MBUNGE
wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge juzi aliokolewa kwa risasi katika
vurugu za kundi la wananchi, waliomvamia karibu na ofisi za Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Simiyu na kusababisha taharuki
katika ofisi za chama hicho.
Mmoja
wa watu waliokuwa kwenye gari la mbunge huyo wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), aliyekuwa na msafara wake kutekeleza shughuli za ubunge jimboni
mwake, ndiye aliyefyatua risasi hewani ili kutawanya umati huo.
Hata
hivyo, hali hiyo ilitafsiriwa na Chadema kuwa ni mkakati wa mbunge huyo
wa kuwafanyia fujo katika ofisi zao, hivyo kulifikisha suala hilo
Polisi ambako wamefungua jalada.
Madai
ya tukio hilo yaliyotolewa na John Heche, Mwenyekiti wa zamani wa
Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA), yamethibitishwa Jeshi la Polisi
ambalo limesema aliyefyatua risasi si Chenge, bali mmoja wa watu
waliokuwa kwenye gari lake.
Risasi Chadema
Akizungumza
jana, Heche alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 1:30 jioni
katika ofisi za chama hicho mkoa wa Simiyu zilizoko eneo la Salunda.
“Mara
baada ya kumalizika kwa Mkutano wa chama hicho uliohutubiwa na Naibu
Katibu Mkuu Chadema Tanzania Bara, John Mnyika baadhi ya wanachama
walipanda magari na wengine kutembea kwa miguu ili kwenda kwenye ofisi
zao za mkoa ambako watu walishtuka kumuona mbunge huyo akishuka katika
gari lake,” alianza kuelezea Heche.
Aliongeza
kuwa, wakati wakiendelea na kikao, magari mengine matano yanayodaiwa
kuwa ya msafara wa Chenge yalifika eneo la ofisi ya Chadema na kusimama
na huku gari moja la matangazo likipiga muziki wa `CCM’ kwa sauti kubwa,
huku mbunge huyo akidaiwa alishuka na kuanza kucheza.
“Kutokana
na kitendo hicho, mmoja wa walinzi wa Chadema aliwaomba waondoke eneo
hilo na pia waache kupiga muziki huo kwani kuna kikao cha ndani cha
viongozi wa chama hicho kinachoendelea lakini waligoma.
“Mara
lilifika kundi la wapenzi na wanachama wa Chadema na kuyazunguka magari
hayo na Chenge kuingia ndani ya gari ndipo risasi zilipopigwa kutoka
katika gari alilokuwemo Chenge ili kutawanya kundi hilo ambalo nalo
lilianza kuwashambulia kwa mawe na hivyo kusababisha taharuki na
kusababisha mkutano huo kuvunjika,” alisema.
Kutokana
na hali hiyo, viongozi wa Chadema mkoa wa Simiyu waliripoti tukio hilo
Makao Makuu ya Polisi wilaya ya Bariadi na kutoa malalamiko yao juu ya
tukio hilo na kufunguliwa faili namba BAR/ RB/1195/2015.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Gemini Mushi alikiri kutokea kwa tukio hilo,
lakini alisema kuwa aliyefyatua risasi si Chenge, bali ni kijana Ahmed
Ismail aliyekuwa katika gari la Mbunge huyo, ambaye pia ni Mwanasheria
Mkuu wa zamani na Waziri aliyeziongoza wizara kadhaa, zikiwemo Katiba na
Sheria na Miundombinu.
Kwa
mujibu wa Kamanda Mushi, Chenge alikuwa akitoka katika mkutano wa CCM
akienda nyumbani kwake kupitia Barabara Kuu moja iliyopo katika jimbo
hilo.
Alifafanua
kuwa wakati akienda nyumbani kwake, alikutana na watu waliozuia gari
lake barabarani, ambapo Chenge alitoka na kuzungumza nao huku wao
wakimshangilia.
Kamanda
Mushi alidai kuwa wakati Chenge akizungumza na wananchi hao, kulitokea
watu wengine kutoka ilipo ofisi ya Chadema ambayo haikuwa mbali na eneo
hilo, ambao walianza kurushia mawe msafara wa mbunge huyo na
kumlazimisha kuingia ndani ya gari lake.
Kutokana
na hali hiyo, Kamanda Mushi alidai kuwa Ahmed aliyekuwa ndani ya gari
la Chenge, alilazimika kupiga risasi tatu angani ili kutawanya wananchi
waliomsimamisha Chenge na kutoa nafasi ya mbunge huyo kupita.
Alipotakiwa
kueleza hatua zilizochukuliwa, Kamanda Mushi alisema alichokifanya
Ahmed si makosa kwa kuwa ndivyo watu wanaomiliki silaha, walivyoelekezwa
kwamba kunapotokea hatari wapige risasi angani kwa ajili ya kutoa onyo.
Alieleza
kuwa silaha hiyo, ingawa imechukuliwa na Polisi kwa uchunguzi zaidi,
lakini ilikuwa ikimilikiwa kihalali na Ahmed. Alifafanua kuwa hata baada
ya tukio hilo, Ahmed aliripoti Polisi kama taratibu zinavyopasa, kwamba
baada ya kutumia silaha, lazima taarifa zitolewe Polisi ikiwa ni pamoja
na kueleza idadi ya risasi zilizotumika.
Chenge
alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, alisema hawezi kulizungumzia, bali
Jeshi la Polisi ndilo lenye mamlaka ya kufanya hivyo, kwa kuwa tukio
hilo limesharipotiwa huko.
0 comments: