Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi.
Karibuni katika makala hii maalumu tuliyokuandalieni kwa mnasaba wa
kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Husain AS. Ni mfululizo wa makala maalumu
ambazo zinakujieni katika kipindi cha siku hizi kadhaa za kuelekea
kwenye kilele cha kumbukumbu hizo zinazofanyika Karbala nchini Iraq
ambapo kwa mwaka huu itakuwa ni Jumatatu ya tarehe 21 Novemba kulingana
na mwandamo wa mwezi nchini Iraq. Karibuni.
Wanavyuoni
wengi wa dini tukufu ya Kiislamu, wanamuhesabu Imam Husain AS kuwa ni
moja ya njia kuu za kuleta umoja na mshikamano kati ya umma wa Kiislamu.
Mapenzi makubwa ya Waislamu kwa Imam Husain AS hayawahusu Waislamu wa
Kishia tu, bali huyo ni kipenzi cha Waislamu wote.
Kuna
hadithi nyingi za Mtume Muhammad SAW zinazoonesha utukufu wa kipenzi
chake huyo na kusisitiza kuwa Imam Husain AS ni wa Waislamu wote.
Miongoni mwa hadithi maarufu ni zile zinazosema, Hassan na Hussein ni
mabwana wa vijana wa peponi, Husain anatokana na mimi na mimi ninatokana
na Husain, Mwenyezi Mungu mpende anayempenda Husain na Husain ni
merikebu ya wokovu na taa ya uongofu na hadhithi nyinginezo nyingi.
Sisitizo lote hilo la Bwana Mtume Muhammad SAW linaonesha kuwa Imam
Husain ni wa Waislamu wote, si wa Waislamu wa Kishia pekee na kumpenda
Husain ni wajibu uliohimizwa mno na Bwana Mtume. Maana ya kumpenda mtu
nako kama tunavyojua, ni kufurahishwa na linalomfurahisha mtu huyo na
kuhuzunishwa na linalomuhuzunisha. Arubaini ya Imam Husain AS ni
kumbukumbu ya siku ya arubaini tangu tarehe 10 Muharram, aliyouawa
shahidi mtukufu huyo katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria. Hiyo ni
siku ambayo wapenzi wa Husain na Bwana Mtume Muhammad SAW wanakusanyika
kwa mamilioni huko Karbala Iraq kuomboleza kuuliwa kikatili mjukumuu
huyo wa Mtume mwaka 61 Hijria. Naam, Arubaini ya Husain ni mjumbe wa
umoja na mshikamano baina ya Waislamu wote.
Kama
tulivyotangulia kusema, wanavyuoni wengi wa dini tukufu ya Kiislamu,
wanamuhesabu Imam Husain AS kuwa ni moja ya njia kuu za kuleta umoja na
mshikamano kati ya umma wa Kiislamu. Mapenzi makubwa ya Waislamu kwa
Imam Husain AS hayawahusu Waislamu wa Kishia tu, bali huyo ni kipenzi
cha Waislamu wote. Hivi sasa njia na mabarabara ya kuelekea Karbala
nchini Iraq yamejaa Waislamu wa madhehebu mbalimbali bali hata wasio
Waislamu, kuelekea kwa mahbubu wao kwa kiu na shauku kubwa. Machofu ya
safari hayana nafasi kwa maashiki hao. Naam, Waislamu wote wanampenda
Imam Husain AS kwa kuwa ni mjukuu wa Mtume Muhammad SAW bali ni sehemu
ya mwili wa mtukufu huyo na wanawahesabu wauaji wa Imam Husain kuwa ni
watu waovu kabisa. Yazid mwana wa Muawiya alikuwa maarufu kwa maadili
maovu na kutoshikamana na dini, na si kwamba alidhulumu haki ya Ahlul
Bayt wa Bwana Mtume pekee bali alifanya dhulma nyingine nyingi na kuua
kikatili mno Waislamu na maswahaba wa Bwana Mtume Muhammad huko Madina
na kuwavunjia heshima wanawake wa Kiislamu. Mauaji hayo maarufu
yanayojulikana kwa jina la mauaji ya Harrah yalifanywa na jeshi la Yazid
dhidi ya Waislamu wa Madina na masahaba wa Bwana Mtume Muhammad SAW
muda mchache baada ya kufanya mauaji ya kutisha dhidi ya mjukuu wa Bwana
Mtume yaani Imam Husain AS. Tab'an kipindi hiki si kwa ajili ya
kuzungumzia jinai zilizofanywa na Yazid, hivyo hatutosema mengi
kuhusiana na suala hilo. Tulichokusudia kusema tu ni kuwa Imam Husain AS
alisimama kupambana na mtu ambaye kivuli kiovu cha dhulma na ufisadi
wake kiliwatesa Waislamu wote bila ya kubagua, na utawala wake wa kiimla
ulilenga moja kwa moja kuaangamiza Uislamu na sunna za Bwana Mtume
Muhammad SAW. Hivyo mtazamao wa maulamaa wakubwa wa dini ya Kiislamu
kutoka madhehebu mbalimbali ni wajibu wa kumpenda Imam Husain AS na
mapenzi hayo ni nukta inayoyaunganisha madhehebu yote ya Waislamu.
Kama
tutazingatia kidogo tu aya za Quráni Tukufu na hadith za Bwana Mtume
SAW tutaona kuwa, dini tukufu ya Kiislamu imehimiza mno suala la umoja
na mshikamano baina ya Waislamu, kiasi kwamba Quráni Tukufu inawataka
Waislamu kujiepusha kuingia katika mizozo na malumbano, hata na
wasiokuwa Waislamu ili isiwe sababu watu hao kumtukana Mwenyezi Mungu
kiuadui na kuwa sababu ya kujenga uhasama baina yao na Waislamu.
Waislamu wamehimizwa mno kujiepusha na vita hata na watu ambao si
Waislamu lakini si maadui. Mwanachuoni maarufu Kashiful Ghitaa ambaye ni
mmoja wa maulamaa wakubwa sana na marajii wa karne ya 13 Hijria katika
ulimwengu wa Kishia ameandika hivi: Uislamu umeundwa juu ya maneno
mawili makuu: کلمه التوحید و توحید الکلمه Yaani
Neno la Tawhidi na Kuunganisha Umma au kwa maneno mengine ni kuwa
Uislamu umeundwa kwa maneno mawili, tawhidi na mshikamano. Tawhidi ikiwa
na maana ya kumwabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake bila ya kumshirikisha na
chochote katika hali yoyote ile, na mshikamano una maana ya kuleta
umoja katika jamii ya Kiislamu. Amma katika aya ya 105 ya Surat Aal
Imran, Mwenyezi Mungu anawakataza Waislamu wasifarikiane kwa kuwambia: Wala
msiwe kama wale waliofarikiana na kukhitalifiana baada ya kuwafikia
hoja zilizo wazi. Na hao ndio watakaokuwa na adhabu kubwa. Naye
Bwana Mtume Muhammad SAW amenukuliwa akisema, Hakuna umma wowote
uliozozana baada ya Mtume wao ila kundi la batili liliwafunika wenye
haki.
Moja
ya baraka za umoja kati ya Waislamu bali hata kati ya watu wowote wale
ni kuweza watu hao kuishi kwa salama na utulivu mkubwa na kupitia
utulivu huo huweza kuchanua vipaji vya watu wa jamii hiyo na kuwafanya
watende mambo yao kimantiki. Mshikamano huo unapokuwa ni kwa ajili ya
Mwenyezi Mungu, waja wema huweza kuongoza mambo ya jamii hiyo na kuwa
sababu ya mafanikio ya duniani na Akhera. Lakini mizozo na mifarakano ni
sawa na moto unaowasha na kuteketeza mavuno yote ya mwanadamu na
hatimaye kuishia kwenye moto wa adhabu ya Mwenyezi Mungu kwani mizozo
huipokonya jamii fursa ya kufikia kwenye ukamilifu wake wa kibinadamu na
hivyo kuwa sababu ya kumwasi Mola wao Muumba.
Tunapotupia
jicho kidogo tu matunda mazuri yasiyo na kifani ya umoja na mshikamano
baina ya Waislamu bilioni moja na nusu duniani tutapata kiurahisi sana
majibu ya kwa mini maadui wa Uislamu wana woga na kiwewe kikubwa cha
kufikiria tu mshikamano wa Waislamu. Na hiyo ndiyo sababu inayowafanya
wafanye kila wanaloweza kuhakikisha kuwa mizozo na ugomvi haumaliziki
katika safu za Waislamu. Hivi sasa pia waistikbari na maadui wa Uislamu
wameongeza njama zao kuliko wakati mwingine wowote kwa ajili ya
kuwagombanisha Waislamu na kujenga uadui mkubwa baina ya madhehebu
mbalimbali ya Waislamu. Leo hii umma mkubwa wa Waislamu unahitajia mno
umoja kwa ajili ya kujiokoa kutoka katika mateso ya kila namna
wanayofanyiwa katika kila kona ya dunia. Mateso ya Waislamu leo hii
yanashuhudiwa kila mahali, kuanzia Myanmar hadi katika nchi za Iraq,
Syria, Yemen, Bahrain, Nigeria na sehemu nyingine nyingi ulimwenguni.
Katika mazingira kama haya, njia iliyooneshwa na Imam Husain AS ambaye
alijitolea kila kitu chake kwa ajili ya kupigania haki na kuulinda
Uislamu, inarejesha matumaini kwa Waislamu ya kuweza kushinda dhulma
zote hizi zilizoukumba umma wa Kiislamu leo hii. Njia hiyo ya Imam
Husain AS ambayo ndiyo njia ya babu yake; Bwana Mtume Muhammad SAW ya
kusimama imara kupigania haki, ni nukta muhimu mno ya kuwaunganisha
Waislamu wa madhehebu yote ambao kama tulivyotangulia kusema, wote
wanakubaliana juu ya wajibu wa kumpenda mjukuu huyo wa Bwana Mtume. Njia
iliyooneshwa na Imam Husain AS inaleta nuru kila pale ambapo giza
linaonekana kukaribia kufunika haki. Arubaini ya Imam Husain AS ni fursa
nyingine kwa wanadamu ya kuweza kurudi kwenye dhati yao, naam, kila
dhati ya mwanadamu imeumbwa kupenda haki na kuchukia dhulma.
Hivi
sasa katika nchi ya Waislamu ya Iraq, kwa miaka mingi wakazi wake
wanaishi katika mazingira ya ukosefu mkubwa wa amani na vitendo vya
kigaidi. Hivi sasa wimbi kubwa la mamilioni ya watu linaendelea
kukusanyika nchini humo likijiandaa kwa ajili ya kumbukumbu ya Arubaini
ya Imam Husain AS. Huo ni mkusanyiko mkubwa zaidi wa watu duniani kila
mwaka. Waislamu wa madhehebu mbalimbali, bali hata wasio Waislamu
hushiriki katika safari ndefu ya kutoka Najaf kwa miguu hadi Karbala,
tajiriba ambayo mtu yeyote hawezi kuilezea kwa maneno ila yule
aliyeshiriki kwenye maandamano hayo ya mamilioni ya watu. Maandamano
hayo yanakusanya watu wa rika zote, watu wa daraja za kila aina katika
jamii bali ukitoa Waislamu wa Kishia, Waislamu wengi wa Kisunni, na pia
Wakristo na wafuasi wa dini nyinginezo hujumuika pamoja kwenye
maandamano hayo. Hata hivyo maadui wanaeneza uongo mwingi kuhusiana na
maandamano hayo. Bali pia wanatenga fedha nyingi kuyasaidia magenge ya
kigaidi kama vile Daesh kueneza chuki baina ya Waislamu. Wanapandikiza
fikra ya kwamba hakuna uwezekano wowote wa Waislamu kuwa kitu kimoja na
wanakabiliana na juhudi yoyote ile ya kuleta mshikamano baina ya
Waislamu. Maadui wanafanya njama za kila namna kuwazuia Waislamu
wasishiriki katika kumbukumbu za Arubaini ya Husain AS na kumbukumbu
nyingine za Karbala kwani kadiri kumbukumbu hizo zinavyopata nguvu,
ndivyo umma wa Kiislamu unavyozidi kuwa imara kwa kumfanya kipenzi huyo
wa Bwana Mtume ruwaza njema ya kupambana na dhulma kwa hali yoyote ile.
Hata hivyo pamoja na kuweko njama zote hizo za maadui, mvuto wa kipekee
wa Imam Husain AS unazivutia nyoyo za wapenda haki na kuzifanya ziweke
pembeni tofauti zao zote ndogo ndogo na kuungana katika mapenzi ya
maashuki na mahbubu wao huyo.
Barabara
za kuelekea Karbala hivi sasa zimejaa vituo ambavyo watu wa kila namna
wa kujitolea, wametenga muda wao wote kuwahudumia maashiki wa Husain AS.
Wahudumu wakuu wa wafanya ziara hao ni wanavijiji wa Iraq ambao
wanajitolea kila kitu chao kuwahudumia wageni hao wa Imam Husain AS.
Fukuto la mapenzi kwa Imam Husain AS limewafanya wanavijiji hao kwa
nyoyo safi kujitolea kila walicho nacho kupiga kambi katika barabara za
kuelekea Karbala ili kupata baraka za kuwahudumia maashiki wenzao wa
Imam Husain AS. Cha kuvutia zaidi ni kuwa Waislamu hao si wa madhehebu
ya Kishia tu, bali Waislamu wa madhehebu ya Kisuni nao hawako nyuma
katika jambo hilo tukufu. Naam, Husain AS ni wa Waislamu wote, bali ni
wa kila mpigania haki duniani. Hata Wakristo nao utawaona wanapiga kambi
katika barabara za kuelekea Karbala na kuvipa jina la Masih Isa AS
vituo vyao vya kuwahudumia wageni wa Imam Husain AS. Wakristo hao
wanasema kuwa, Imam Husain AS anatuhusu sote. Misafara ya Waislamu wa
Kishia kutoka Pakistan, India na Afghanistan huwa inalazimika kupitia
nchini Iran kwa ajili ya kujiunga na wimbi kubwa la maashiki wa Husain
wanaoelekea Karbala. Wakati wanapoanza safari yao ya kuingia Iran, huwa
wanapitia maeneo ya Waislamu wa Kisuni, na wakati wanapoingia katika
ardhi ya Iran huwa wanapokewa kwa mapenzi makubwa na Waislamu wenzao wa
Iran wa madhehebu ya Kisuni na huu ni katika muujiza wa mvuto wa mjukuu
huyo wa Bwana Mtume SAW ambaye mapambano yake yameziteka nyoyo za
wanadamu na kuwa nguzo ya mshikamano baina yao.
Kwa
kweli ni vigumu mno kuitolea maelezo mandhari ya kipekee ya watu wa
makabila, mataifa, rika, madhehebu na dini tofauti wanaojumuika pamoja
na kukubali mashaka na tabu nyingi za safari na hatari za kiusalama za
kushambuliwa na magaidi kwa ajili ya kwenda kumzuru mjukuu wa Bwana
Mtume Muhammad SAW Imam Husain AS huko Karbala Iraq. Bila ya shaka ni
kwa sababu hii ndio maana Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW wamewahimiza
sana wafuasi wao kulipa umuhimu mkubwa suala la kumzuru Imam Husain AS.
Kwani mtu anapokuwa na welewa sahihi kidogo tu kuhusiana na mtukufu
huyo, welewa huo huujaza moyo wake mapenzi makubwa sana kwa Husain AS na
ndio maana leo hii, kadiri siku zinavyopita, kumbukumbu za Imam Husain
AS hususan Arubaini zinavutia nyoyo za watu wengi zaidi tena kwa
mamilioni kutoka kona zote za dunia na haijalishi ni watu wa madhehebu
na dini gani, muhimu ni kuwa wawe wapenda haki na ni maadui wa batili,
na huo ni uthibitisho tosha kwamba Arubaini ya Imam Husain AS ni mjumbe
wa umoja wa Kiislamu, ulimwenguni. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi
Wabarakaatuh.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: