National Arts Council BASATA
Wasanii nchini wametakiwa kuwa
mstari wa mbele kuhamasika na kushiriki kikamilifu kwenye maazimisho ya
Siku ya Msanii maarufu kama Msanii Day ambayo yanatazamiwa kufanyika
mwezi Desemba mwaka huu wa 2015 jijini Dar es Salaam na maeneo
mbalimbali nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye programu maalum ya
kujadili ushiriki wa wasanii kwenye siku hii muhimu kwao marais wa
mashirikisho ya wasanii nchini walisema kwamba wakati umefika kwa
wasanii wote nchini kuamka na kuwa mstari wa mbele kutambua maazimisho
haya ya siku yao kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakitumiwa katika
kuazimisha vilele vya tasnia zingine.
“Tumekuwa tukitumika sana sisi Wasanii kung’alisha na kuzifanya
kazi za wengine kuwa na mafanikio, tumekuwa tukihamasisha kazi za
wengine. Hii siku ya Msanii ni yetu, tuamke, tuibebe zaidi ya
tunavyofanya kwenye kazi za wengine. Tuungane tuifanye siku hii yenye
tija” alisisitiza Symon Mwakifamba ambaye ni Rais wa shirikisho la Sanaa
za Filamu nchini.
Aliongeza kusema kwamba, Wasanii wana nguvu na mchango mkubwa
katika jamii na kwamba kwa idadi yao wanatosha kabisa kuwa na uwakilishi
katika maeneo mbalimbali ya maamuzi ili kuhakikisha hawaachwi nyuma.
“Naomba wasanii wote tuitumie siku ya Msanii kuonesha nguvu
yetu, tuwaoneshe na tutume ujumbe kwa viongozi kwamba kundi hili ni
kubwa na muhimu katika kujenga Taifa lenye ustawi” Aliongeza Mwakifamba.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Adrian
Nyangamale alisema kwamba siku ya msanii ni mahsusi kwa ajili ya wasanii
wote nchini na kwamba kama ilivyo kwa maadhimisho ya siku zingine kama
za walemavu, wanawake, wanasheria na nyinginezo wasanii nao hawana budi
kuhakikisha wanaifanya siku hii kuwa yenye kufana na mafanikio makubwa.
“Hauwezi kuizungumzia siku ya Msanii bila kuwataja na
kuwahusisha wasanii moja kwa moja. Wasanii lazima tujiunge pamoja na
tushirikiane kwa dhati ili kuifanikisha siku hii” Alisisitiza
Nyangamale.
Awali viongozi wa mashirikisho ya Wasanii nchini Msule Jumanne
(Sanaa za Ufundi), Samwel Mbwana (Sanaa za Muziki), Dennis Mango (Sanaa
za Maonesho) na Biko wa Sanaa za Filamu walieleza namna wasanii
walivyojipanga kushiriki siku hiyo na kusisitiza kwamba kila msanii
nchini ajisikie furaha na heshima kushiriki siku hii muhimu kwao.
Siku ya msanii Tanzania inatarajiwa kuanza kuazimishwa kwa
shamrashamra mbalimbali yakiwemo maonesho ya kazi za wasanii, semina na
makongamano ya kujadili mustakabali wa sekta hiyo nchini kuanzia tarehe
7-11 Desemba mwaka 2015 na baadaye kilele chake tarehe 12 Desemba mwaka
2015 kwenye Ukumbi wa Blue Pearl uliko jengo la Ubungo Plaza Ubungo
jijini Dar es Salaam.
IMETOLEWA NA KITENDO CHA HABARI NA MAWASILIANO, BASATA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: