EID MUBARAK NA HADITHI YA MTUME MUHAMMAD

Image may contain: one or more people, beard and closeup
Ndugu zangu,
Kwa ndugu zangu Waislamu, moja ya hadithi za Mtume Muhammad S.A. W ni pale Mtume Muhammad alipokuwa msikitini na maswahaba wake. Mara akaingia msikitini mtu wa kabila la Mabedui na kuanza kukojoa. Maswahaba wa Mtume wakasimama kwa hamaki kutaka kumwadhibu Bedui yule.
Mtume akawasihi maswahaba wake wasifanye jambo lolote litakalomdhuru Bedui yule. Hapo ikavutwa subira. Bedui yule akakojoa na akamaliza haja yake.
Mtume Muhammad alipomuhoji Bedui yule ikabainika kuwa alikuwa ni mtu wa hovyo na wala hakujua kuwa alimokuwa ni msikitini. Bedui yule akaelimishwa, akaelewa. Akarudi kwenye ustaarabu.
Ndio, mkojo ule ulifutwa kwa maji na amani ikawepo. Wahenga walinena; Subira yavuta heri. Siku zote, kwa mwanadamu hamaki si jambo jema. Kwa kutanguliza subira na kutumia hekima, Mtume Muhammad S. A.W aliivuta heri na kuepusha shari.
Maana, kama Mtume alisingewaasa maswahaba wake kuvuta subira, basi, makubwa matatu yangetokea ndani ya msikiti ule; Mosi, zingezuka vurugu na watu kuumizana na hata kutoana roho. Pili, mkojo wa Bedui yule ungesambaa msikitini kwa vile alishaanza kukojoa na isingekuwa rahisi kwake kukatisha mkojo wake. Tatu, kwa mwanadamu, mkojo una madhara ya kiafya pia.
Ni nini basi adili ya hadithi hii?
Jibu: Kwa mwanadamu, ni muhimu kuwa na subra na kutafakari kabla ya kusema au kutenda jambo, usiwe mtu wa kusema au kutenda kisha ukafikiri ulichokisema kwa kukitenda. Fikiri kwanza faida na hasara wa unachokusudia kusema au kutenda.

Kwa ndugu zangu Waislamu, tunaona kuwa Mtume Muhammad ameweza kuonyesha hilo. Na kwa ndugu zangu Wakristo, kuna mifano mingi pia ya jinsi Yesu Kristo alivyoonyesha subra.
Ndio, Uislamu, kama ilivyo kwa Ukristo, na dini nyingi za humu duniani, msingi wake ni amani , upendo na kuvumiliana kwa wanadamu miongoni mwao.

0 comments: