SHINDANO LA "MAVUNDE NA UTAMADUNI WETU" LATIA FORA DODOMA


NA K-VIS BLOG, DODOMA
SHINDANO la ngoma za utamaduni liitwalo ‘Mavunde na utamaduni wetu’ limefanyika leo mjini Dodoma likiwa na lengo la kuenzi, kulinda na kuhifadhi utamaduni wa watu wa Dodoma.

Shindano hilo limeandaliwa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini Anthony Mavunde(pichani juu katikati), na lilihusisha vikundi vya ngoma za asili ya Dodoma 7.

Vikundi hivyo ni Simba dume, changamoto, Noti mtemi, Neema Yerusalem, Chipukizi, Finga Vikonje na Imani Makulu.

Akizungumza katika shindano hilo, Mbunge wa Dodoma Mjini  Anthony Mavunde ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, amesema uwepo wa shindano hilo ni utekelezaji wa ahadi yake ambayo aliitoa wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu 2015 na kumpongeza  Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa kuhamishia shughuli za serikali Dodoma, kupiga vita Rushwa na Ubadhirifu na Kulinda Maliasili za Taifa kwa manufaa ya watanzania wote.

“Tamaduni zetu zilikuwa zimeanza kusahaulika watu hawakuona tena umuhimu wa ngoma za jadi na hii ni kutokana na utandawazi na kuwa watu wa mjini sana tumesahau tumetoka wapi,”amesema Mavunde

Amebainisha katika kampeni hizo aliahidi kwa nafasi yake atajitahidi kuviunganisha vya kutoka maeneo mbalimbali ili kuenzi na kulinda utamaduni wa Dodoma.

“Hatua yetu ya kwanza ni kukusanya vikundi na kuvipambanisha lakini baadaye tutakuwa na makubwa ya kimkoa kila mwaka na hii nawashawishi na wenzangu pia, ili mkoa wetu uendelee kutunza na kuhifadhi utamaduni wetu,”amesema

Mavunde amesema shindano hilo linalenga kuwakumbusha vijana kuwa mababu zao waliishi kwa namna gani.

Kwa upande wake, Chifu wa Dodoma mjini Lazaro Chihoma amempongeza mavunde kwa kuandaa tamasha hilo na kudai kuwa wamepita viongozi wengi lakini hawakuona umuhimu wa kuenzi utamaduni wao.

Vikundi vilivyoibuka kidedea ni pamoja na kikundi cha Imani Makulu ambacho kimepata kombe na fedha Sh.300,000, mshini wa pili ni Kikundi cha Chipukizi kimepata Sh.250,000 na ngao na mshindi wa tatu Figa Vikonje kimepata Sh.150,000 huku vingine vikipatiwa Sh.80,000 kila kimoja.



Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Anthony Mavunde, ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma mjini (CCM), akizungumza katika Shindano la Mavunde na Utamaduni wetu lililofanyika mjini Dodoma.


Chifu wa Dodoma mjini Lazaro Chihoma akizungumza katika Shindano la Mavunde na Utamaduni wetu, mjini Dodoma


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Anthony Mavunde akiwa na viongozi mbalimbali katika Shindano la Mavunde na Utamaduni wetu.


Umati wa wakazi wa Dodoma waliohudhuria shindano la Mavunde na Utamaduni wetu.


Umati wa wakazi wa Dodoma waliohudhuria shindano la Mavunde na Utamaduni wetu.


Moja ya vikundi vya ngoma za kiasili vilivyoshiriki katika Shindano la Mavunde na Utamaduni wetu.


Moja ya vikundi vya ngoma za kiasili vilivyoshiriki katika Shindano la Mavunde na Utamaduni wetu.

0 comments: