Akizungumza wakati wa kukabidhi mfano wa hundi, mwakilishi wa Kampuni ya GSM, Shannon Kiwamba, alisema wameguswa na changamoto zinazowakabili Watanzania ndiyo maana imeamua kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli ya kuboresha huduma za afya hapa nchini.
Shannon alisema, pamoja na msaada wa fedha ambazo GSM imeipa Moi, vilevile watafadhili kambi za upasuaji (Surgical camps) kwa watoto wenye matatizo ya vichwa kujaa maji na mgongo wazi katika mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Dkt Othman Kiloloma, alisema anaishukuru GSM kwa kuguswa na hali za Watanzania hususan watoto wenye matatizo ya vichwa kujaa maji na mgongo wazi ambao kimsingi wanahitaji kufarijiwa.
Dkt kiloloma aliongeza, GSM imefanya uamuzi sahihi wa kuunga mkono jitihada za Serikali kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya kwa wakati mwafaka.
Alisema, fedha zilizotolewa na GSM zitatumika kama ilivyoelekezwa, vilevile Moi ipo tayari kutoa wataalamu kwenda mikoani kuwafanyia upasuaji watoto katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ili kuwapunguzia wagonjwa adha ya kusafiri kwenda Dar es Salaam.
Taasisi ya Moi imekuwa ikichukuwa jitihada madhubuti za kuhakikisha Watanzania hususan watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wanapata huduma bora pale walipo, ambapo imekuwa ikipeleka wataalam mikoani kwa ufadhili wa wadau mbalimbali na kuwafanyia upasuaji.
Takwimu zinaonesha hapa Tanzania watoto zaidi ya 5,000 kwa mwaka wanazaliwa na vichwa vikubwa na mgongo wazi ambapo watoto 400 mpaka 500 pekee ndiyo wanapokelewa Moi.
0 comments: