ODINGA; KESHO JUMATATU MSIENDE KAZINI, JUMANNE NITATOA TANGAZO MUHIMU

Kinara wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amewataka wafuasi wake wasiende kazini kesho Jumatatu na wajiandae kupokea kile alichokitaja kuwa maelekezo na tangazo zito litakalotikisa taifa siku ya Jumanne.
Akihutubia maelfu ya wafuasi wake katika mtaa wa mabanda wa Kibera jijini Nairobi, Odinga ambaye aligombea kiti cha rais na kuibuka wa pili kwa mujibu wa matokeo rasmi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, amevituhumu vyombo vya usalama kuwa vinatumia nguvu kupita kiasi katika kuzima maandamano ya wapinzani.
Kinara huyo wa muungano wa upinzani wa NASA amesema: "Tulitabiri kuwa wataiba kura na kuchakachua matokeo, na hayo yamefanyika, hatujakata tamaa, msubiri tangazo juu ya hatua tutakayochukua siku ya Jumanne."
Hapo jana mrengo huo wa upinzani ulidai kwamba, jeshi la polisi nchini humo limeua watu mia moja tangu yalipoanza maandamano ya kulalamikia ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Jumanne iliyopita, madai ambayo yamekanushwa vikali na serikali kupitia Kaimu Waziri wa Usalama wa Taifa, Fred Matiang'i.
Odinga (kushoto) na Rais Kenyatta
Kwa mujibu wa Kamisheni ya Taifa ya Kutetea Haki za Binadamu, watu 24 wameuawa kwa kufyatuliwa risasi hadi sasa, katika maandamano na ghasia za kupinga ushindi wa Rais Kenyatta.
Matokeo rasmi ya IEBC yanaonyesha kuwa, Uhuru Kenyatta aliyegombea kwa tiketi ya chama cha Jubilee alipata ushindi baada ya kujizolea kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27 ya kura zote, huku mshindani wake mkuu Raila Odinga  aliyegombea kwa tiketi ya ODM akipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74 ya kura zote.
Hata hivyo viongozi wa NASA wanadai kuwa, Odinga alipata kura zaidi ya milioni nane huku Rais Kenyatta aliyewania kiti hicho kwa muhula wa pili akipata kura milioni saba na laki saba. 

0 comments: