Ripoti iliyotolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika,
AfDB, kuhusu mustakabali wa ukuaji uchumi wa Afrika inaonesha kwamba
Waafrika wengi wanaona kuna ustawi katika hali za maisha yao.
Wakati idadi kubwa ya wakaazi wa bara la Afrika karibu watu bilioni
1.2 wanaishi katika umasikini, mataifa mengi kati ya 54 ya bara hilo
yamepata mafanikio makubwa katika nyanja za afya, elimu na hali ya
maisha.
"Angalau theluthi tatu ya nchi za afrika zimepata
mafanikio ya kati ya viwango vya juu vya maendeleo ya binadamu", imesema
ripoti hiyo ya AfDB, ikimaanisha mkusanyiko wa kipimo cha hali ya
taifa.
Afrika Kaskazini ina kiwango cha juu, ikikaribiana na
viwango vya kimataifa, ambapo Misri na Tunisia zinatajwa kuwa zina mfumo
wa bima ya afya unaowafikia watu kwa asilimia 75 kati ya 100.
Pia
kumeshuhudiwa mafanikio kadhaa katika mataifa mengine tangu kuanza kwa
karne ya 21. Rwanda imetajwa kuwa nchi iliyopiga hatua zaidi katika
mataifa yaliyo kusini mwa Jangwa la Sahara, ikifuatiwa na Ghana na
Liberia, katika mapambano dhidi ya umaskini tangu mwaka 2005. Mojawapo
ya jitihada kubwa za Rwanda, ilikuwa ni mfumo wa huduma ya bima ya afya
ya kijamii ambapo hadi mwaka 2010, ilikuwa imewafikia watu tisa kati ya
10.
Rais wa Rwanda Paul Kagame
Matumizi
katika elimu, suala ambalo linachukuliwa kuwa kigezo muhimu cha
maendeleo limefikia juu ya asilimia sita ya pato la taifa nchini Afrika
Kusini, Ghana, Msumbiji na Tunisia, lakini Nigeria, taifa lenye idadi
kubwa zaidi ya watu barani humo, inatumia chini ya asilimia moja ya pato
lake la ndani katika elimu.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya
Dunia, mataifa ya Umoja wa Ulaya yanatumia wastani wa asilimia 4.9 ya
pato la taifa katika elimu kwa mwaka 2013.
Afrika ya Kati, ambako
viwango vya kuhitimu shule kwa wasichana ni vya chini katika bara zima,
pengo baina yao na wavulana linazidi kupungua. Idadi ya wasichana
waliomaliza sekondari kwa mwaka 2014 imefikia mara tatu zaidi tofauti na
muongo mmoja uliopita.
Usawa wa kijinsia umeongezeka katika
mataifa kadhaa yakiwemo Botswana, Namibia, Rwanda ambako wanawake
wanafikia viwango sawa vya maendeleo ya binadamu kama ilivyo kwa
wanaume, imesema ripoti hiyo.
Mkuu wa Benki ya maendeleo ya Afrika Akinwumi Ayodeji Adesina
Licha
ya hatua hizo, Waafrika milioni 544 wanaishi bado katika umaskini,
imesema ripoti hiyo iliyopewa kichwa cha habari "Muonekano wa Kiuchumi
wa Afrika mwaka 2017", ambapo bado changamoto nyingi zinasalia katika
mapambano ya vita dhidi ya umaskini. Moja kati ya hizo ni ukosefu wa
upatikanaji wa nishati ya kupikia, umeme na usafi wa mazingira. Watu
milioni 645 kusini mwa Jangwa la Sahara wanaishi bila ya umeme.
Ripoti
hiyo inasema kuwa mustakabali hauonekani kuwa mzuri kwa vijana wadogo
ambao wengi wao hawana ajira, kutokana na vijana hao kupatiwa elimu
isiyo na ujuzi sokoni.
Ripoti hiyo inatabiri kwamba yapo
matumaini ya ukuaji wa uchumi kwa asilimia 3.4 kwa mwaka huu, ikiwa ni
ongezeko baada ya kukua kwa asilimia 2.2 mwaka jana.
Afrika
Mashariki inasalia kuwa ukanda ulio na nguvu kiuchumi kwa bara lote
ikiongozwa na Ethiopia. Kwa ujumla Afrika iko nafasi ya pili katika
ukuaji duniani kote nyuma ya mataifa yanayoendelea ya Asia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: