zake za
ukandamizaji.
Kwa hakika matukio ya Bahrain yanabainisha uhakika huu kwamba, kuna
ukandamizaji mkubwa kabisa unaofanywa na utawala wa Aal Khalifa dhidi ya
wananchi wa nchi hiyo. Kamatakamata na utiaji mbaroni ni vitendo
ambavyo vimekuwa vikichukua mkondo mpana zaidi na wa kutia wasiwasi.
Hukumu za kidhalimu dhidi ya wanaharakati wa kisiasa zinaendelea
kutolewa nchini Bahrain katika hali ambayo, ripoti kutoka nchini humo
zinaonyesha kuwa, kwa sasa kuna zaidi ya wanaharakti elfu kumi katika
magereza ya Bahrain huku 150 kati yao wakiwa wamehukumiwa kifungo cha
maisha jela.
Ukiukaji wa haki za binadamu wa utawala
wa Aalha Khalifa umeigeuza nchi hiyo na kuifanya kuwa gereza kubwa. Kama
ilivyokuwa huku nyumba, utawala wa Baharin umeendelea kupata himaya na
msaada wa Saudia katika hatua zake za ukandamizaji dhidi ya raia.
Tangu Februari mwaka 2011, Bahrain
imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala
wa Aal Khalifa. Matakwa makuu ya Wabahrain ni kuwepo utawala wa
kisheria, kukomeshwa ubaguzi wa kimadhehebu, kufanyika mageuzi ya
kisiasa na kuheshimiwa haki za binadamu. Matakwa na madai hayo ya kiraia
ya wananchi wa Bahrain yanamaanisha kupoteza uhalali wa kutawala
utawala wa kifamilia wa Aal Khalifa. Hata hivyo matukio ya Bahrain
yanaonyesha kuwa, hatua ya utawala wa Manama ya kusimama kidete mkabala
na matakwa halali ya wananchi ni kufuata njia ya madikteta wa zamani
kama Kanali Muammar Gaddafi wa Libya, Hosni Mubarak wa Misri, na Zeinul
Abidiin wa Tunisia; njia ambayo haina natija nyingine ghairi ya
kukumbwa na ghadhabu za wananchi na mwisho wa usiku ni kudhalilika.
No comments:
Post a Comment