NGUVU YA WANANCHI WA YEMEN, MSINGI WA KUKABILIANA NA NGUVU KUTOKA NJE

Nguvu ya wananchi wa Yemen, msingi wa kukabiliana na nguvu kutoka nje
Msemaji wa jeshi la Yemen lenye mfungamano na Harakati ya Ansarullah ametangaza kuwa, maeneo yote ya mji mkuu Sana'a yanadhibitiwa na jeshi na kwamba, hali ya usalama ni ya amani na utulivu kabisa.
Fitina au mapinduzi? Hapana shaka kuwa, haya ni maneno na istilahi kwa ajili ya kutoa wasifu wa kile ambacho kilifanywa na rais wa zamani wa Yemen Ali Abdallah Swaleh kabla ya kuuawa siku ya Jumatatu. Kimsingi sio muhimu kwamba, hatua hiyo inapewa jina gani, bali la muhimu ni kuwa, mzozo na fitina hiyo ilimalizika kwa muda mfupi au ilipoteza taathira yake. 
Ali Abdallah Swaleh ndiye aliyekuwa mshindwa mkuu wa fitina hiyo iliyokuwa imeanza Jumamosi iliyopita. Licha ya kuwa kuna sababu nyingi zinazoweza kutajwa za kushindwa fitina ya Ali Abdallah Swaleh dhidi ya Ansarullah, lakini moja ya sabahu za kushindwa huko ni hatua ya Ansarullah ya kutegemea nguvu ya wananchi ambayo ndio msingi na nguzo.
Ali Karimi, mhadhiri wa Chuo Kikuu anaamini kwamba nguvu ya wananchi ni nguzo katika Mashariki ya Kati ambayo inatokana na matukio ya ndani na ya nje katika eneo hili ambayo huupa changamoto utawala ambao misingi yake inategemea nguvu kutoka nje. Kimsingi nguvu ya wananchi ni msingi ambao unasimama na kuwa imara kwa kutegemea uungaji mkono wa wananchi.
Rais wa zamani wa Yemen aliyeuawa hivi karibuni
Saad Zari'i mtaalamu wa masuala ya kisiasa anaamini kwamba: Usalama wa wananchi sio msingi wa usalama ambao ni kitu cha pembeni ambacho tawi lake liko katika nchi fulani na mizizi yake katika nchi nyingine, bali jambo hilo linatoka katika muundo na moyo wa nchi husika na kwa kuwa hali iko namna hiyo, basi inawezekana kusimama  na kukabiliana na vitisho.
Ni jambo lisilo na shakka kuwa, msingi na nguzo kuu ya nguvu ni wananchi na vikosi vya wananchi. Kabla ya matukio ya mwaka 2011 katika ulimwengu wa Kiarabu ni Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ya Lebanon tu ndiyo iliyokuwa ikihesabiwa kuwa nguvu yenye misingi ya wananchi.
Baada ya mwaka 2011 nchini Syria, Iraq na Yemen nako kulisisitizwa suala la kurejea katika nguvu yenye msingi na chimbuko la wananchi. Kuundwa vikosi vya kujitolea vya wananchi huko Syria na Hashd al-Sha'bi huko Iraq sambamba na kuimarishwa Harakati ya Wananchi ya Ansarullah ya Yemen ni miongoni mwa mambo yanayohesabiwa kuwa dhihirisho la nguvu yenye misingi na chimbuko la wananchi. 
Hata kama katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kwa namna fulani kumekuweko na ushirikiano wa kiufundi baina ya Ansarullah na vikosi vinavyofungamana na Chama cha Kongresi ya Wananch kwa uongozi wa mwendazake Ali Abdallah Swaleh kwa ajili ya kukabiliana na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia pamoja na vikosi vinavyofungamana na Rais Abdu Rabbuh Mansour Hadi, rais aliyejiuzulu na kuikimbia nchi, lakini kutokana na Ansraullah kupata baraka za wananchi kutokana na kuwa kwake harakati ya wananchi, haiwezekani kulilinganisha kundi hilo na makundi mengine ya Yemen.
Abdul Malik al-Houthi, Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen
Ni kwa msingi huo ndio maana njama na ukwamishaji mambo mbalimbali uliofanywa na Ali Abdallah Swaleh katika kipindi cha miaka mitatu cha kuwa pamoja na Ansarullah hasa katika nusu ya pili ya mwaka huu, haujawa na natija yoyote ya maana kutokana na Ansarullah kupata uungaji mkono wa wananchi. Kufeli njama za Ali Abdallah Swaleh siku mbili kabla ya kufikia ukingoni maisha yake siku ya Jumatatu ni mfano wa wazi wa jambo hilo.
Tunaweza kusema kuwa, kuibuka tukio jipya la "Nguvu Yenye Chimbuko la Wananchi" hasa katika eneo la Mashariki ya Kati katika miaka ijayo kunaweza kuunda nguvu tofauti ambapo sifa muhimu ya nguvu hiyo ni kupunguza nafasi na mchango wa nguvu kutoka nje kwa ajili ya kudhamini usalama.

0 comments: