KUFICHULIWA UUNGAJI MKONO MPYA WA UTAWALA WA KIZAYUNI KWA MAKUNDI YA KIGAIDI NCHINI SYRIA

Kufichuliwa uungaji mkono mpya wa utawala wa Kizayuni kwa makundi ya kigaidi nchini Syria
Katika taarifa yake gazeti la utawala haramu wa Israel la Haaretz limekiri kwamba Tel Aviv inajishughulisha zaidi na kuwapatia silaha magaidi nchini Syria.
Kabla ya hapo pia Wizara ya Afya ya utawala huo wa Kizayuni katika taarifa yake ilitangaza kwamba, zaidi ya magaidi 1400 waliojeruhiwa na jeshi la Syria, wamepatiwa matibabu katika hospitali tofauti za Israel. Katika uwanja huo Elizabeth Surcouf, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Marekani anayejishughulisha na matukio ya Syria anasema: "Zaidi ya makundi saba ya kigaidi yanapata misaada ya silaha, zana za kijeshi na fedha kutoka Israel kupitia eneo la Golan la nchini Syria. Aidha kabla ya hapo gazeti la The Wall Street Journal liliripoti kwamba Israel inafanya haraka kuwapatia silaha na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi ya Syria. Kwa mujibu wa gazeti hilo la Marekani, mwaka 2016 Israel ilianzisha kikosi maalumu cha kuyapatia misaada tofauti makundi ya kigaidi kama vile silaha, zana za kijeshi na fedha kwa ajili ya kuwalipa mishahara magaidi hao.” Mwisho wa kunukuu." 
Netanyahu akimtembelea hospitalini mmoja wa magaidi aliyejeruhiwa na jeshi la Syria
Ukweli ni kwamba utawala wa Kizayuni umekuwa ukishirikiana bega kwa bega na makundi ya ukufurishaji nchini Syria, huku majeruhi wao, wakitibiwa katika hospitali za Israel ndani ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Mashambulizi ya mara kwa mara ya anga na makombora ya utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya maeneo ya serikali ya Syria, mbali na kwamba yanabainisha wazi uchokozi wa utawala huo katili, yanaweza pia kutafsiriwa kuwa ni msaada wa kwa magaidi hao wa Kiwahabi. Kwa hakika hivi sasa Syria inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa ndani unaotokana na njama chafu za madola ya Magharibi na washirika wao katika eneo pamoja na utawala wa Kizayuni.
Raia wa Syria wakiandamana kuiunga mkono serikali yao pamoja na Iran
Kupitia njama hizo, Israel na madola hayo ya Magharibi yanayompinga Rais Bashar al-Assad, yanatumia vibaya baadhi ya malalamiko ya Wasyria kuyaunga mkono kilojestiki makundi ya kigaidi na yanayofanya ghasia, kwa lengo la kuvuruga usalama na amani ya nchi hiyo ya Kiarabu. Hata hivyo kipigo ambacho magaidi hao wamekipata kutoka kwa jeshi shupavu la serikali ya Damascus, kimekuwa na taathira kubwa katika kudhoofisha uungaji mkono huo wa madola ya Magharibi, baadhi ya tawala za Kiarabu na utawala wa Kizayuni. Katika mazingira hayo, Israel inakusudia sambamba na kufanya mashambulizi dhidi ya jeshi la Syria, iimarishe harakati za makundi ya kigaidi hususan katika maeneo ya kistratijia ndani ya taifa hilo la Kiarabu.
Mabaki ya ndege ya kisasa ya Israel aina ya F16 iliyotunguliwa na jeshi la Syria
Ni kwa ajili hiyo ndio suala la kuongezeka mashambulizi ya utawala wa Kizayuni nchini Syria sambamba na kuongeza kiwango cha misaada ya Marekani na baadhi ya watawala wa Kiarabu kwa makundi hayo ya kigaidi, kukawa na maana ya kupewa pumzi bandia na za mwisho vibaraka wao hao wa kigaidi. Matukio ya Syria yanaonyesha kwamba, nchi hiyo kwa sasa inakabiliwa na harakati chafu na za shari, yaani utawala haramu wa Kizayuni na makundi ya kigaidi kupitia uungaji mkono wa madola ya Magharibi. Ni katika hali hiyo, ndipo wakati sehemu ya ardhi ya Syria yaani eneo la Golan bado liko chini ya udhibiti wa utawala wa Kizayuni, nchi hiyo ya Kiarabu inaendelea kulengwa na hujuma pana za makundi ya kigaidi kwa lengo la kuvuruga usalama na amani ya taifa hilo. Suala hilo linabainisha njama pana zinazofanywa dhidi ya nchi hiyo ambayo ina nafasi muhimu ya kistratiji na moja ya mihimili mikuu ya muqawama katika eneo la Mashariki ya Kati.
Magaidi wa kundi la Daesh ambao wanalelewa na Israel
Katika uwanja huo, madola ya Magharibi sambamba na kuzishughulisha nchi za eneo na wimbi la ugaidi, yameongeza pia njama katika eneo hili ili kwa njia hiyo yaweze kutumia misaada yao kwa Israel, kufikia malengo yao ya kuibua fitina katika eneo hili muhimu. Ni kwa kuzingatia kuwa njama hizo zimeratibiwa tangu mapema, ndio maana tukawa tunashuhudia kiwango kikubwa cha ushirikiano wa makundi ya kigaidi na utawala haramu wa Israel sambamba na kuongezeka jinai zao nchini Syria.

0 comments: