Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ushindi huo, Kyaw, mwenye umri wa miaka 69, amesifu kuchaguliwa kwake katika wadhifa huo. ''Hii ni huruma na mapenzi waliotuonyesha watu. Huu ni ushindi kwa watu wote wa nchi hii. huu pia ni ushindi kwa Aung San Suu Kyi,'' alisema Kyaw.
Mfumo wa uchaguzi wa Myanmar unahitaji rais achaguliwe kutoka kwenye orodha ya majina ya wagombea watatu, huku jina moja likiwa limewasilishwa na mabunge yote mawili na jina la tatu litakalopendekezwa na jeshi, ambalo huchukua robo ya viti vya bunge.
NLD kilimteua Kyaw
Alhamisi iliyopita, chama cha Suu Kyi cha National League for Democracy-NLD, kilimteua Kyaw kuwa mgombea wake. Wagombea wengine wawili walikuwa ni Henry Van Thio, mshirika wa Suu Kyi, ambaye jina lake liliwasilishwa na bunge na jeshi lilimteua Myint Swe, jenerali mstaafu wa jeshi.
Swe atakuwa makamu wa kwanza wa rais baada ya kupata kura 213, huku Van Thio mbunge wa watu wa jamii ya Chin akiteuliwa kuwa makamu wa pili wa rais baada ya kupata kura 79. Suu Kyi mwenye umri wa miaka 70, mshindi wa tuzo ya Nobel, na chama chake cha NLD walishinda katika uchaguzi wa Novemba ambao ulionekana kama kuidhinisha sera yake ya mabadiliko. Hata hivyo, Suu Kyi amezuiwa na katiba ya Myanmar iliyo chini ya jeshi, kugombea urais kwa sababu watoto wake wawili ni Waingereza.
Baraza jipya la mawaziri pia linatarajiwa kutangazwa kabla ya mwisho wa mwezi huu na litakuwa na majukumu ya kushughulikia changamoto kadhaa zinazolikabili taifa hilo, ikiwemo umasikini, ukosefu wa miundombinu na mizozo katika maeneo ya mipakani dhidi ya jamii ya watu wachache.
Rais Kyaw anatarajiwa kuapishwa Aprili Mosi, kuliongoza taifa hilo kwa miaka mitano na kuchukua nafasi ya rais anayeondoka madarakani, Thein Sein aliyekuwa akiungwa mkono na jeshi. Kiongozi huyo anasifiwa kwa kuliweka taifa hilo katika mkondo sahihi wa kuondokana na utawala wa moja kwa moja wa kijeshi.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP,AP,DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
0 comments: