Friday, November 25, 2016

RAIS ROUHANI: MAUAJI YA WAFANYA ZIARA IRAQ NI KITENDO CHA KINYAMA

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kitendo cha kinyama cha magaidi cha kuwaua shahidi Waislamu katika mji wa Hilla ambao walikwenda nchini Iraq kuzuru Haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein (as) kinaonesha upeo wa juu wa kubakia nyuma kwa wahalifu hao wenye nyoyo zilizopofuka.
Taarifa iliyotolewa na Rais Rouhani kuhusu uhalifu huo imelaani shambulizi la kigaidi lililotokea jana katika mji wa Hilla kwenye mkoa wa Babel nchini Iraq na kusema kuwa: Kufanyika kwa mafanikio hamasa ya Arubaini ya Imam Hussein bin Ali (as) ni sehemu ya adhama ya mapenzi ya mataifa ya Waislamu kwa kizazi cha Mtume Muhammad (saw), suala ambalo haliwezi kuvumiliwa na makatili wenye nyoyo zilizopofuka.
Taarifa ya Rais Rouhani imesema kuwa, shambulizi la kigaidi lililofanyika katika mji wa Hilla na kuua shahidi makumi ya Waislamu waliokwenda kuzuru kaburi la Imam Hussein (as) wakiwemo raia wa Iran, linawaumiza Waislamu wote hususan wafuasi na wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw).
Picha ya eneo lililoshambuliwa na magadi wa Daesh, Hilla
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ameitaka serikali ya Iraq kuwashughulikia ipasavyo watu waliotenda jinai hiyo na kutangaza kuwa Iran iko tayari kikamilifu kutoa ushirikiano na kuwasaidia watu waliopatwa na maafa katika tukio hilo. Amesema kuwa serikali ya Iran imeazimia vilivyo kufanya mapambano ya pande zote dhidi ya magaidi na makundi yenye misimamo ya kufurutu mipaka na kuongeza kuwa, hivi karibuni dunia itashuhudia ushindi wa mwisho wa taifa la Iraq katika mapambano yake na makundi ya kigaidi na waungaji mkono wao.
Mlipuko wa gari lililokuwa limetegwa mabomu katika kituo cha mafuta ya petroli katika eneo la al Shomali huko Hilla nchini Iraq umeua shahidi karibu Waislamu 100 waliokwenda kufanya ziara ya Imam Hussein na kujeruhi wengine zaidi ya 20. Makumi ya mashahidi waliouawa katika shambulizi hulo la kigaidi ni raia wa Iran.
Jeshi la Iraq baada ya kuwasili katika eneo la Shomali, Hilla
Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuwa, ndilo lililofanya mauaji hayo. Mji wa Hilla uko umbali wa kilomita 80 kutoka mji mtakatifu wa Karbala, sehemu lilipo kaburi la mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as) aliyeuawa shahidi na Yazid bin Muawiya mwaka 61 Hijria.

No comments:

Post a Comment