WAZIRI MUHONGO AKUTANA NA RAIS WA KAMPUNI YA TBEA YA CHINA


NA MWANDISHI MAALUM
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amekutana na Rais wa Kampuni ya TBEA ya China, Zhang Xin kwa ajili ya kujadili masuala ya uwekezaji kwenye Sekta ya Nishati nchini.
Mkutano huo wa Waziri Muhongo na Rais huyo ambaye ameongozana na Ujumbe wake umefanyika Mei 21, 2017 jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Waziri Muhongo aliuelezea ujumbe huo baadhi ya fursa za uwekezaji kwenye Sekta ya Nishati nchini na kuwashauri wachague eneo ambalo wanahitaji kuwekeza ili taratibu zianze mapema.
“Fursa ni nyingi sana, ni nyinyi kuamua wapi mmelenga ili taratibu ziendelee ikizingatiwa kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha tunakuwa na Tanzania ya Viwanda,” alisema Waziri Muhongo.
Aliagiza wataalamu wa Wizara ya Nishati na Madini kukutana na Ujumbe huo hapo kesho ili kujadili kwa undani dhamira yao ya uwekezaji ikiwemo kuchagua eneo ambalo wangependa kuwekeza.

Kwa upande wake Xin alisema kampuni yake inaridhishwa na kasi ya Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais John Pombe Magufuli na hivyo wanatarajia kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani bilioni 10 kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Nishati, Barabara, Uendelezaji wa Miji, na Usafirishaji.
Alisema uchumi wa Tanzania umezidi kuimarika na hivyo kuzidi kuvutia wawekezaji kwenye maeneo mbalimbali hususan ikizingatiwa kuwa Tanzania ni Taifa lenye amani  linalokuwa kwa kasi kubwa.
Ujumbe huo upo nchini Tanzania na unatarajia kukutana na Wizara mbalimbali ili kubaini fursa zaidi za uwekezaji nchini.





0 comments: