SAKATA LA MELI ZINAZOBEBA MIHADARATI ZIKIWA NA BENDERA YA TANZANIA, LAMLAZIMU RAIS MAGURULI KUSITISHA USAJILI WA MELI

Sakata la meli zinazobeba mihadarati zikiwa na bendera ya TZ, lamlazimu Rais Magufuli kusitisha usajili wa meli
Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania ameagiza kusitishwa mara moja usajili wa meli mpya nchini humo kufuatia kukamatwa dawa za kulevya na bidhaa nyingine zilizopigwa marufuku kimataifa ndani ya meli zinazopeperusha bendera ya Tanzania.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar, Balozi Ali Abeid Karume kufuatilia suala hilo mara moja. Kadhalika Magufuli amemuagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga kusimamia utekelezaji wa agizo hilo na kuhakikisha kuwa jina la Tanzania halichafuliwi ndani na nje ya nchi.
Moja ya meli zenye bendera ya Tanzania
“Kafanyeni uchunguzi wa kina kwa meli zote zinazopeperusha bendera ya Tanzania, fanyeni uchunguzi kwa meli zilizokamatwa ambazo ni tano na pia hizi 470 zilizosajiliwa na zinaendelea kufanya kazi zichunguzeni, hatuwezi kuacha jina la nchi yetu lichafuliwe na watu wanaofanya mambo kwa masilahi yao.” Amesema Rais Magufuli. Kadhalika amehimiza kutekelezwa kwa maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais Bi Samia Suluhu Hassan juzi, ambaye alitangaza kuzifutia usajili meli mbili zilizokamatwa hivi karibuni sanjari na kuamuliwa kushushwa bendera ya Tanzania kwenye meli hizo.
Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania
Suluhu alizitaja meli hizo kuwa ni Kaluba iliyokamatwa maeneo ya Jamhuri ya Dominican Desemba 27 mwaka jana ikiwa na wastani wa tani 1.6 ya dawa za kulevya pamoja na Andromeda ambayo nayo iliyokamatwa ikisafirisha silaha kinyume cha sheria za kimataifa. Matukio ya kukamatwa meli zenye mihadarati na zinazopeperusha bendera ya Tanzania, yamekuwa yakiripotiwa nchi tofauti za dunia.

0 comments: