KUJIUZULU MUGABE NA MUSTAKABALI WA KISIASA WA ZIMBABWE

Kujiuzulu Mugabe na mustakabali wa kisiasa wa Zimbabwe
Hatimaye baada ya takribani wiki moja ya changamoto, mivutano na uingiliaji wa jeshi hatimaye Rais Robert Gabriel Mugabe wa Zimbabwe ameng'atuka madarakani. Mugabe amechukua hatua hiyo baada ya Bunge kuanzisha mchakato wa kumsaili kwa lengo la kumuuzulu.
Kujiuzulu Mugabe kumehitimisha karibu miongo minne ya utawala wake nchini Zimbabwe. Pamoja na hayo japokuwa kujiuzulu kwake kumewafurahisha Wazimbabwe wengi wakiwemo wanachama na wafuasi wa chama chake tawala cha ZANU-PF lakini wako pia waliohuzunishwa. Ni kama alivyosema Terence Mukupe, mbunge na mwanachama wa Zanu-pf ya kwamba: "wabunge wa chama tawala hawakutaka mwisho wa rais wao uwe kama hivi. Sisi tunampenda rais, lakini wakati ulikuwa umeshafika wa yeye kujistaafisha mwenyewe. Waliomzunguka walikuwa wakimshauri vibaya sana. Tunasikitika sana amefikia ukingoni namna hivi".
Mugabe akihutubia siku ya uhuru wa Zimbabwe mwaka 1980
Robert Mugabe aliingia madarakani nchini Zimbabwe mwaka 1980 akiwa anajulikana kama shakhsia mashuhuri zaidi wa mapambano dhidi ya ukoloni na harakati za kupigania uhuru wa nchi yake. Mugabe alikuwa pia mmoja wa shakhsia wakubwa wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na mfumo wa Apathaidi katika nchi jirani na Zimbabwe ya Afrika Kusini.
Robert Mugabe aliongoza mapambano dhidi ya wakoloni hadi nchi yake ikapata uhuru; na akiwa kiongozi wa mapambano ya ukombozi wa Zimbabwe, akawa waziri mkuu wa kwanza wa taifa hilo changa wakati huo. Mara baada ya kushika madaraka, kwa kutumia kaulimbiu ya umoja alianzisha sera ya kuleta maridhiano nchini. Waziri Mkuu huyo wa Zimbabwe aliamua kukabidhi nyadhifa na vyeo muhimu kwa raia wazungu. Kutokana na hatua yake hiyo, katika kipindi cha karibu muongo mmoja Zimbabwe ilipata mafanikio mazuri kiuchumi, ikapiga hatua kuelekea kwenye ustawi kwa kujenga mashule, vituo vya afya na tiba pamoja na kuwajengea nyumba raia wazalendo weusi ambao ndio wanaounda idadi kubwa ya watu wa nchi hiyo. 
Majenerali wa jeshi walioongoza kampeni ya kumwondoa Mugabe madarakani
Pamoja na hayo, kuwakandamiza wapinzani na kutekeleza sera za chama kimoja zilikuwa miongoni mwa siasa za Mugabe zilizokosolewa sana na wapinzani. Katika hali kama hiyo, umri mkubwa alionao, uingiliaji wa mke wake Grace na kampeni zake za kutaka kutwaa madaraka, hali mbaya ya uchumi  na vilevile kufichuliwa ufisadi uliofanywa na baadhi ya jamaa wa Mugabe na wanachama wa chama chake cha Zanu-pf yote hayo yalishadidisha upinzani dhidi ya kiongozi huyo.
Hivi ndivyo wabunge na maseneta walivyoipokea habari ya kujiuzulu Mugabe
Hivi sasa baada ya Mugabe kuondoka madarakani, hali ya kisiasa nchini Zimbabwe imebadilika. Kwa mujibu wa habari mbalimbali Emmerson Mnangagwa, makamu wa rais ambaye alitimuliwa na Mugabe na ambaye sasa amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Zanu-pf, ndiye atakayeshika hatamu za urais wa nchi. Wachambuzi wengi wanaamini kuwa Mnangagwa ataendeleza siasa za Mugabe, tab'an kwa kutegemea nguvu za jeshi. Pamoja na hayo watu wengi wana wasiwasi wa kutokea hali ya kukomoana na ulipizaji visasi wa ndani ya chama na kuvurugika hali ya kisiasa ya Zimbabwe. Kiasi kwamba kwa kuchelea hali hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa Wazimbabwe wote "kudumisha utulivu na uvumilivu".
Wananchi wakipachua picha ya Mugabe baada ya kujua kwamba si rais tena wa Zimbabwe
Kurejesha uthabiti wa kisiasa, kujiepusha na sera za kutawala kijeshi na kidikteta, kustawisha maelewano na nchi za eneo na nje ya eneo, kuboresha hali ya uchumi na kuitishwa uchaguzi mkuu katika mwaka ujao wa 2018 katika mazingira tulivu na kwa kuheshimu sheria ni miongoni mwa matarajio muhimu zaidi waliyonayo wananchi; matarajio ambayo kama hayatotimizwa si hasha yakawafanya Wazimbabwe wengi watamani kurejea tena kwenye enzi za Mugabe.../

0 comments: