MWENYEKITI WA BUNGE LA KATIBA MPYA SAMUEL SITTA AWAAHIDI WALEMABU KUTENDEWA HAKI KATIKA KATIBA MPYA IJAYO
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 12:28 PM
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta
akiwahakikishia suala la haki kwa Watu wenye Ulemavu katika Katiba Mpya ijayo
wakati wa mkutano na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA)
iliyofanyika 01 Septemba, 2014 kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Inclusive Development
Promoters and Consultants ya Dar es Salaam, Bw. Kaganzi Rutachwamagyo akisoma
taarifa ya hoja zao walizoziwasilisha mbele ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la
Katiba wakati wa mkutano na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu
(SHIVYAWATA) iliyofanyika 01 Septemba, 2014 kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa mjini
Dodoma.
Baadhi ya wanachama wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu
(SHIVYAWATA) wakifuatilia mada katika mkutano hiyo iliyofanyika 01 Septemba,
2014 kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifutilia mada ya mkutano
hiyo iliyofanyika 01 Septemba, 2014 kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu
(SHIVYAWATA) Bw. Felician Mkude (kushoto) akikabidhi taarifa kwa Mwenyekiti wa
Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta wakati wa mkutano iliyofanyika 01
Septemba, 2014 kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye
Ulemavu (SHIVYAWATA), Bi. Amina Mollel akichangia mada wakati wa mkutano
iliyofanyika 01 Septemba, 2014 kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma. Picha zote na Benedict
Liwenga, Maelezo-Dodoma
********************************
Na Benedict Liwenga,
Maelezo-Dodoma
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta amewahakikishia Watu wenye Ulemavu nchini
kuwa wanatendewa haki katika Katiba Mpya itakayopatikana.
Mhe. Sitta ameyasema hayo leo Septemba Mosi, 2014 katika
mkutano wake na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye
Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) ambalo lilikuja katika Bunge Maalum kwa lengo la kuwasilisha
hoja zenye msisitizo kuhusu haki za watu wenye ulemavu katika mchakato Katiba
Mpya.
Mhe. Sitta amesema kuwa kazi wanayoifanya ya kuyapokea
makundi mbalimbali Bungeni hapo haina lengo la kuja na hoja mpya na kuziwasilisha katika Bunge hilo, bali ni
mawasiliano ya kawaida yanayohusu safari kutoka Rasimu Mpya ya Katiba mpaka
kufikia katika Katiba Mpya inayopendekezwa ipatikane.
“Jambo lolote lililoandikwa na binadamu halikosi kasoro,
katika Rasimu hii ya Katiba tumegundua inayomapungufu kadha wa kadha, kuna
baadhi ya maoni ambayo hayakuzingatiwa ndiyo maana tunayafanyia kazi ili yawemo
katika Katiba Mpya itakayopatikana,”.alisema Mhe. Sitta.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Inclusive Development
Promoters and Consultants kutoka Dar es
Salaam, Bw. Kaganzi Rutachwamagyo ambaye pia ni mwanachama wa Shirikisho hilo,amesema
kuwa Kikosi cha Ushauri kuhusu masuala ya watu wenye Ulemavu kimeweka
kipaumbele cha msisitizo wao ambao unajielekeza katika hoja za kuongeza masuala
ya mambo ya Muungano ambapo wamependekeza kuwa kwenye orodha ya Mambo ya
Muungano kuongezewe suala moja zaidi la Nane kwa mujibu wa Rasimu ya Pili ya
Katiba ambalo ni uratibu wa masuala ya haki, usawa na fursa na uwajibikaji kwa
watu wenye ulemavu kama jambo la Muungano.
Bw. Rutachwamagyo ameongeza kuwa hoja nyingine ya msisitizo
inahusiana na suala la uanzishwaji wa chombo cha uratibu wa haki, usawa wa
fursa na uwajibikaji wa haki za watu wenye ulemavu ambayo hii ni kwa mujibu wa
Ibara ya 33 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu na Mkataba
mwenza wa nyongeza iliyoridhiwa kwa pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na amesema kuwa wanataka chombo hiko kijulikane kama Tume ya Kitaifa Juu ya
Haki, Usawa wa Fursa na Uwajibikaji kwa Watu wenye Ulemavu.
Aidha, Bw. Rutachwamagyo amegusia pia juu ya hoja nyingine inayohusu
suala la Uwakilishi wa watu wenye ulemavu kwenye Bunge la Tanzania, Baraza la
Wawakilishi, Mabaraza ya Madiwani utamkwe na Katiba na ukokotolewe kwa misingi
ya asilimia badala ya kuweka idadi mahsusi.
“Mathalani, tunapendekeza kifungu 113 kisomeke kuwa asilimia
5% ya Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watakuwa ni watu
wenye ulemavu wakiwakilisha kundi hili na watapatikana kwa kuchaguliwa na
wahusika wenyewe,” alisema .
Aliongeza kuongeza kwa kuzitaja hoja nyingine ikiwemo suala
la matumizi ya lugha sanifu kwa muktadha wa watu wenye ulemavu na amesema kuwa
kuna hali ya matumizi ya misamiati na islahi ambazo zinakinzana na dhana za
walemavu kimataifa hivyo ni vema kukawa na tafsiri sahihi ya majina kwa watu
hao ili kuepuka kukinzana huko, aidha amegusia pia suala la Hifadhi ya jamii
huku akifafanua kuwa wadau wenye ulemavu nchini wanadai kuwepo kwa ibara maalum
ndani ya Katiba inayoelekeza masharti ya upatikanaji wa hifadhi ya jamii kwa
watu wenye Ulemavu ikiwa ni pamoja na kulipwa gharama ama kupewa unafuu ya
kupunguza makali ya walemavu kwa mujibu wa ibara ya 28 ya Mkataba wa Haki za
Watu wenye Ulemavu ya 2006.
Akiongea kwa niaba ya watu wenye ulemavu, Mhe. Amon Mpanjo ambaye
ni mjumbe wa Bunge hilo amemuomba Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba kuunga
mkono sio kupokea maoni mapya, bali kuyaboresha yale yaliyokwisha wasilishwa
hapo awali.
“Tukuombe Mwenyekiti ulisisitizie Bunge letu Maalum la Katiba
liweze kuzingatia haki za watu wenye Ulemavu ili nao wapate kuwa na maisha bora,”
alisema Mpanjo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa SHIVYAWATA, Bi. Amina Mollel
amesisitiza juu ya hitaji la wanawake la hamsini kwa hamsini na kati ya hizo,
asilimia 5% wawe ni wabunge walemavu na ameitaka Tanzania kuwa mfano wa kuigwa
kwa kutoa nafasi nyingi za uongozi kada
mbalimbali kwa walemavu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: