Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Awatoroka Waandishi wa habari

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda jana alilazimika kutumia mlango wa uani kuondokea badala ya ule mkuu kwa kile kinachohisiwa kuwakwepa waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia ufunguzi wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje na mazingira kutoka nchi za Afrika. 
 
Pinda ambaye alikuwa akifungua mkutano huo, aliondoka mara tu baada ya kumaliza shughuli iliyompeleka huku akiacha kushiriki tukio la kupiga picha lililoandaliwa kwa ajili yake upande wa lango kuu wa ukumbi huo ambako waandishi walikuwa wakimsubiri  kwa ajili ya kufanya naye mahojiano. 
 
Awali wakati Pinda akihutubia mkutano huo uliokuwa ukifanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, baadhi ya maofisa wa itifaki walionekana wakisimamia zoezi la kupanga viti kwa ajili ya tukio la picha ya pamoja ambalo Waziri Mkuu huyo kama mgeni rasmi ilitakiwa ashiriki.
Pinda
 
Ni maofisa hao pamoja na baadhi ya watumishi wa idara zinazohusika na mkutano huo, ndio waliowaelekeza baadhi ya waandishi wa habari ambao hawakubahatika kuingia ndani kusubiri katika eneo hilo la lango kuu ili waweze kufanya mahojiano na Pinda hata hivyo ahadi hiyo haikutimia.
 
Hatua hiyo ndiyo iliyoibua hisia kwamba huenda, Pinda alifanya hivyo kukwepa maswali ya waandishi wa habari hasa kutokana na kuwepo kwa taarifa zinazodai kuwa ametangaza dhamira yake ya kuwania ukuu wa dola mwaka 2015.
 
Tangu taarifa hizo ziripotiwe kwa mara ya kwanza na vyombo vya habari Jumapili iliyopita, si Pinda wala wasaidizi wake wa karibu ambao walijitokeza kuthibitisha juu ya taarifa hizo.
 
Kutokana na hilo vyombo vya habari nchini vimekuwa vikimtafuta Pinda ili aweze kuzungumzia habari hizo, ambazo anadaiwa kuzitoa mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa aliokutana nao Ikulu ndogo ya jijini Mwanza, Jumamosi iliyopita.
 
Katika tukio la jana wakati waandishi wakimsubiri nje ya lango kuu, Pinda alionekana akishuka chini na kuingia katika eneo la pembeni ya ukumbi, ambako inasemekana eneo hilo lina mlango wa nyuma wa kutokea nje ya ukumbi.
 
Waandishi hao, kwa matumaini waliendelea kumsubiri  Pinda kwa zaidi ya dakika kumi bila mafanikio, huku viti vilivyoandaliwa kwa ajili ya picha ya pamoja vikiwa  vimetelekezwa na mkutano ukiendelea kama kawaida ndani ya ukumbi huo.
 
Baada ya muda alijitokeza kijana  ambaye inasemekana ni mmoja wa wafanyakazi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira akisema kuwa; “Jamani tuliwaalika watu wachache Waziri Mkuu ameshamaliza na ameondoka, kama kuna mtu hajamsikiliza Press release (taarifa ya vyombo vya habari) ya Waziri Mkuu ipo akatoe ‘photocopy’ karatasi ipo kwa  yule dada, (huku akionyesha mmoja kati ya waandishi waliokuwa ndani ya ukumbi na kwa wale wa Tv naomba mchukue kwa kaka pale wa Tumaini.”
 
Akiwa mkoani Mwanza wiki iliyopita, Pinda anadaiwa kuwaeleza wajumbe hao wa CCM kuwa ameamua kuwania nafasi ya  Urais  baada ya kushawishiwa na viongozi wakuu wastaafu  na viongozi wa dini.

0 comments: