AZAM FC YAINGIA MKATABA WA UDHIMINI NA NMB, YAKADIRIWA KULAMBA BILIONI 1

Mwenyekiti wa Azam fc, Said Muhammad Said (wa pili kulia) akipokea jezi mpya kutoka NMB
Na Baraka Mpenja, 
BENKI ya NMB imeingia mkataba wa udhamini wa miaka miwili na mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc, utaohusisha gharama za usafiri na baadhi ya nyingine za uendeshaji wa timu.
Mwenyekiti wa Azam fc, Said Muhammad Said amewaambia waandishi wa habari leo makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo, Azam Complex, Mbande, Chamazi, nje ya jiji la Dar es salaam kuwa mkataba huo utaanza utekelezaji mara moja.“Tumeupokea kwa furaha mkataba huu na tunapenda kuwashukuru NMB kwa kuungana nasi”. Alisema Said.
Naye katibu mkuu wa Azam fc, Nassor Iddrisa ‘Father’ alifafanua kuwa NMB watanufaika na mkataba huo kwa kutangaza nembo yao katika jezi za Azam fc, mabasi ya Azam fc na kuweka mabango katika uwanja wa Azam Complex.
Pia Azam watavaa jezi zenye nembo ya NMB kuanzia mazoezini na katika mechi za ligi kuu na mashindano ya kimataifa.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa NMB, Mark Weissing amesema mafanikio ya Azam fc ndio chachu ya kuingia ushirikiano na timu hiyo.
Azam fc inakuwa timu ya pili kuingia mkataba na taasisi ya kifedha nchini ambapo timu ya kwanza ni Simba ambayo iliingia mkataba na NMB mwaka 2004, lakini 2004 walitemana.
Pia NMB iliwahi kuidhamini timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa stars kati ya mwaka 2007 na 2010 ikiwa chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo ambaye kwasasa ni kocha mkuu wa Yanga sc.
Wakati wa utiaji saini wa mkataba baina ya Azam fc na NMB, watu wengi walikuwa na hamu ya kujua una thamani gani.

Hata hivyo viongozi wa Azam fc waligoma kutaja thamani ya mkataba huo, lakini taarifa za uhakika zinasema mkataba huo unakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi za Kitanzania Bilioni 1.
Imeelezwa kuwa kwa kila mwaka Azam fc watanufaika na shilingi milioni 500 za Kitanzania kutoka NMB.
Tangu imeanzishwa mwaka 2004 ba kupanda ligi kuu 2008, Azam fc inapata mdhamini kwa mara ya kwanza .
Azam fc inakuwa miongoni mwa timu chache za Tanzania zinazonufaika na udhamini.
Simba na Yanga ndio timu pekee zilizokuwa zinanufaika na udhamini, kwa miaka mingi, lakini siku za karibuni Mbeya City walivuna milioni 360 kutoka kwa Binslum.
Udhamini ni moja ya vyanzo vya mapato kwa klabu za mpira wa miguu, lakini imekuwa changamoto kwa timu mbalimbali kufikia mafanikio ya kupata wadhamini.
Siku zote mdhamini anawekeza sehemu anayoweza kunufaika, hivyo sio rahisi kuweka fedha kwenye timu yenye kiwango kibovu.
Kilio cha kukosa udhamini kwa timu za ligi kuu kinasikika kila kukicha, lakini zimeshindwa kutegua mtego huo tofauti na Azam fc na Mbeya City.
Hakuna haja ya kulia kwa kukosa udhamini, ukiucheza mpira kwa nafasi uliyopata  na kufanikiwa kama Mbeya City, Azam fc, Yanga, na Simba, mabilioni na mamilioni yatakuja yenyewe.
Mafanikio ya Azam fc yamewafanya walambe mabilioni kutoka NMB, na timu nyingine zinatakiwa kujipanga kwa kutafuta mafanikio uwanjani zaidi ya kulia kila wakati.

0 comments: