MAY ATAKA KUUNDA SERIKALI NA DEMOCRATIC UNIONIST

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema atabakia madarakani na kuunda serikali,  baada ya uchaguzi mkuu hapo jana ambapo chama chake cha Conservative kilipoteza wingi wake bungeni.

London Theresa May (picture-alliance/empics/J. Brady)
Waziri Mkuu May alielezea uamuzi wake wa kuunda serikali licha ya chama cha Conservative kutokuwa na wingi bungeni, katika taarifa yake kwa waandishi habari nje ya makao yake makuu ya Nambari 10 mtaa wa Downing mjini London, na baada ya kuonana na Malkia Elizabeth kwenye kasri la Buckingham na kumuomba ampe nafasi ya kuunda serikali mpya.
May ameahidi kushirikiana na wale aliowaita marafiki na washirika na hasa katika Chama cha  Democratic Unionist (DUP), ambacho ndicho kikubwa kabisa katika Ireland ya Kaskazini na kinaweza kumpa May uungaji mkono wa kutosha kuweza kutawala.
"Vyama vyetu hivi viwili vimekuwa na uhusiano imara kwa miaka mingi na nina matumaini kuwa tutaweza kufanya kazi pamoja kwa maslahi ya Uingereza," alisema May. 
DUP kinachotetea jimbo hilo libakie kuwa sehemu ya Uingereza na chenye msimamo wa kihafidhina panapohusika masuala ya kijamii, kimeongeza idadi yake ya viti kufikia 10. Chama cha Conservative kimepata viti 318 , Labour 261, Scotish Nationalist (SNP) 35 na Liberal Democrats viti 12.
May ajipanga upya kwa Brexit
London Labour Führer Jeremy Corbyn (Getty Images/C. Furlong)
Kiongozi wa chama cha Labour, Jeremy Corbyn, ambaye chama chake kimeongeza viti bungeni licha ya kushindwa kupata wingi wa kutosha kuunda serikali.
Akizungumzia majadiliano ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya, mchakato unaojulikana kama Brexit, yatakayoanza tarehe 19 mwezi huu, Waziri Mkuu huyo aliyeitisha uchaguzi wa mapema kwa lengo la kujipa nguvu za kusimama imara kwenye mazungumzo hayo alisema serikali yake mpya itaiongoza nchi kupitia mazungumzo muhimu kwa kutekeleza "maamuzi ya umma wa Uingereza kwa kuitoa kwenye Umoja wa Ulaya".
"Nitafanya kazi kuiweka nchi yetu katika hali ya usalama kwa kutekeleza malengo niliyoyaweka baada ya  mashambulizi ya Manchester na London," amesisitiza May.
Mapema leo chama cha DUP kilikataa kutamka lolote kuhusiana na ripoti kwamba kimekubali kukiunga mkono chama tawala cha Waziri Mkuu May, ingawa kilikubali kuwa tayari mazungumzo baina yao yameanza.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaashiria huenda serikali ya May isidumu muda mrefu na wanafikiri kuna uwezekano wa kuitishwa uchaguzi mwengine. 
Kivutio kikubwa katika uchaguzi wa safari hii kuwania viti 650 ni kuchaguliwa kwa idadi kubwa ya wanawake kuliko wakati mwengine wowote, ambapo jumla ya wabunge wanawake 207 wamechaguliwa ikilinganishwa na 196 katika uchaguzi wa 2015. 

0 comments: