RAIS WA UGANDA ATAFAKARI KUREJESHA HUKUMU YA KIFO

Rais wa Uganda atafakari kurejesha hukumu ya kifo
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema anatafakari kurejesha hukumu ya kifo nchini humo ili kukabiliana na wimbi kubwa la uhalifu nchini.
Katika ujumbe aliotuma katika akaunti yake ya Twitter, Rais Museveni amesema amekuwa akisita kutia saini kila hukumu ya kifo anayoletewa tokea mwaka 1999. Hukumu ya kifo ambayo ndio adhabu kali zaidi Uganda kwa wanaohusika na uhalifu kama vile mauaji, uhaini na kunajisi haijawahi kutekelezwa tangu mwaka 1999. Idara ya Magereza Uganda inasema hivi sasa kuna wafungwa 278 ambao wamehukumiwa kifo lakini Rais Museveni hajatia saini amri ya utekelezwaji wa hukumu hizo.
Rais Museveni amesema watu wanatumia vibaya moyo wake wa huruma na sasa wengine wanadhani wanaweza kutenda uhalifu bila kuadhibiwa. Amesema anatafakari kuhusu kubadili msimamo wake huo wa kutotia siani adhabu ya kifo.
Kitanzi
Katika nchi jirani ya Kenya pia, hukumu ya kifo iko katika sheria lakini marais wa nchi hiyo hawajatia saini amri ya utekelezwaji hukumu hiyo kwa miaka 30 sasa. Oktoba mwaka 2016 Rais Uhuru Kenyatta alitia saini amri ya kubatilisha hukumu ya kifo ya wanaume 2,655 na wanawake 92 na kuifanya iwe hukumu ya maisha jela. Wakosoaji wanasema kutotekelezwa hukumu ya kifo kumepelekea kuongezeka kesi za uhalifu katika nchi hizo.

0 comments: