Posted by
khamisimussa77@gmail.com
at
12:24 PM
Baada
ya kuona kuwa kuna maeneo mbalimbali ya vivutio vya kitalii muhimu na
ambavyo vimesahaulika kwa njia moja au nyengine na pengine hakuna pa
kuvitangaza ili watanzania na Dunia kwa ujumla wapate kuvifahamu kwa
ukaribu , Tone Multimedia Group kupitia
mtandao wake wa Mbeya yetu Blog wameamua kuanza rasmi kuvitembelea na
kutangaza kwa Jamii kwa ujumla wapate kuvifahamu ili nao waje
kuvitembelea.
Safari
hiyo ambayo moja kwa moja ilianzia Mkoa wa Mbeya Wilaya ya
Rungwe-Tukuyu kwenda kujionea vivutio hivyo mbalimbali kikiwepo cha
kwanza kabisa ambacho ni Kijungu eneo ambalo ni la kipekee na lenye
historia ya aina yake.
Hivi ndivyo safari ilivyokuwa Fuatilia hapa kwa makini.
Kwanza
kabisa tulifika katika kibao hiki ambacho kimetoa maelezo ya awali
ikiwa ni pamoja na Bei ambazo mtu anatakiwa kutozwa wakati anapotaka
kuingia katika eneo hilo, Bei hizo zimewekwa na uongozi wa Serikali ya
Kijiji ambapo fedha hizo zinasaidia katika mambo mbalimbali za
kuendeleza kijiji hicho ingawa hata hivyo kuna changamoto kadha wa kadha
ambazo zinawakabili ikiwa ni pamoja ni Gharama kubwa za kuingia katika
eneo hilo kwa wazawa ambapo haichagui kwamba umetoka nje ya nchi au
ndani Jambo ambalo Serikali inapaswa kutazama kwa sababu ni zaidi hata
ya kuingia katika Hifadhi za Taifa.
Picha hii ilipigwa kwa juu kabisa kuonesha Jinsi eneo la Kijungu linavyo onekana
Hapa
ni eneo ambalo Maji ya mto huo yanatokea katika eneo linaitwa Namba One
eneo la ukanda wa juu kabisa wa eneo hilo, Majihayo pamoja na mengine
mengi hata wakati wa mvua kubwa ni lazima yazunguke yanapo kwenda lakini
mwisho wa siku ni lazima yaishie hapa, Pia hapa ndipo maji haya
yanapoanza kutililikia moja kwa moja katika kijungu.
Maji
hayo sasa huingia katika eneo hili la kijungu, Wamekiita jina la
kijungi kwa sababu kubwa kuwa eneo hilo lipo kama chungu, Maji hayo hata
yakiwa na kasi kiasi gani, hata yawe mengi kwa namna gani hayawezi
kujaa katika Kijungu hiki, Pia kijungu hiki hakuna mtu aliyekijenga bali
ni maajabu tuu ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu, hilin eneo limeumbwa kwa
miamba ya mawe yanayofanana na Chuma kigumu. Maji haya yakishafika hapa
huwa si mwisho kuna eneo yanaelekea..kwa hakika ni maajabu na kama huna
wazo la kutembelea ni wakati wako sasa.
Kulia ni upinde unao onekana kutokana na kasi ya maji, upinde huu ni kivutio kikubwa hasa wakati wa jua kali huonekana vizuri
Tulipo
wasili katika eneo hilo la kijungu tulipata wasaa wa kuongea na Mzee
mmoja wa zamani sana ambaye kwa hakika yeye alikiona kijungu zamani sana
miaka yani miaka ya 1933 , mzee huyo ambaye anatambulika kwa jina la
Elia Kabadhasya aliye zaliwa mwaka 1927 alieleza kwamba alikijua
kijungu hiki wakati alipokuwa akitafuta sehemu ya Kunyweshea Ng'ombe
Maji ndipo aliposhuka eneo hili na kukiona Kijungu hiki, hata hivyo
wakati anawanywesha maji Ng'ombe wake kwa bahati mbaya moja kati Ng'ombe
hao alitumbukia ndani ya kijungu hicho na kupotea moja kwa moja. Wa
kwanza kutoka kushoto ni Joseph Mwaisango Mwandishi mkuu wa Mbeya yetu
Blog na wa Kwanza kutoka kulia ni Fredy Anthony Njeje kutoka Tone
Multimedia group akiwa anachukua maelezo kwa makini ya Mzee Elia
Kabaghasya wa kati kati.
Baada
ya maji hayo yenye kasi ya ajabu kuingia katika kijungu hicho hutokea
katika eneo hili ambapo yanaonekana meupe na yenye mapovu . hii ni
kutokana na sababu ya kwamba yanakuja kwa kasi na kufikia hapa, baada ya
kufika hapa mbele kunaonekana kwamba kuna uwazi, uwazi huu kwa mujibu
wa wanakijiji wanaotokea eneo hili wanasema kwamba maji haya huingia
hapa katika uwazi ambao unakadiliwa kuwa na urefu kwa Kilometa moja
husafiri huko na baadae hutokea katika upande mwengine ambapo ukitazama
vizuri katika picha hiyo kwa mbele ya haya maji kuna maji yamepoa hayana
kasi hapo ndipo yanapo tokea, hakuna yanapo kutana haya maji mpaka
yaingie pangoni ndio yatokee upande wa pili, hii itaonekana katika picha
inayofuatia, hili ni moja ya ajabu kwa sababu waweza dhania haya maji
yanakutana kumbe hayakutani hata kidogo.
Picha
hii inaonesha vizuri na ni mwendelezo ya wa maelezo ya maji hayo hapa
kama inavyo onekana upande wa juu ni kijungu maji ambapo yanaingilia
hapo kisha yanatokea upande huo wa pili yanapoonekana meupe sana na povu
kutokana na povu kisha yanaingia katika pango hilo linalokadiliwa kuwa
na Kilometa moja kisha yanatokea upande wa pili hapo yanapo onekana kama
yamepoa kisha kuendelea na safari , Cha ajabu maji hayo hayakutani hata
kidogo.
Fredy
Anthony Njeje Kutoka Tone Multimedia Group ambao ni wamiliki wa Mtandao
huu wa Mbeya yetu wa upanda wa kulia akipata maelezo zaidi ya Kina
kuhisiana na Kijungu hiki kutoka kwa Mzee Elia Kabaghasya mwenye umri wa
Miaka 87 sasa mzee mwenye nguvu na ambaye anajua historia nzima ya
eneo hili la kijungu alieleza kwamba hili ni eneo zuri sana la utalii
ambapo aliwataka watu wengi zaidi waje kutembelea katika eneo hili na
kujionea mambo mengi zaidi na Maajabu ya Mungu ya eneo hilo la kipekee
ambalo kwa Tanzania hata kwa Dunia ni hapo tuu ndipo papo hivyo,
Alieleza zaidi kwamba maji hayo ya mto huo hutumika zaidi kwa ajili ya
kunyweshea mifugo, na kufulia tuu hayatumiki kwa kazi zengine. Alitoa
wito kuwa watu wanatakiwa kuwa makini wanapokuja kutembelea eneo hilo na
kuchukua tahadhali kama maeneo mengine kwa kuwa mtu anaweza teleza
ingawa eneo hilo kuna wataalam na watu maalum wa kuwaongoza. alimalizia
kwa kusema kuwa kuna haja ya Serikali kukiboresha Kivutio hiki cha
Kijungu.
Mmoja
wa wanakijiji ambao wanaishi katika eneo hilo akipita njia kati kati ya
Kijungu hicho na kusema kwamba zamani kutokana na imani za mababu zetu
ilikuwa ili upite ni lazima utumbukize kitu chini ndio upate kupita
hapo, lakini kadili siku zinavyozidi kwenda na hivi miaka ya karibuni
imani hiyo imetoweka na mtu anaweza kupita bila shida, pia alisema
kwamba katika eneo hilo mtu anapokatiza katika mwamba huo katikati
anatakiwa aanze kutanguliza mguu wa kulia kwanza ndio anaweza akavuka.
Mwisho alisema kwamba ukivuka upande wa pili unatokea moja kwa moja
mpaka Uporoto ingawa ni parefu hivyo mababu zetu ndio njia walikuwa
wakipita enzi hizo.
Kikosi kazi cha Mbeya yetu kazini
Mzee Elia Kabaghasya (87) akionesha eneo ambalo anaishi halipo pichani kuwa maji hayo yamefika mpaka eneo hilo nyumbani kwake.
Kutoka
kushoto ni Joseph Mwaisango akiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya
waliofika eneohilo ambao ni Doreen, Ruby, Happy na Eric kufanya utalii
wa ndani.
******
Inawezekana
umehamasika na unataka na wewe kufika katika eneo la Kijungu kujionea
wewe mwenyewe kwa macho yako na haya ndio maelekezo.
Namna ya kufika
Kutoka
Mbeya Mjini hadi Sehemu moja inaitwa KK Wilaya ya Rungwe-Tukuyu ni
zaidi ya Kilometa 50 , Baada ya hapo kuna njia ambayo inakatiza upande
wa kulia kuelekea Chuo cha Magereza, Ukifika Chuo cha Magereza ndani
utapata maelekezo yote ya namna utakavyofika, Muhimu kufuata taratibu
maana ni eneo la Jeshi la Magereza kuna sheria zake.
MAONI
Baada
ya kutembelea na kujionea wenyewe tulikuwa tunaomba Serikali iangalie
swala zima kwanza la Afya za hawa wanaotembelea katika Kivutio hiki cha
kitalii, kwamba hakuna sehemu ya watu kijisaidia-Choo hivyo inawalazimu
watu wajisadie hovyo hovyo katika vichaka jambo linalosababisha uchavuzi
wa mazingira na pengine inaweza sababisha mripuko wa magonjwa, Hilo ni
swala muhimu.
Pili
ni swala la mapato tumejionea kwamba kwanza hakuna Risiti inayotolewa
wakati watu mbalimbali wanaenda kutembelea katika kivutio hicho cha
Kijungu, Kila mtu anajiwekea bei zake ingawa wameweka Bei ya kutazama
pale ni Tsh 5,000 kwa mtu ambapo hicho ni kiasi kikubwa kwa wazawa na
inabidi hapa paangaliwe, na kwamba mwanakijiji yoyote ambaye yupo eneo
hilo ndiye anayetoza watu, utaratibu huo unatakiwa kuangaliwa na
kutengenezwa vizuri na kurekebisha viwango hivyo kwani watu wanapenda
kuona lakini wanashindwa, Pia mapato hayo yanaonekana hayana msaada
wowote kwa wakazi wa eneo hilo.
Tatu
ni Miundombinu ya eneo hilo, ambayo inatakiwa kuboreshwa zaidi hasa
eneo la kuingilia hapo Serikali itazame waweke hata ngazi kuanzia eneo
la kuingilia mpaka hapo katika Kijungu ili watu waweze kufika kiurahisi
Mwisho
Serikali iangalie jinsi gani wanaweza kuweka Ofisi ili hata watu
wanapofika waelewe kabisa kwamba sasa wamefika katika kijungu na kupata
maelekezo yote ya awali kabla ya kwenda katika eneo la tukio.
Ikiwa unapenda kujua na kuungana nasi katika mpango huu wa kutangaza vyanzo hivi muhimu wasiliana nasi kwa namba +255 754 374 408 au +255 765 056 399
Imeandaliwa
na Tone Multimedia Group kupitia Mtandao wake wa Mbeya yetu Blog, Huu
ni Mwanzo bado kuna Mengi sana usikose Kujua juu ya Maporomoko ya Kaporogwe ambapo ndipo tutawaletea hapa usikose.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: