KESI YA KIFO CHA KANUMBA SURA MPYA.. ELIZABERTH MICHAEL HALI TETE

Jipya! Baada ya kimya cha muda mrefu, imefichuka kwamba kesi ya kuuawa kwa aliyekuwa staa mkubwa wa sinema za Kibongo, marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’ imechukua sura mpya baada ya kuanza kusikilizwa kimyakimya, Ijumaa Wikienda limenasa kinachoendelea.

Staa wa sinema za Kibongo, Lulu Elizabeth Michael, 'Lulu".
WATU WANATAKA KUJUA KINACHOENDELEA
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba watu wengi wana kiu ya kujua kinachoendelea katika kesi hiyo ambapo ilidaiwa kwamba imehamishwa eneo la wazi (open) na kusikilizwa kimyakimya katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, huku usikilizwaji wa kesi hiyo ukiwa tofauti kama ilivyozoeleka.
Kwa mujibu wa shushushu wetu anayependa kufuatilia maisha ya mastaa wa tasnia tofautitofauti Bongo ndani ya mahakama hiyo, chombo hicho cha kusimamia sheria kimeamua kubadili aina ya usikilizaji wa kesi hiyo.
Wakili maarufu Bongo anayemtetea 'Lulu', Peter Kibatala.
YAHAMISHIWA BARAZA LA KESI ZA MAUAJI
Habari zilieleza kwamba, kwa sasa kesi hiyo itakuwa ikisikilizwa kwenye kikao cha baraza la kusikiliza kesi za mauaji kwenye mahakama hiyo, kwa lugha ya kigeni kinaitwa High Court Murder Session.
“Kama ukienda pale mahakamani ili kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo, huwezi kufanikiwa kupata chochote kwa sababu ipo kwenye baraza la kusikiliza kesi za mauaji yaani High Court Murder Session ambalo huwa linasikiliza kesi kimyakimya tofauti na kesi nyingine zinazosikilizwa kwenye kizimba,” kilisema chanzo chetu hicho.
ETI LULU HAJUI KINACHOENDELEA
Uchunguzi wetu ulibaini kwamba wakati hayo yakiendelea kortini hapo, aliyekuwa mwandani wa Kanumba aliyekuwa naye chumbani siku ya kifo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ hajui chochote kinachoendelea na wala hajaitwa mahakamani.

Mama mzazi wa marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa.
“Tangu imeanza kusikilizwa hakuna siku Lulu ameitwa na sidhani kama anajua kinachoendelea.
“Labda anayejua kinachoendelea ni mama Kanumba (Flora Mtegoa) ambaye hupenda kuulizia kuhusu hatima ya mwanaye,” kilisema chanzo hicho.
WAKILI KIBATALA ANASEMAJE?
Baada ya kujikusanyia data hizo, Ijumaa Wikienda lilimtafuta wakili maarufu Bongo anayemtetea Lulu, Peter Kibatala ili kupata ufafanuzi wa aina hiyo ya usikilizwaji wa kesi ya mteja wake ambapo alifichua siri hiyo juu ya kesi ya kifo cha Kanumba.
Wakili Kibatala alikiri kwamba kesi ya kifo cha Kanumba ambayo Lulu ni mshitakiwa wa kwanza akituhumiwa kuua bila kukusudia, imebadilishwa aina ya uitwaji huku akigoma kuingia kiundani kwani bado kesi hiyo ni mbichi na hairuhusiwi kwa wakili kuzungumza nje ya mahakama.

Aliyekuwa staa mkubwa wa sinema za Kibongo, marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’ enzi za uhai wake.
“Ni kweli inaitwa hivyo, huyo aliyekueleza hajakosea na tunategemea mwezi huu wa nane kikao cha baraza hilo la usikilizaji kitaendelea lakini nisingependa kuongea sana kwani mimi siyo msemaji wa Lulu bali ni wakili na si maadili ya kazi yangu kuzungumza nje ya mahakama. Hata Lulu haruhusiwi kuzungumza chochote nje ya mahakama,” alisema Kibatala aliyewahi kuwa wakili wa mwigizaji Kajala Masanja na mwanahip-hop, Waziri Makuto ‘Lord Eyez’.
TUMGEUKIE LULU
Mwanahabari wetu alipomtafuta Lulu ili kujua kama anajua chochote juu ya kesi hiyo, mkali huyo wa sinema za Kibongo aligoma kuzungumza chochote kama aliyoelekezwa na wakili wake, Kibatala.
TUJIKUMBUSHE
Kanumba aliyewatoa mastaa wengi wa filamu unaowaona kwa sasa, alifariki dunia April 7, 2012 nyumbani kwake, Vatican-Sinza jijini Dar. Kifo cha Kanumba kilidaiwa kwamba kilitokana na kuangukia sehemu ya nyuma ya kichwa ambapo alipata mtikisiko wa ubongo kisha kuzikwa kwenye Makaburi ya Kinondoni, Dar.

0 comments: