KUULIWA WAISLAMU MSIKITINI KATIKA SAMBULIO LA BOMU LA KUJITOA MHANGA NCHINI NIGERIA

Kuuliwa Waislamu msikitini katika shambulio la bomu la kujitoa mhanga nchini Nigeria
Watu wasiopungua 50 wameaga dunia katika mlipuko wa bomu uliotokea msikitini kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Othman Abubakar Msemaji wa polisi ya Nigeria ametangaza kuwa shambulio hilo la kujitolea mhanga dhidi ya msikiti katika mji wa Mubi jimboni Adamawa lilifanywa wakati waumini walipokuwa katika Sala ya Alfajiri. Kundi la kigaidi la Boko Haram limetangaza kuhusika na shambulio hilo. 
Hii ni mara ya kwanza kutokea tukio kama hilo la kigaidi tangu kukombolewa mji wa Mubi kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la Boko Haram mwaka 2014. Hujuma na mashambulizi ya kigaidi ya Boko Haram hadi sasa yamesababisha kuuliwa watu zaidi ya elfu 20 huko Nigeria. Kundi hilo linaendeleza hujuma zake hizo za kigaidi  khususan dhidi ya Waislamu wa Nigeria; huku kwa muda sasa jeshi la nchi hiyo likidai kuwa linafanya juhudi za kuliangamiza. 
Udhaifu wa jeshi la Nigeria na kushindwa kwake kukabiliana na makundi ya kigaidi kumeyaandalia fursa makundi hayo ya kuendeleza harakati zao likiwemo kundi la Boko Haram. Kuna ishara zinazoonyesha kuwa baadhi ya nchi za Magharibi na utawala wa Kizayuni zinaliunga mkono nyuma ya pazia kundi la kigaidi la Boko Haram nchini Nigeria ili kuendelea kudhamini maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi kwa kulipatia kundi hilo misaada ya silaha na zana za kijeshi kisirisiri ili kuliimarisha. 
Wanamgambo wa kundi la Boko Haram  
Jeshi la Nigeria huko nyuma liliwahi kunasa silaha elfu 10 yakiwemo makombora aina ya M-302 yaliyoundwa Israel ambayo yana uwezo wa kulenga umbali wa kilomita 200. Silaha hizo zilinaswa katika kambi ya Boko Haram katika msitu wa Sambisa kaskazini mashariki mwa nchi. Uchunguzi uliofanywa na maafisa usalama kuhusiana na suala hilo unaonyesha kuwa silaha hizo zilitumwa moja kwa moja kwa Boko Haram kutoka Israel. Aidha mkono wa Israel unashuhudiwa katika mashinikizo yanayozidi kuwaandama Waislamu wa nchi hiyo. Viongozi wa utawala ghasibu wa Kizayuni ambao wamegonga mwamba katika siasa zao katika eneo hili la Mashariki ya Kati; hivi sasa wanatafuta eneo jingine barani Afrika la kuwa na ushawishi ambapo Nigeria inaonekana kuwa chaguo lao  zuri kutokana  kuwa na makabila mengi na nafasi nzuri ya kiuchumi na kisiasa. 
Sheikh Adam Soho, mwanachama mwandamizi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anasema kuwa: Serikali ya Nigeria iko chini ya ushawishi wa serikali za Saudi Arabia, Marekani na utawala wa Kizayuni na pande zote hizo zinaendesha njama dhidi ya Waislamu khususan wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria. 
Waislamu wa madhehebu wa Shia wa nchini Nigeria 
Katika upande wa kiuchumi, Nigeria ni nchi yenye umuhimu; ni nchi ambayo ina jamii ya kizazi cha vijana na utajiri mkubwa wa mafuta, ambayo siku zote imekuwa ikikodolewa jicho la tamaa na madola ya kikoloni. Kwa msingi huo kuwepo mivutano ya kisiasa na kiusalama kunayaandalia fursa madola hayo ya  kutimiza malengo yao nchini humo. Aidha nchi nyingi za Magharibi zimekuwa zikizungumzia suala la kuisaidia Nigeria katika vita dhidi ya Boko Haram, na si tu kuwa  kivitendo nchi hizo hazijatoa msaada wowote kwa Nigeria, bali zimekuwa zikishadidisha tu hujuma za kundi hilo.

0 comments: