ZAIDI ya wanafunzi 500 waliochaguliwa kujiunga na kidato
cha kwanza katika Shule mbali mbali za Sekondari Wilayani Chunya Mkoani Mbeya
wameshindwa kuripoti Mashuleni kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo kujiingiza
katika biashara za uchimbaji wa Madini na Uvuvi.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus
Kinawiro, amewataka Wazazi wa Wanafunzi hao kuhakikisha wanawapeleka watoto wao
Shuleni haraka kabla ya kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa mzazi atakayekaidi
agizo hilo.
Kinawiro aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza
na wananchi wa Kitongoji cha Majengo kata ya Sangambi Wilayani humo baada ya
kupokea taarifa kutoka kwa Afisa elimu wa Wilaya kuhusu kukithiri kwa utoro wa
wanafunzi mashuleni, Hivyo kuifanya Serikali kushindwa kufikia malengo yake ya
kufuta ujinga miongoni mwa wananchi.
Alisema Wilaya ya Chunya inakabiliwa na Wimbi kubwa la
wafugaji wenye tabia ya kuhamahama jambo ambalo husababisha kuwakatisha masomo
wanafunzi ili hali wengine wakijikita kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na
uvuvi katika Ziwa Rukwa.
Alisema kufikia Mwishoni mwa mwezi huu mzazi yeyote
ambaye hatampeleka Mwanaye Shule bila kujali kisingizio cha aina yoyote
atakamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kumwachisha masomo
mwanafunzi na kumpatia ajira kinyume cha Sheria.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema Idadi ya watoto 500 ni kubwa
sana hivyo hali hiyo ikiachwa itazalisha Wajinga wengi jambo ambalo litakuwa
mzigo kwa taifa kutokana na wengine kuwa majambazi baada ya kukosa fedha
kutokana na ajira walizojiingiza katika umri mdogo na kukwamisha juhudi za
Serikali za kujenga Shule katika kila kata.
Kinawiro alisema Wilaya ya Chunya kitaaluma inafanya
Vizuri katika ngazi ya Mkoa ukilinganisha na Wilaya zingine hivyo hayuko tayari
kuona sifa hiyo inapotea kutokana na wazazi wachache kuzembea na kutokujua
umuhimu wa kumsomesha mtoto, na kuongeza kuwa Halmashauri inaunga mkono juhudi
za Serikali kwa kuimarisha ujenzi wa Mabweni ili kuhakikisha watoto wa kike
hawakatizwi masomo kutokana na mimba zisizotarajiwa.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wafugaji
wote waliohamia Wilayani Chunya kinyume cha Sheria kuondoka mara moja na atakae
kaidi agizo hilo atakumbana na Operesheni kubwa ya kuwaondoa kwa nguvu ambapo
kwa sasa wanafanya doria kwa kutumia ndege maalumu ili kuwabaini wahamiaji
hao.
Alisema zoezi hilo litafanyika hivi karibuni baada ya
kumalizi kuwabaini wafugaji waliovamia misitu na sehemu za hifadhi ambapo
wanaharibu kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mifugo ambayo huharibu mazingira
ya Chunya kwa Ujumla.
Hivi karibuni kulifanyika zoezi la kuwaondoa wafugaji
waliovamia msitu wa hifadhi wa kijiji cha Mbangala ambapo Jumla ya mifugo 1000
ilikutwa msituni humo na kufanyika uharibifu mkubwa lakini zoezi hilo
liliingiliwa na hitilafu baada ya wafugaji hao jamii ya Wamang’ati kuwashambulia
kwa mishale na mikuki maofisa pamoja na Askari wa Jeshi la Polisi waliokimbia
kunusuru maisha yao.
Na
E . Kamanga Chunya
|
0 comments: