Posted by
khamisimussa77@gmail.com
at
12:33 AM
Pendekezo la Rasimu ya Katiba kuwa
wabunge walau wawe na elimu ya kidato cha nne limetupiliwa mbali na
wajumbe wa Bunge Maalumu, baada ya Kamati karibu zote kulikataa.
Kamati hizo zimependekeza kigezo cha elimu kuanzia walau kidato cha nne
kama sharti muhimu la mtu anayetaka kugombea Ubunge kiondolewe, badala
yake mgombea ama ajue tu kusoma na kuandika, au ajue kusoma na kuandika
Lugha ya Kiswahili au Kiingereza kama ilivyo kwenye Katiba ya sasa.
Mbali na pendekezo hilo, kamati hizo zimegawanyika kuhusu Ibara ya 129
ya Rasimu ya Katiba inayowapa wananchi nguvu ya kumuondoa mbunge wao
madarakani kabla ya miaka mitano kumalizika.
Hayo yalijitokeza bungeni Dodoma jana, wakati kamati hizo zikiwasilisha
taarifa zake kuhusu Sura ya 9 na 10 ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa
bungeni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akiwasilisha maoni ya Kamati Namba 10, Mjumbe wa kamati hiyo, Dk Dalaly
Kafumu alisema suala la kugombea nafasi yoyote ni la kidemokrasia, hivyo
haipaswi mtu yeyote kuzuiwa kwa kigezo cha elimu.
“Haki ya kuamua iwapo mgombea anafaa au hafai ni ya wapigakura.
Wasizuiwe kikatiba kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua mtu
wanayemtaka,”alisema na kuongeza:
“Utaratibu huu haupo duniani kote hata nchi zilizo na demokrasia
iliyokomaa. Hivyo ibara hiyo isomeke tu ajue kusoma na kuandika na si
kiwango cha elimu kama sifa ya msingi.”
Mapendekezo hayo yaliungwa mkono na Kamati Namba 8 kupitia kwa Mjumbe
wake, Juma Alawi aliyesema kuweka kiwango cha elimu kwa wagombea ubunge
ni ubaguzi.
Kuondolewa kwa kigezo cha elimu ya kidato cha nne pia kumeungwa mkono na
kamati namba 10, 4, 12, 9 na 12 za Bunge hilo zilizowasilisha taarifa
zake jana asubuhi.
Kamati namba 12 ndiyo iliyokwenda mbali zaidi na kudai kuwa ibara hiyo
itasababisha ubaguzi kulingana na elimu wakati kiwango cha chini cha
elimu kwa Tanzania Bara ni darasa la saba na Zanzibar ni darasa la 10.
Hata hivyo, ni Kamati Namba 2 tu inayoongozwa na Shamsi Vuai Nahodha
iliyokubali pendekezo la Rasimu la kutaka kuwapo kigezo cha elimu.
Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, Vuai alitaka ibara hiyo ifanyiwe
marekebisho na kufuta maneno “anajua kusoma na kuandika Kiingereza na
Kiswahili” na badala yake isomeke, “ana elimu isiyopungua kidato cha
nne”.
Wakati kamati karibu zote zikikubaliana kuhusu kuondoa kigezo cha elimu
katika kuwania ubunge, zimetofautiana kuhusu Ibara ya 129 ya inayowapa
wananchi nguvu ya kumuondoa mbunge wao asiyewajibika kwao.
Mapendekezo ya Tume ya Jaji Warioba yalitaka wananchi wawe na haki ya
kumuondoa mbunge, endapo ataunga mkono sera zinazokwenda kinyume na
masilahi ya wapigakura wake au iwapo atashindwa kutetea kwa dhati hoja
zinazotokana na kero zao au ataacha kuishi au kuhamisha makazi yake
kutoka jimbo lake kwa miezi sita bila sababu.
Kamati Namba 12 iliafiki wananchi kupata nguvu hiyo ya kumuondoa mbunge
endapo tu atakuwa ameunga mkono sera ambazo zinakwenda kinyume na
masilahi ya taifa na si ya wapiga kura waliomchagua.
“Kimsingi hakuna namna bora ya kumtathmini mbunge kuwa ameshindwa
kutekeleza na kutetea hoja na kero za wapigakura,” alisema Jaffo kwa
niaba ya kamati.
Kamati namba 8, 2, 10, 4 na 9 zilipendekeza ibara hiyo ifutwe isipokuwa
kamati namba 9 iliyoenda mbali zaidi na kupendekeza kutungwa kwa sheria
ya kumdhibiti mbunge anayeshindwa kutekeleza majukumu yake.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe walio wachache katika kamati zao walipendekeza ibara hiyo ibaki kama ilivyo kwenye Rasimu.
Maoni ya kamati mbalimbali za walio wachache waliounga mkono kubaki kwa
ibara hiyo yalisomwa na Dk Tulia Ackson na Elizabeth Minde ambao wote
ni wanasheria kitaaluma.
Wakati huo huo, suala la kuwapo au kutokuwapo kwa Mahakama ya Kadhi
katika Katiba Mpya jana liliibuka tena Bungeni baada ya wajumbe walio
wachache kutaka liingizwe kwenye Katiba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: