RAIS DK. MAGUFULI: MKAPA NA KIKWETE WALINITENGENEZEA MAISHA YA KISIASA

NA MWANDISHI WETU
Rais John Magufuli ameukumbuka mchango wa marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na kuwashukuru huku akieleza kuwa wao ndiyo waliotengeneza maisha yake ya kisiasa hadi kuwa kiongozi.

Magufuli ameyasema hayo leo Jumatatu, Julai 10 wilayani Chato wakati wa uzinduzi wa nyumba 50 zilizojengwa na Taasisi ya Mkapa Foundation.


“Nakumbuka siku hiyo tulikuja hapa Chato na wewe (Mkapa) Msafara ulisimamishwa na ukawaambia wananchi wa Chato nichagulieni huyu, nakumbuka ulikuwa umevaa viatu vyekundu,” amesema na kuongeza:

“Kwa bahati nzuri, wananchi wa Chato wakanichagua, baadaye ukanichagua kuwa naibu waziri. Wewe ulinitangaza, sikustahili chochote, maneno yako yalikuwa na nguvu kwa Watanzania.”
Amesema anamkushukuru pia Rais Mstaafu Jakaya Kkwete na kusema: “Baada ya kipindi cha Mkapa, Kikwete alipokuja, lakini kwanza wewe ukanipitisha kugombea ubunge tena kwa mara nyingine, nikachaguliwa bila kupingwa katika jimbo hili.” Amesema
Amesema hata katika kipindi cha awamu ya nne, Rais Kikwete alimteua katika wizara mbalimbali.
“Kwangu mimi nyinyi mlitengeneza maisha yangu katika uongozi. Pia nawashukuru sana viongozi wa awamu ya kwanza, Nyerere na Mwinyi ambao walitengeneza mazingira mazuri ndani ya Chama cha Mapinduzi,” amesema na kuongeza:
“Kwangu mimi sina cha kuwalipa jukumu langu ni kuwatetea na ninawaahidi Watanzania kuwa nitafanya kazi kwa nguvu zangu zote, namuomba Mungu asinifanye nikawa na kiburi namuomba asinifanye nikasahau nilipotoka.”

0 comments: