ONGEZEKO LA UTUMIAJI WA WANAWAKE WA KIAFGHANI KATIKA MAGENDO YA DAWA ZA KULEVYA
Posted by khamisimussa77@gmail.com at 12:57 PM
Msemaji wa Idara ya Kupambana na Magendo ya
Dawa za Kulevya nchini Afghanistan amesema kuwa kumekuwepo ongezeko la
utumiaji wa wanawake wa Kiafghani katika magendo ya dawa za kulevya.
Khaled Muvahhed ametaja umaskini, ujinga, matatizo ya kiuchumi
na kulazimishwa na watu wa familia kuwa ni miongoni mwa sababu za
wanawake wengi wa Afghanistan kujielekeza katika biashara haramu na
magendo ya dawa za kulevya. Ameongeza kuwa, katika miezi 11 iliyopita
askari usalama wa Afghanistan wamewatia nguvuni makumi ya wanawake kwa
tuhuma za kujihusisha na magendo ya dawa za kulevya.
Mbali na sababu zilizotajwa kuwa zinawasukuma wanawake wa Afghanistan
katika magendo ya dawa za kulevya, lakini pia inatupasa kusema kuwa,
suala hilo ni kielelezo cha kuongezeka sana uzalishaji wa dawa hizo
nchini Afghanistan na jitihada za magenge ya mafia ya utoroshaji wa dawa
hizo kwa ajili ya kupata njia mpya za biashara hiyo.
Mafanikio ya kiwango fulani ya serikali ya Afghanistan katika kufunga
baadhi ya njia za kusafirisha dawa za kulevya yameyalazimisha magenge
ya mafia ya mihadarati kutafuta njia mpya za magendo ya dawa hizo na
kulenga zaidi tabaka la wanawake. Suala hili, badala ya kuhusishwa na
serikali ya Afghanistan, linafungamana zaidi na sera za madola ya
kikoloni kama Marekani na Uingereza huko Afghanistan. Nchi hizo
zimetengeneza mazingira ya kustawisha zaidi uzalishaji wa dawa
za kulevya na magendo ya dawa hizo huko Afghanistan na kutatiza sana
uchumi wa nchi hiyo. Nchi hizo pia katika upande wa pili zinafanya njama
za kuangamiza jamii ya Afghanistan hususan kizazi cha vijana wa nchi
hiyo kupitia njia ya kuwatumbukiza katika uraibu wa mihadarati na ukweli
huo unathibitishwa na takwimu zinazosema kuwa, katika kipindi cha chini
ya miongo miwili ya udhibiti wa Marekani huko Afghanistan, zaidi ya
raia milioni tatu wa nchi hiyo wamekuwa wateja na waraibu wa dawa za
kulevya.
Mtaalamu wa masuala ya siasa wa Afghanistan, Sayyid Wahiid Dhuhuri Hussaini anasema: Marekani
na muungano wa kijeshi wa NATO unatumia jiografia ya Afghanistan kwa
ajili ya kukidhi mahitaji yao na kuhakikisha kwamba, dawa za kulevya
zinazalishwa nchini humo bila ya kizuizi chochote. Nchi hizo
zinasafirisha baadhi ya dawa za kulevya zinazozalishwa Afghanistan na
kuzipeleka katika nchi nyingi kwa ajili ya kudhamini mahitaji ya madawa
ya nchi za Marekani na Ulaya na jamii ya Afghanistan ndiyo inayodhurika
na kupata hasara kubwa zaidi kutokana na dawa hizo za kulevya."
Marekani na Uingereza ambazo ndizo zinazodhibiti hali ya mambo nchini
Afghanistan zimeyawezesha makundi ya waasi na ya kigaidi kudumisha
harakati zao nchini humo kwa kuyapa uhuru wa kuzalisha fedha kupitia
magendo ya dawa za kulevya. Makundi hayo ya kigaidi ambayo daima
yanahudumia malengo ya siasa za kikoloni za Marekani na washirika wake,
hivi karibuni yaliingia vitani na katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe
ya kudhibiti maeneo yenye hali bora zaidi kwa ajili ya kuzalisha dawa
za kulevya na mihadarati. Mtaalamu wa siasa wa Russia, Anatoly Maradasov
anasema: "Sababu ya hitilafu na mapigano ya kundi la Taliban na
Daesh huko Afghanistan ni kutaka kudhibiti mikoa inayozalisha kwa wingi
dawa za kulevya na kunyang'anyana tonge hilo nono."
Alaa
kulli hal, kutumbukizwa wanawake katika magendo na usafirishaji wa dawa
za kulevya nchini Afghanistan ni matokeo ya karibu miongo miwili ya
kuwepo kwa majeshi ya Marekani na Uingereza nchini humo. Nchi hizo mbili
na washirika wao wanavunja nguzo za usalama na amani ya Afghanistan na
nchi jirani kupitia njia ya kusaidia ustawishaji wa dawa za kulevya
nchini humo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: