TRUMP, ADUI WA HAKI ZA BINADAMU DUNIANI

Trump, adui wa haki za binadamu duniani
Katika kukaribia mwaka wa pili wa Rais Donald Trump kuwa ofisini, mashirika ya haki za binadamu yamekosoa vikali utendaji wa serikali ya Marekani na hasa Trump mwenyewe kwa kuvunja haki za binadamu.
Akizungumzia suala hilo hivi karibuni, Kenneth Roth, mkurugeni mwandamizi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lililo na makao makuu yake mjini New York Marekani, ameutaja utendaji wa Trump kuhusiana na suala zima la haki za binadamu kuwa janga kubwa na kusema rais huyo ni dikteta anayeunga mkono tawala zisizo za kidemokrasia kama Saudi Arabia. Wakati huohuo maripota wasio na mipaka wametoa taarifa wakiashiria matamshi ya hujuma na dharau ya Trump dhidi ya vyombo vya habari na kusema kuwa tabia yake hiyo ni tishio kubwa kwa demokrasia ya Marekani. Zeid bin Ra'ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Biandamu wa Umoja wa Mataifa pia amesema kuwa Donald Trump anatishia uhuru wa vyombo vya habari nchini humo.
Kenneth Roth, Mkurugezi Mwandamizi wa Human Rights Watch
Hata hivyo ni wazi kuwa suala la ukiukaji wa haki za binadamu halihusiani tu na Rais Trump bali kwa miongo kadhaa sasa marais wa Marekani wamekuwa wakikiuka wazi haki za binadamu ndani na nje ya mipaka ya nchi hiyo. Kwa mfano katika utawala wa George W. Bush, ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ulifanyika ndani na nje ya nchi hiyo kukiwepo kuanzishwa jela za mateso na za kuogofya za Guantanamo nchini Cuba na Abu Ghurain huko Iraq na vilevile kuteswa wafungwa kwa kuzamishwa majini. Katika kipindi cha Barack Obama pia, ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ulifanywa na askari jeshi wa nchi hiyo katika pembe tofauti za dunia na hasa nchini Afghanistan ambapo ndege za kijeshi zisizo na rubani za Marekani zilitumika kuua maelfu ya raia wasio na hatia. Hii ni katika hali ambayo uungaji mkono wa Marekani kwa nchi na tawala nyingine zinazokiuka wazi haki za binadamu kama Saudi Arabia, Bahrain na utawala haramu wa Israel umekuwa ukiendelea kwa miaka hii yote.
Sehemu ya maafa na uharibifu unaofanywa na Saudia nchini Yemen
Pamoja na hayo lakini vitendo na matamshi ya Trump dhidi haki za binadamu na uhuru wa vyombo vya habari yameufikisha ukiukaji huo wa haki za binadamu katika hatua nyingine hatari. Trump anachukuliwa kuwa ni mtu aliye na chuki kali dhidi ya wahajiri, wageni na Waislamu na asiyesita kutumia matusi dhidi ya binadamu wenzake. Ni hivi majuzi tu ambapo Trump aliwataja Wamexico kuwa watenda jinai, Waislamu kuwa magaidi na Waafrika kuwa shimo la choo. Ushindi wake chini Marekani hivi sasa umeyapa nguvu mpya makundi yenye misimamo ya kupindukia mipaka, ya kibaguzi na yenye chuki kali na yanayotumia mabavu dhidi ya wenzao ndani na nje ya mipaka ya Marekani, makundi ambayo huwa hayasiti hata kidogo kutenda jinai na kukiuka haki za binadamu pamoja na uhuru wa watu binafsi na wa kiraia.
Kuhusu siasa za nje pia, hatua ya Trump ya kuichagua Saudia kuwa nchi ya kwanza aliyoitembelea akiwa Rais wa Marekani, nchi ambayo iko mstari wa mbele wa kukiuka haki za binadamu na inayohusika moja kwa moja katika mauaji ya Waislamu katika vita vyake vya kivamizi huko Yemen, inaonyesha ni kwa kiwango gani Marekani haijali kuhusu suala la kuheshimiwa haki za binadamu.
Ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Wazayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia
Trump pia ameyakasirisha mno mashirika mashuhuri ya kutetea haki za binadamu kutokana na hatua yake ya kuunga mkono kuendelea kujengwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina pamoja na uamuzi wake wa hivi karibuni wa kutambua rasmi mji mtakatifu wa Quds eti kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Pamoja na hayo, lakini haionekani kuwa malalamiko na ukosoaji huo wote wa mashirika na taasisi za kimataifa utamfanya Donald Trump ambaye ameipa kipaumbele nara ya 'Marekani Kwanza' katika siasa zake kulegeza msimamo na kuheshimu haki za binadamu pamoja na uhuru wa kujieleza wa vyombo vya habari.

0 comments: